Mayele na Phiri washtua, Mgunda aombewa sapoti Simba

MBEYA. KASI waliyonayo Fiston Mayele wa Yanga na Moses Phiri wa Simba imemshtua staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mohamed Husein ‘Mmachinga’ akisema kuwa ushindani wao unazinufaisha timu zao, huku akimuombea sapoti Juma Mgunda.

Katika mechi za mkondo wa kwanza hatua ya awali, Mayele aliifungia Yanga mabao sita alipopiga hat-trick mbili kwenye mechi mbili mfululizo wakiizamisha Zalan FC ya nchini Sudan iliyonyooshwa jumla ya mabao 9-0 na kutupwa nje.

Kwa upande wa Phiri aliifungia Simba mabao matatu katika mechi mbili wakati Wekundu wakisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0 dhidi ya Nyassa Big Bullets ya nchini Malawi.

Kutokana na kasi hiyo, imemuamsha usingizini Mmachinga akieleza kuwa anaipa zaidi nafasi Yanga kufika mbali kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika kutokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na muunganiko uliopo kikosini.

“Kwa ujumla ni wachezaji wanaoonesha faida kwa timu zao, lakini naipa Yanga nafasi kubwa kufika mbali kutokana na muunganiko wa wachezaji, Simba wanaweza ila kuna mapungufu madogo madogo,” alisema Staa huyo mwenye rekodi zake bongo.

Nyota huyo aliongeza kuwa anachokifanya Kocha Mkuu wa muda wa Simba kwa sasa, Mgunda ni uhalisia na kuonesha wazawa wanaweza kufanya makubwa na kuwaomba mashabiki wa soka na mabosi wa Wekundu kumuamini.

“Kimsingi lazima aendelee kuaminiwa na kupewa sapoti, binafsi naona Mgunda anaweza kuwapa mafanikio makubwa Simba kwa sababu mwanzo wake tumeuona, hakuna anayeweza kubeza mafanikio ya haraka aliyowapa Simba,” alisema Mkali huyo wa mabao.