Mayanga atoweka Prisons, anukia Mtibwa

KOCHA wa Prisons, Salum Mayanga ametimka ndani ya klabu hiyo huku taarifa zikidai muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kuwa kocha mpya wa Mtibwa Sugar.
Mayanga ameinoa Prisons tangu Agosti 14 mwaka jana akichukua mikoba ya Mohammed Adolph Rishard lakini pia aliwahi kuinoa timu hiyo msimu wa 2015/ 2016 na kuiwezesha kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi nyuma ya bingwa Yanga, mshindi wa pili, Azam na Simba iliyomaliza ya tatu.
Kocha huyo inadaiwa ameondoka ndani ya kikosi cha Prisons bila kutoa taarifa rasmi kwa uongozi hivyo kwa sasa timu hiyo inayojiandaa kucheza na Yanga Jumamosi iko chini ya kocha msaidizi Shabani Kazumba.
“Kocha ameshaondoka na kuna baadhi ya watu wachache tu ndio amewaambia kwani tangu tucheze na Polisi Tanzania ugenini (Desemba 4) hakuonekana tena na hajashiriki mazoezi ya timu na kumuachia majukumu kocha msaidizi,” alisema mmoja ya watu walio ndani ya timu hiyo.
Habari za ndani zinadai kuwa tayari Mayanga ameshamalizana na Mtibwa Sugar na wakati wowote ataonekana katika benchi la timu hiyo ambayo inadaiwa imevunja mkataba na kocha Mcameroon, Joseph Omog.
Alipoulizwa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakary kuhusu ujio wa Mayanga ndani ya timu hiyo alijibu bado suala hilo halijawa rasmi.
“Hakuna chochote kinachoendelea kuhusu suala hilo la ujio wa Mayanga labda hadi kesho (leo) kikao cha kamati ya utendaji kitakapokaa na kama jambo hilo litazungumzwa na kutolewa uamuzi basi tutatoa taarifa rasmi,” alisema Aboubakary.
Katibu wa Prisons, Ally Mrisho aliliambia gazeti hili kuwa bado wanajua Mayanga ni kocha wa timu hiyo na kama kutakuwa na lingine watatoa taarifa rasmi.
“Mayanga ni kocha wetu ingawa kama kuna timu inamtaka hatuwezi kumzuia ili mradi tu mambo ya kimkataba na kisheria yafuatwe,” alisema Mrisho.
Mayanga ana leseni ya ukocha ya daraja A inayotambuliwa na CAF na anatajwa kurejea Mtibwa ambayo aliinoa kwa vipindi tofauti tofauti na pia aliwahi kuichezea miaka ya nyuma.
Kama atarejea ndani ya timu hiyo itakuwa mara ya tatu kwani mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2008/09 na 2009/10 alipoiwezesha kutwaa Kombe la Tusker, Kombe la Mapinduzi na pia kutwaa Ngao ya Jamii.
Aidha, kabla ya kuwa mwalimu mkuu, Mayanga alikuwa kocha msaidizi wa klabu ya Mtibwa kwa kipindi kirefu chini ya makocha kadhaa wakiwemo Twahir Muhidin, Tom Olaba, James Sianga na Abdallah Kibadeni.