Prime
'Mandonga hata kila siku freshi'

LICHA ya wadau wa ndondi nchini kushangazwa na bondia Karim ‘Mandonga’ Said kupigana mfululizo, Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), imesema bondia huyo yuko sahihi.
Mandonga ndani ya siku 35, amezichapa mapambano manne huku matatu akizichapa kila baada ya siku saba na kupigwa mfululizo mawili likiwamo la Moses Golola la Jumamosi iliyopita jijini Mwanza.
Golola ambaye hakuwa kwenye ndondi alimchapa kwa TKO, Mandonga ambaye wiki moja kabla ya pambano hilo alitoka kuchapwa kwa pointi nchini Kenya na Daniel Wanyonyi.
Bondia huyo, Juni 24, alitoka sare na Charles Misanjo baada ya kumaliza raundi nane huku pambano jingine akicheza Julai 15 na Mussa Omary.
Kucheza mfululizo kwa Mandonga kuliwashtua wadau wengi wa ndondi nchini akiwamo bondia nyota wa zamani, Ally Bakari Champion ambaye sasa ni mwamuzi na kocha wa ndondi.
Champion alisema pamoja na kwamba muda wa mabondia kucheza kati ya pambano na pambano haupo kikanuni, lakini alitoa ushauri kwa viongozi wa TPBRC na kamati yake ya afya sanjari na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Mandonga na bondia mwingine aliyemtaja kwa jina la Abdallah Luaga kupumzishwa kupigana kwa muda.
“Huenda hawana ufahamu halisi ya madhara yanayompata bondia anayetikiswa ubongo kwa kugongwa kichwa kila mara na kitu kizito mithili ya ngumi bila kupata kupumzishwa,” alisema Champion.
Kauli ya Champion inakolezwa na utaalamu wa mmoja wa madaktari nchini ambaye alisema bondia anapopigwa kichwani mara kwa mara nirahisi kupata ugonjwa wa kitetemeka na kushauri wawe na desturi ya kupima afya kabla na baada ya pambano.
Hata hivyo, Rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa alisema; “Hakuna tatizo kucheza mfululizo, mbona wapo mabondia wanafanya sparing kila siku, bondia mwenyewe akiwa fiti na daktari akiridhia apigane anacheza wala hakuna tatizo.” Hata hivyo, Champion ambaye aliwahi kushiriki semina ya utabibu kwenye masumbwi, alisema madhara ya bondia kupigwa kichwani mara kwa mara bila ya mapumziko madhara yake ni makubwa.
“Hayaonekani sasa kwa macho ya kawaida baada ya muda yatajitokeza, taratibu zipo wazi kwa wale waliocheza ngumi unapopigwa TKO unatakiwa upumzike miezi miwili kulingana ulivyopigana piga nikupige.
“Ukipigwa KO unahitajika mapumziko takribani miezi mitatu na zaidi kulingana na kipigo ulichopokea, ingawa unaweza kupigwa TKO hata wiki mbili ukacheza lakini sio kwa hili la Mandonga,” alisema.
Alisema hata Kamati ya ufundi ya TPBRC ilipaswa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa bondia huyo na wenzake. “Siku ya kupima uzito alizidi kilo kumi, ni sheria ipi iliyotumika kuruhusiwa kucheza kwa kilo hizo? alipewa masaa mangapi kuweza kupunguza kilo? tusiangalie pesa.”