Kibu kuliamsha kama kawa

ULILIANGALIA pambano la Ligi Kuu Bara lililopigwa juzi kati ya Simba na Mbeya City na ulimuona namna Kibu Denis alivyocheza? Bila shaka ulimuona jamaa alivyoshindwa kuonyesha makali mbele ya matajiri wake wa zamani kabla ya kutolewa.
Hata hivyo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola aliliambia Mwanaspoti licha ya Kibu kukutwa na hali hiyo,lakini ataendelea kumtumia kwani, makosa aliyoyafanya uwanjani ni ya kimpira na huwa yanamtokea yeyote.
“Kama kocha nafurahi kuona timu inatengeneza nafasi, lakini naumia pale wachezaji wanaposhindwa kuzitumia vyema nafasi hizo. Kibu mara nyingi amekuwa akishindwa kutumia vyema nafasi, ila sio kama ni mchezaji mbaya kwani hata ukiangalia yupo kwenye listi ya vinara wa mabao kikosini kwetu,” alisema Matola na kuongeza;
“Nitaendelea kumuelekeza namna ya kufanya tukiwa mazoezini pia nitampa mechi ili kuwa bora zaidi kwani ni mchezaji mzuri na anapambana kuhakikisha anatimiza maelekezo na malengo ya timu kwa ujumla.”
Kibu alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea Mbeya City na hadi sasa amefunga mabao saba kwenye ligi ya msimu huu inayokwenda kumalizika mwishoni mwa mwezi huu. Simba tayari imeanza kusuka kikosi kipya na huenda ikapiga chini sura nyingi maarufu ingawa Kibu si mmoja wapo.