Enekia awania ufungaji bora Ligi Kuu Morocco

KAMA utani vile, mchezaji wa kike wa Tanzania, Enekia Lunyamila anayeichezea Ausfaz amekuwa miongoni mwa washambuliaji wanaowania kiatu cha ufungaji bora kwenye Ligi Kuu ya wanawake huko Morocco ‘Professional Women’s Football Championship’.
Kabla ya michezo ya wikiendi iliyopita kuchezwa, Enekia alikuwa akishika nafasi ya pili kwenye orodha hiyo akiwa na mabao 12 nyuma ya Diarra Agueissa (14) wa Amlff kwa tofauti ya mabao mawili.
Wakiwa kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa jana ambao Ausfaz walicheza dhidi ya timu ya ANCS ambayo anaichezea Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Enekia alionyesha kuwa na njaa ya kuwa mfungaji bora kwa kusema ni kitu ambacho kwake kinawezekana.
“Mpinzani wangu kwenye vita ya ufungaji alicheza Jumamosi na hakufunga bao lolote maana walifungwa mabao saba, na ukiangalia tofauti na mabao iliyopo kati yetu ni ndogo sana, kama nitaendelea kuwa fiti naweza kuwa mfungaji bora,” alisema.
Enekia ana wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo, takwimu hizo zinambeba na kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi kwenye ligi hiyo.
Kiwango cha Enekia kimeanza kuzua hofu huko Morocco kwa viongozi wa klabu yake ya Ausfaz kuwa huenda wakampoteza mshambuliaji huyo kwani zipo tetesi kuwa ameanza kumezewa mate na vigogo mbalimbali ligi hiyo, ikiwemo ASFAR.
Zipo pia taarifa kuwa Enekia ana ofa ya kwenda kucheza soka la kulipwa Finland hiyo ni kwa mujibu wa wasimamizi wake, ambao wamepokea ofa hiyo.