Bilionea Yanga amjibu Mo Dewji

Monday August 02 2021
bilionea pic
By Mwandishi Wetu

NI kama vile Yanga imeamua kuijibu Simba kwa vitendo siku chache baada ya Mwenyekiti wa Bodi wa klabu hiyo ya Msimbazi, Mohammed ‘Mo’ Dewji kusema hataki timu yao ifananishwe na nyingine hukua kitamba msimu ujao wanataka kufanya makubwa zaidi.

Mabosi wa Jangwani kupitia bilionea wao, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ wameanza kufanya vurugu kubwa za usajili wa majembe ya maana, huku akitumia fedha zake kuzipiga kimtindo klabu mbili tofauti wakiwamo watani wao Simba na Waarabu wa Afrika Kaskazini.

Jeuri ya Ghalib ilianzia kwa staa wa kwanza Yanga kumleta nchini juzi, winga Jimmy Julio Ukonde kutoka Msumbiji, aliyekuwa kwenye rada za Simba ili kuanza mapema kumtafuta mbadala wa Luis Miquissone aliye mbioni kutua kwa wababe wa Afrika, Al Ahly ya Misri.

Alichofanya Ghalib ni kupiga hesabu za haraka na kumshusha nchini usiku mkubwa Ukonde akikumbuka alivyolizwa wakati akitaka kumsajili Luis misimu miwili iliyopita kabla ya kutua Simba.

Ukonde alikuwa akitakiwa na Simba kuja kuziba pengo la Miquissone pale Msimbazi na Wekundu hao walikuwa tayari kumtumia tiketi ili aje haraka jijini Dar es Salaam kumalizana naye.

Unaambiwa kama Ghalib angechelewa kidogo tu kumleta nchini Ukonde ambaye alikuwa ni kama pacha wa Luis walipokuwa pamoja UD Songo ya huko kwao Msumbiji, wote wakiwa hatari kwa matumizi ya mguu wa kushoto basi Yanga wangelia tena safari hii.

Advertisement

Tayari Ukonde ameungana na wenzake kambini ikielezwa atasainishwa mkataba wa miaka miwili kama ilivyo kwa mshambuliaji mwingine mpya aliyeshushwa na Yanga na jana kutambulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo, hapa tunamzungumzia Fiston Mayele.

Mayele, tayari amepewa jezi namba 9, wachezaji wengi wamekuwa wakiikacha kwamba ina gundu.

Advertisement