Mbeya City, Simba ni visasi, ubora

Mbeya City, Simba ni visasi, ubora

Mbeya. Simba inashuka kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kuikabili Mbeya City, huku ikijivunia rekodi nzuri za msimu uliopita dhidi ya wapinzani wao.

Lakini licha ya rekodi za ushindi wa mechi mbili za msimu uliopita, miamba hiyo ya Mbeya ina msimu mzuri kutokana na kupoteza mchezo mmoja pekee msimu huu.

Mbeya City inayonolewa na Mathias Lulle inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, huku ikiwa na safu nzuri ya ushambuliaji iliyokuwa na mabao zaidi ya 10.

Safu ya ushambuliaji ya Mbeya City inaongozwa na Juma Luizio mwenye mabao manne, sawa na Richard Ngondya, huku Paul Nonga akiwa na matatu na Hamis Kanduru, Peter Mapunda na Siraji Juma wakiwa na moja moja.

Simba, ambayo imetoka katika shangwe za kutwaa taji la Mapinduzi, itakuwa na wakati mgumu mbele ya Mbeya City, lakini ikijivunia kiwango bora ilichokionyesha wakati wa mashindano ya Zanzibar.

Ujio wa kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama unaifanya Simba kujiamini zaidi katika ushambuliaji kutokana na mechi za kwanza kuonekana kupata shida kutengeneza nafasi.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema jana kuwa baada ya kumaliza kazi kwa kishindo kwenye Kombe la Mapinduzi, sasa wanageukia Ligi Kuu kuhakikisha wanaendelea ubabe akisema hakuna wanachotaka zaidi ya pointi tatu.

Kuhusu uwezekano wa Clatous Chama kuanza katika mechi ya kesho, Franco alisema nyota huyo ni muhimu na ndiyo maana klabu imeamua kumrejesha na ameona uwezo wake uwanjani na anaweza kusaidia kitu katika mchezo huo.

“Tunajua Mbeya City ni timu nzuri, lakini malengo yetu ni kushinda mchezo ili kujiweka pazuri katika kutetea ubingwa wetu, tutamkosa Thadeo Lwanga ambaye ameachwa Dar kwani ni mgonjwa,” alisema Franco.

Nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe alisema ubingwa wa kombe la Mapinduzi umeongeza nguvu kwa wachezaji na sasa wanageukia mchezo dhidi ya Mbeya City kuhakikisha wanashinda ili kuuanza vyema mwaka mpya kutetea upya taji lao la Ligi Kuu.

Nahodha wa Mbeya City, Paul Nonga alisema hawatarajii kurudia makosa kwani licha ya kutopoteza mchezo wowote uwanjani hapo, lakini matokeo mengi ilikuwa ni sare kuliko ushindi na kuwaomba mashabiki kujitokeza.