Frank Domayo ilikuwa ndiyo basi tena uwanjani!

Muktasari:
Upasuaji huo kwenye mguu wa kushoto umefanyika katika Hospitali ya Vincent Palloti ya nchini humo na amepewa masharti ya kutokunja goti kwa muda wa wiki sita. Ataanza mazoezi ya soka Januari mwakani baada kukaa nje kwa miezi sita.
KIUNGO mpya wa Azam FC, Frank Domayo, amefanyiwa upasuaji wa paja juzi Jumanne nchini Afrika Kusini na kama matibabu hayo yasingefanyika ingekuwa ndiyo basi tena kucheza soka.
Upasuaji huo kwenye mguu wa kushoto umefanyika katika Hospitali ya Vincent Palloti ya nchini humo na amepewa masharti ya kutokunja goti kwa muda wa wiki sita. Ataanza mazoezi ya soka Januari mwakani baada kukaa nje kwa miezi sita.
Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alisema: “Tatizo la Domayo kama lisingefanyiwa matibabu hayo mapema, huenda ndiyo ingekuwa basi tena kulingana na ripoti ya Daktari.”
Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa, alisema: “Domayo aliumia miaka miwili iliyopita, amechanika msuli wa paja la kushoto, ni tatizo linaloitwa ‘Rectus Femoris’.
“Huyu aliumia akiwa na timu ya Taifa kule Namboole, Uganda kwenye mechi ya Taifa Stars na Uganda, aliumia dakika ya nne. Tatizo hilo lilikuwa linaendelea kukua kadiri ya siku zilivyokwenda huku akipatiwa matibabu madogo madogo na kutokana na uhodari wake uwanjani wa kufanya vizuri, aliendelea kutumika akiwa na maumivu hivyo hivyo.”
Daktari wa Yanga, Juma Sufian, naye alisema: “Ni kweli Domayo alikuwa na tatizo hilo, lakini alikuwa akipatiwa matibabu. Unajua matibabu yapo ya aina nyingi, si lazima upasuaji.”
Daktari wa Yanga wa zamani, Nassor Matuzya, alisema: “Ni kweli Domayo alikuwa na tatizo la msuli, lakini halikuwa la kiasi kikubwa cha kufanyiwa upasuaji.” Domayo anatarajiwa kurejea nchini Jumapili.