Farid Mussa kumfuata Samatta England

MILTON Keynes Dons ya Ligi Daraja la Pili England inatajwa kuwa miongoni mwa klabu zenye mpango wa kumsajili winga wa Kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa ambaye mkatabaka wake wa kuichezea CD Tenerife ya Hispania, unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu wa 2019/20.
The Dons ambao imekuwa ikishiriki Kombe la FA, inadaiwa kuwa na mpango wa kumsajili winga huyo wa zamani wa Azam FC baada ya jina lake kupendekezwa kwa mkuu wa kitengo cha utafutaji vipaji, Jon Goodman.
MK Dons iliyopo nafasi ya 18 kati ya timu 23 za Ligi Daraja la Pili, kwa sasa iko katika mchakato wa kukijenga kikosi chake kinachonolewa na Russell Martin ili kuhakikisha kinapanda daraja kwa misimu ijayo.
Martin yupo katika wakati mgumu kwa sasa kutokana na udogo wa bajeti wa klabu hiyo, hivyo inawabidi maskauti wa klabu hiyo kutumia nguvu kubwa kutafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa kutoka katika timu za madaraja ya chini.
Tangu ajiunge na CD Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza, Farid hajawa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na badala yake amekuwa akichezea kikosi B ambacho kimekuwa kikishiriki Ligi Daraja la Tatu Hispania ‘Tercera’.
Kabla ya kufunguliwa dirisha la usajili la Januari, Farid alikaririwa akisema, “Kuna klabu nyingi ambazo zimeonyesha kunihitaji, zilivutiwa na mimi wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika, najiona kuwa na uhitaji wa kubadilisha mazingira.”
Lakini baada ya kufunguliwa kwa dirisha hilo, uhamisho wa Farid ulishindikana na hakutaka kuziweka wazi klabu hizo, ikiwamo Milton Keynes, tuliyoibaini na yote hiyo, imetokana na ukaribu wa kibiashara uliopo kati ya klabu hiyo na wasimamizi wake.
Farid yupo chini ya wakala John Sorzano ambaye pia kwa hapa Tanzania, anawasimamia, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu wote wa Simba.
Sorzano ana uhusiano mzuri wa kikazi na Milton Keynes ambayo ilianzishwa 2004. Ben Reeves ambaye ni kiungo anayeichezea klabu hiyo ni mchezaji wa wakala huyo.
Mbali na Sánchez mchezaji mwingine anayesimamiwa na Sorzano ni Gonzalo Sánchez wa Club Alianza Lima, Peru.
KOKOTE FRESHI
Wengi tumezoea kumuona akicheza kama winga au namba 10 pindi alipokuwa akicheza Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Azam na hata akiwa katika majukumu ya Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Kwa sasa Farid ana uwezo mzuri wa kucheza kama beki wa kushoto, amekuwa akitumika katika nafasi hiyo akiwa na kikosi cha vijana cha CD Tenerife licha ya kuwa kiasili ni winga.
Kama atafanikiwa kwenda England, Farid atakuwa amefuata nyayo za Mbwana Samatta anayekipiga Aston Villa EPL.