Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matola -7: Tulimvua taji Mwarabu kwa mbinu hizi

JANA tuliishia sehemu ambayo wachezaji wa Simba wamepewa hoteli yenye vurugu za kutosha, ilikuwa sehemu yenye fujo sana na ipo katikati ya jiji wakiwa wapo gorofa ya pili, lakini juu yao kuna ukumbi wa disco hivyo kelele ni nyingi na kubwa sana.

Lakini kumbuka huko nyuma tulishaona sehemu ambayo Selemani Matola alianzia soka lake na kupambana hadi kufikia kuwa mchezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Simba akiwa ameshaanza kuonja ladha ya makombe.

Tumeona hajacheza mechi ya kwanza Dar es Salaam kutokana na kuwa na majeraha ya kidole, kuna maswali mengi kama atacheza mchezo wa pili kwa kuwa aliyecheza mchezo wa kwanza alikuwa bora kweli kweli.
Je, nini kitafuata, Simba watahama hoteli au wataendelea kufanyiwa vituko? Tiririka nayo...!


MABOSI WAKUTANA, TIMU YAHAMISHWA
"Asubuhi tuliamka tukaenda zetu mazoezini lakini gumzo la kuwa tulilala sehemu ya hovyo na vicheko vya hapa na pale viliendelea wakati tukiwa kwenye gari na hata kule uwanjani.

"Kila mmoja alikuwa akizungumza lake, wengine wakiongea kuhusu zile picha tulizoziona kwenye televisheni, kumbuka kuwa kwenye ile hoteli hata viongozi nao walilala palepale kwa hiyo walikuwa wanafahamu nini kinaendelea.

"Tulipotoka mazoezini kama saa nne hivi asubuhi, tuliwakuta viongozi wamekaa mapokezi wakiwemo wale wadau wengine ambao tulikwenda nao wakiwemo akina Dau, wakatuambia hakuna kuvua nguo, tuingie vyumbani na kuchukua mabegi yetu tuondoke.

Matola anasita kidogo, anaomba tena maji, anapokea na kupiga fundo moja anacheka na kutoa neno la utani, dah! umeniweza sana, unajua mimi huwa siongei sana, sijui hata imekuwaje, lakini poa tuendelee...

Anaendelea kuzungumza: "Kweli tulitii na kila mchezaji akatoka na begi lake, watu wa pale hotelini walishangaa kwa kuwa kila kitu kilifanyika kwa muda mchache sana, lakini walishangaa kwa kuwa hoteli ile wenyeji wetu walishalipia, lakini viongozi hawakujali, tukatoka nje na kukuta gari tukapanda na kuhama hoteli ambapo tulipelekwe Apatimenti moja matata sana.

"Kule tulikuta vile vyakula ambavyo kina Kusaga walikuja navyo na tulikuwa tunapika chai wenyewe, tunakaanga mayai wenyewe kwa kuwa kulikuwa na majiko lakini ulipofika muda wa kwenda kula chakula cha mchana ulikuwa unafanyika umafia wa hali ya juu.
"Tulikuwa tunapanda kwenye magari tunaanza safari kama kilomita 50 hivi tunavamia hoteli tunakaa na kuangiza chakula, lakini viongozi wakiwa makini sana kukwepa hujuma zozote.
"Hata mazoezini tulikuwa tunakuta jamaa wameshatuletea juisi na maji, lakini tulikuwa hatutumii vitu vyao, tulikuwa tunavipokea na kugawa kwa mashabiki wetu, sisi tulikuwa tunatumia yale ambayo yalitoka Tanzania."


WAUNGANA NA MASHABIKI WA AL AHLY
Matola anasema siku moja kabla ya mechi yao, kulikuwa na mechi ya Kombe la Shirikisho ambapo Al Ahly walikuwa wanacheza siku hiyo, viongozi wakawaambia waondoke wote waende wakacheki mechi wakiwa na makocha wao.

"Tuliondoka, tulipofika uwanjani, tukaa upande wa Al Ahly, walifurahi sana, walituambia wanatamani kuona tunawatupa nje Zamalek, hapa kuna jambo la kujifunza, wakati jamaa wanatueleza hivi, walisema kabisa wanatuunga mkono lakini hawawezi kutushangilia hadharani kwa kuwa hawaruhusiwi kushagilia timu pinzani inayocheza na timu ya Misri, lakini wanatamani sana kutuona tunawatupa nje wapinzani wao.

Anasema anakumbuka kuwa Al Ahly walifanikiwa kushinda mchezo ule nao wakatoka vizuri kwenda hotelini kwao, lakini wakishangaa jinsi jamaa walivyokuwa mahiri kushangilia na mashabiki walikuwa wengi sana wote wakishangilia timu moja tu ya nyumbani kwao.


