Makambo amerudi, Yanga ileee!

AMEANZA. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya straika Heritier Makambo kuanza kikosi cha kwanza katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kupiga hat trick na kuivusha Yanga mbele ya Ihefu SC ya Mbeya waliyoifumua mabao 4-0.
Hat trick hiyo ilikuwa ya tatu kwenye michuano hiyo, baada ya awali Boban Zirintusa wa Mtibwa Sugar na Iddi Kipagwile wa KMC kufunga kwenye mechi ya mapema wakati timu zao zikigawa dozi kwa Tunduma United na Majimaji Songea.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, kocha wa Yanga Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko madogo kulingana na kikosi kilichovaana na Simba wikiendi iliyopita na vinara hao wa Ligi Kuu waliendelea kuonyesha soka tamu la pasi nyingi.
Makambo aliyeanzishwa katika Namba 9 katika siku ambayo straika ambaye huanzishwa, Fiston Mayele, aliachwa jukwaani, alifunga bao la kwanza kwa kichwa katika dakika ya sita akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Saido kabla ya kuongeza jingine dakika ya 23 akisukumia mpira wavuni katika lango tupu akimalizia krosi kali ya chini kutoka kwa Djuma Shaban.
Sekunde chache kabla ya mapumziko Khalid Aucho alitupia kambani bao la tatu akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Ihefu, Isihaka Luhamba baada ya mfungaji huo kuupiga kichwa akiimalizia krosi tamu ya Djuma iliyoanzia kwenye mfululizo wa pasi nyingi za kupasua mapafu wapinzani.
Licha ya kufungwa, Ihefu ilionyesha soka tamu na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo zilikuwa ikiishia miguuni mwa mabeki ama kutoka nje na mipira michache iliishia mikononi mwa Diarra Djigui. Katika kipindi hicho cha kwanza Ihefu ilizidiwa na Yanga kwani walimiliki mpira kwa asilimia 19 dhidi ya 81 ya Yanga ikiwa pia haijapiga shuti lolote lililolega lango ya Yanga.
Kipindi pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji, yaliyoinufaisha zaidi Yanga kwa kuandika bao la nne lililowekwa kimiani na Makambo likiwa la tatu kwake kwenye mchezo huo uliochezeshwa vyema na mwamuzi Ahmed Aragije wa Manyara. Bao hilo lilifungwa dakika ya 65 kwa kichwa akimalizia krosi tamu ya Farid Mussa.
Upande wa Ihefu, nyota wake waliitumia mipira mirefu kutengeneza mashambulizi, lakini mipira yao ilinaswa kirahisi na viungo wa Yanga ambapo Mauya na Aucho walionekana kucheza kwa maelewano wakipigwa tafu na Mwamnyeto na Bangala aliyekuwa akipanda hadi mbele. Ushindi huo wa Yanga umeifanya Yanga kuzifuata timu nyingine za Ligi Kuu zilizofuzu raundi ya nne, ikiwamo Simba, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Geita Gold, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons, Coastal Union, KMC, Mbeya Kwanza, Namungo, Ruvu Shooting, huku Mbeya City iking’olewa na African Sports.