Kwa ukuta huu Simba, Yanga sijui!

SAFU za ulinzi na ushambuliaji za Simba na Yanga kwa kiasi kikubwa zimeshikilia hatima ya kila upande katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo utakaochezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Upande ambao safu yake ya ushambuliaji itatumia vyema uimara wake na udhaifu wa safu ya ulinzi ya timu pinzani utakuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo utakaochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha na kinyume chake unaweza kujikuta unapoteza mchezo.

Simba ambao ni wenyeji wa mchezo huo, safu yake ya ulinzi hasa mabeki wa kati imekuwa na udhaifu wa kupata wakati mgumu wa kukabiliana na washambuliaji wenye kasi, chenga na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.

Ingawa ndio timu ambayo haijaruhusu idadi kubwa ya mabao msimu huu katika Ligi Kuu, nyakati kadhaa mabeki wake wamekuwa wakifanya makosa yanayojirudia mbele ya washambuliaji wenye kasi na chenga ingawa bahati nzuri kwao, mara nyingi huwa hawaadhibiwi nayo.

Safu hiyo ya ulinzi ya Simba inaundwa na kipa Aishi Manula na mabeki Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Pascal Wawa na Joash Onyango.

Lakini ukiondoa hilo, Simba imekuwa ikisumbuliwa na mipira ya juu inayotokea pembeni hasa ya krosi na kona na kati ya mabao 10 iliyofungwa, nane yalitokana na aina hiyo ya mipira au mabeki wake kuzidiwa kasi na chenga za wapinzani.

Uwepo wa wachezaji wa safu ya ushambuliaji ya Yanga ambao wana kasi, uwezo wa kumiliki mpira, chenga na kupiga mipira ya kona na krosi kama Saido Ntibazonkiza, Songne Yacouba, Tuisila Kisinda na Carlos Carlinhos unaweza kuiweka matatani safu ya ulinzi ya Simba ikiwa itashindwa kufanyia kazi udhaifu ilionao.

Ikumbukwe katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, bao la Yanga lilitokana na mkwaju wa penati ambayo ilitolewa baada ya beki Joash Onyango kumfanyia madhambi Tuisila Kisinda ambaye alimzidi kasi.

Wakati Simba ikiwa na changamoto hizo kwenye safu yake ya ulinzi, ukuta wa Yanga nao una kasoro zake ambazo kama wakishindwa kuzirekebisha kabla ya mchezo huo na watani wao wakazitumia vyema, mambo yanaweza kuwa magumu kwa upande wao.

Uelewano baina ya walinzi wa Yanga hasa wale wanaocheza nafasi ya beki wa kati na kipa umekuwa duni na hiyo kwa kiasi kubwa imetokena na mabadiliko ya mara kwa mara ambayo benchi la ufundi la timu hiyo limekuwa likiyafanya lakini pia makipa wake Metacha Mnata na Farouk Shikhalo wamekuwa na muendelezo wa kufanya makosa binafsi ambayo huwa yanaigharimu timu.

Shikhalo ameonekana kuwa na makosa ya kushindwa kumudu mashuti ya nje ya eneo la hatari wakati Metacha amekuwa akisumbuliwa na mipira ya krosi na kona na hivyo mara kadhaa kuruhusu mabao ya namna hiyo.

Ukiondoa hilo, matumizi ya nguvu na rafu za mara kwa mara ambazo baadhi ya wachezaji wa safu ya ulinzi ya Yanga wamekuwa navyo pindi wakutanapo na washambuliaji wasumbufu na viungo wabunifu na wenye uwezo wa kumiliki mpira, chenga na kasi, vinaweza kuzaa faulo zinazoweza kuwagharimu katika mechi hiyo.

Simba ina kundi kubwa la washambuliaji na viungo wenye uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira, wabunifu, kasi, chenga na wenye uwezo wa kufanya uamuzi wa haraka wawapo na mpira kama Clatous Chama, Rally Bwalya, Bernard Morrison, Luis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu, ambao wamekuwa chauchu ya timu hiyo kupata matokeo mazuri katika mechi mbalimbali.

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema kuwa Simba wanaonekana kuwa imara zaidi katika ushambuliaji, ingawa katika safu ya ulinzi hawana utofauti mkubwa na Yanga.

“Simba ina safu ya ushambuliaji bora muda wote na wanalisakama lango la wapinzani wao, Yanga wana safu nzuri lakini inalingana na falsafa ya mwalimu katika mchezo husika.

“Yanga naona kadri siku zinavyozidi kwenda mbele wanaimarika katika nafasi ya beki kama ilivyo kwa Simba. Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anakuja vizuri na anaweza kikwazo katika mchezo huo kwa washambuliaji wa Simba,” alisema Pawasa.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Herry Morris alisema kuwa kwenye ushambuliaji Simba wako vizuri kuliko Yanga ingawa safu yao ya ulinzi inaweza kuwaangusha.

“Simba wana viungo wazuri ambao wanatengeneza nafasi nyingi sana halafu washambuliaji wake huwa wanazitumia, Yanga wao wanatengeneza nafasi nyingi lakini katika umaliziaji ndio changamoto.

“Kwa Yanga, kiwango cha Ninja kwa sasa kinawapa matumaini watu wengi kwenye eneo la kati kwani ndio palikuwa panaonekana kuna shida. Simba wapo vizuri pia lakini beki zao za kati hazina spidi, ukipata mtu mwenye spidi lazima wapate tabu lakini kama ukicheza nao kwa pasi pasi huwezi kuwapita wapo vizuri sana,” alisema Morris.