ZAMALEK NA UBINGWA WA FA

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, anasema pamoja na mambo mengine mengi ambayo yalitawala kwenye mchezo wao na Zamalek, lakini siku ya mchezo waliamka na kukuta magazeti yote ya Misri yamepamba picha za Zamalek yakionyesha kuwa hiyo ni siku yao.

"Unajua wale jamaa siku chache nyuma walikuwa wametwaa kombe moja kule kwao nafikiri ndiyo kama FA hapa, hivyo wakachagua siku ya mechi yetu nao ndiyo maalumu kwa ajili ya kukabidhiwa kombe lao kwa kuwa walifahamu moja kwa moja kuwa wanatufunga na hawakuwa na shaka hata kidogo, wakaalika na viongozi wao wa serikali kwa ajili ya sherehe.

"Siku hiyo mji mzima ulijaa rangi nyekundu tupu, lakini jambo la ajabu ni kwamba tulijiamini sana, tuliamini hawawezi kutufunga, tulikuwa na uwezo mkubwa sana, uwepo wa Talib pia ulitusaidia kwa kuwa alikuwa amegundua sana saikolojia ya wachezaji kuna wakati alikuwa anazungumza na mchezaji mmojammoja kumweka sawa.

"Fanya mambo yote kuhusu Simba, lakini hawa Friends kina Mo Dewji, Try Again kina Mulam, walifanikiwa kufanya kazi kubwa sana, walitumia nguvu yao yote kuhakikisha kuwa timu inapata ushindi kwenye ule mchezo walikuwa na vikao kila mara, kila dakika walitamani kutuona tukiwa tunajiamini, jambo moja ambalo walikuwa wanasema kila mara ni tunawachapa hapahapa kwao.


AKABIDHIWA ESSAM ABDEL-AZIM
Matola anapokea simu na kuongea na mtu kwa dakika mbili, wanacheka na kukumbushana masuala ya kwenda chuoni kesho yake, si unajua kuwa jamaa anasoma lugha na kompyuta jijini Dar es Salaam, anakata siku na kuuliza tuliishia wapi? namwambia, anaendelea.

"Wakati tunafanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo huu, kuna wakati Talib na Siang'a walikuwa wananipa mazoezi mengine magumu sana mwenyewe au na wakati mwingine walikuwa wananitaka kujiamini zaidi, siku ya mechi ilipofika kila mtu aliitwa na makocha kwa wakati wake akapewa majukumu yake, mimi nilipoitwa nilionyesha video za mshambuliaji wa Zamalek anaitwa Essam, jina la pili nimesahau, nikaambiwa nitembee naye kokote, kazi yangu kubwa ni kunyima utulivu, nilipewa maelekezo ya jinsi anavyocheza.

"Jamaa alikuwa ndiye staa wao, hakuwa mkubwa sana lakini alishatengeneza jina sana kwenye timu hiyo, alikuwa anajua chenga, anajua kufunga na mwepesi kwelikweli, makocha Talib na Siang'a wakanipeleka namba nane kwenye mechi hiyo ili niweze kutembea vizuri na jamaa na namba sita akapangwa Christopher Alex.


BARABARA NYEUEPE
"Tulichukukuliwa na msafara hapo hotelini, viongozi wetu walikuwa wamejiandaa sana hakukuwa na masihara hata kidogo kila mmoja alikuwa anatimiza majukumu yake ipasavyo, kabla hatujaenda uwanjani wengi walishafika hapo na kugundua kila kitu kilichokuwa kinaendelea.

"Wakati tunaanza safari tulikuwa na hofu labda tutakutana na foleni, lakini huwezi kuamini hakukuwa na magari mengi njiani, tulienda kwa mwendo wa kawaida lakini kila mtu nje alikuwa anatuangalia sisi, tukiwa kwenye gari,  tuliingia uwanjani na kukuta mashabiki wamejaa hadi wengine wamezuiwa nje.

"Kumbuka kulikuwa na hiyo mechi, lakini walikuwa na sherehe yao ya kukabidhiwa kombe, pia walikuwa ndiyo mabingwa wa Ligi ya Mabingwa mara mbili, hivyo walikuwa wamejiandaa kwelikweli na mashabiki walikuwa na vibu la hatari.

"Tulipoingia walizomea uwanja mzima, kumbuka kwao hauruhusiwi kushangilia wapinzani kwa wakati huo, hivyo wote waliungana ingawa wale wa Al Ahly walishangilia kinafiki wakitaka tushinde ili wakachekee uani.