‘Mayay anastahili ukurugenzi’

BAADA ya Ally Mayay Tembele kuteuliwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, wadau mbalimbali wa michezo wamepongeza uteuzi huo huku wakiwa na matumaini makubwa na mchezaji huyo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa CDA ya Dodoma, Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ amepewa wadhifa huo akichukua nafasi ya Yusuph Singo aliyepangiwa majukumu mengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini, John Mapepele ilisema Mayay aliyekuwa Afisa Mwandamizi katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, amehamishiwa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na kuruhusiwa kukaimu majukumu hayo kwa mujibu wa kibali cha ofisi ya Rais Utumishi.

“Katika kuimarisha utendaji kwenye sekta ya Maendeleo ya Michezo nchini na kufuatia maelekezo ya waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa ya kufanya maboresho ili kuongeza tija, wizara inamtambulisha Ally mayay Tembele kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini wakati taratibu zingine zikiendelea,” ilifafanua taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema mkurugenzi wa awali, Yusuph Singo amepangiwa majukumu mengine huku ikiwataka wadau wa michezo kumpa ushirikiano Mayay.

Kuondolewa kwa Singo kunatimiza kauli ya Waziri Mchengerwa aliyotoa hivi karibuni kwa kutaka kufanyika kwa mabadiliko ya watendaji kwenye kurugenzi ya michezo ili kupata watu wenye sifa na kiu ya mafanikio, weledi, wachapakazi na wabunifu ili kuleta mabadiliko ya kweli kwenye sekta hiyo.


Wasikie wadau

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema; “Kwanza yeye mwenyewe ni mshirika mkubwa wa fani ya michezo hivyo naamini hakuna kitakachomsumbua, sasa labda aje kujiangusha mwenyewe lakini wengi wana matarajio makubwa naye kuendeleza michezo nchini. “Licha ya kwamba alikuwa mchezaji wa soka lakini naamini ataangalia kwa uzuri na ukaribu michezo yote kwa sababu ana upeo mkubwa, “alisema Mogella.

Naye mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garincha’ alisema; “Nimefurahi sana, tena naona kama wamechelewa kumpa hiyo nafasi, ana upeo mkubwa, ana sifa za uongozi hivyo najua ataitendea haki hiyo nafasi, nampongeza sana.

Bingwa wa zamani wa dunia wa riadha, Filbert Bayi alisema “Licha ya kwamba ametokea kwenye soka. Kikubwa asiyumbishwe ni siasa za kwenye michezo, binafsi namwona kama mkurugenzi wa michezo atakayekuwa tofauti na watangulizi wake.”

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya mpira wa kikapu, Bahati Mgunda alisema, “Kwanza nimpongeze, lakini naamini uelewa wake katika michezo utamuongoza kutoka hatua moja kwenda nyingine, wanamichezo naamini kwa umoja wetu tutampa ushirikiano wa kutosha.”

Mwenyekiti wa Judo, Zaid Hamis alisema, “Kikubwa atende haki, tunafahamu kila mmoja ana mchezo anaoupenda, Mayay amecheza soka na ana shauku na soka, lakini kwa kuwa sasa ni mkurugenzi wa michezo, basi asimame katikati kwenye michezo yote, uwezo anao,” alisema.

Akizungumza baada ya uteuzi huo, Mayay alisema “Kwangu ni kama sapraizi, bado sijapewa barua rasmi nimeona mtandaoni tu, nikipewa barua, nitakuwa na cha kuzungumza.”