Adios Andres Iniesta Lujan, adios sana

Muktasari:
- Zidane alikuwa amesimama akimsubiri Andres Iniesta Lujan atoke na wachezaji wenzake wa Barcelona katika pambano la El Clasico Jumapili usiku. Alimkumbatia na kumuaga. Ilikuwa ni mechi ya mwisho kwa Iniesta Clasico.
ALISUBIRI, akasubiri, akaendelea kusubiri, na akasubiri sana. kwa dakika zaidi ya tano. Heshima iliyoje? Zinedine Yazid Zidane alikuwa amesimama katika sehemu ya kutokea wachezaji katika Uwanja Nou Camp uliojengwa mwaka 1957.
Zidane alikuwa amesimama akimsubiri Andres Iniesta Lujan atoke na wachezaji wenzake wa Barcelona katika pambano la El Clasico Jumapili usiku. Alimkumbatia na kumuaga. Ilikuwa ni mechi ya mwisho kwa Iniesta Clasico.
Alitangaza kuondoka wiki moja iliyopita huku akilia katika mkutano wa waandishi wa habari pale Nou Camp. Zidane alistahili kumsubiri Iniesta amkumbatie na amuage kwa heshima. Nimewahi kuandika hapa kwamba hauwezi kuwapata wachezaji wengi kama Iniesta katika zama hizi. Nalazimika kurudia tena.
Hawa mafundi ndio wanaishia. Hata Zidane anafahamu wachezaji wa aina yake, kama yeye, kama ilivyo Iniesta, hawaji sana. Wanapoondoka wanastahili kuheshimiwa. Sio kwamba Iniesta anastaafu soka, hapana, anaachana na mpira wa kiushindani uliompa heshima, anakwenda katika mpira wa biashara pale China au Japan.
Nyuma yake, Iniesta anakuwa kiungo wa mwishomwisho kabisa ambaye alifanya mambo yote mawili uwanjani. Alifanya mambo ya msingi na kando ya mambo hayo aliambatana na burudani. Alikuwa kiungo kamili.
Wakati Xavi Hernandez alikuwa fundi wa pasi nyingi, Iniesta alikuwa amekamilika zaidi kwa sababu angeweza kupiga pasi nyingi uwanjani na angeweza kukokota mpira na kupenya sehemu ambayo usingeweza kuamini.
Utawala wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ndio ambao ulifanya watu wasifahamu kwa undani zaidi ubora wa Iniesta. Utawala huu ndio ambao pia ulisababisha Iniesta asiwe Mwanasoka Bora wa Dunia, hasa kwa mwaka 2010.
Zidane na Ronaldinho walipata bahati ya kuwa viungo waliochaguliwa kuwa wanasoka bora wa dunia kwa nyakati mbalimbali. Moja kati ya sababu ni kwamba wafungaji wa zama zao hawakufunga mabao mengi kama Messi na Ronaldo.
Leo ubora wote wa Iniesta ulifunikwa na mabao ya Messi na Ronaldo. Wamefunga sana katika zama hizi kiasi kwamba kwa kiasi kikubwa tuzo zao zinatokana zaidi na mabao yao kuliko uhodari wao mwingine. Hapa ndipo lilipokuwa tatizo la msingi la Iniesta. Iniesta pia anaondoka katika soka la ushindani akikumbukwa kama mwanadamu mzuri. Nje ya kipaji chake ni mwanadamu mzuri. Wakati mwingine mambo haya mawili hayaendi sambamba sana. Wakati mwingine inakuwa ngumu kuwa na kipaji halafu bado ukawa mwanadamu mzuri. Unapokea shinikizo kubwa la kukufanya ujidai lakini haikuwa hivyo. Iniesta ni mmoja kati ya wachezaji wachache sana kuwahi kushangiliwa katika uwanja wa wapinzani wao wakuu katika soka la Hispania, Cornellà-El Prat unaotumiwa na Espanyol. Hawa ndio wapinzani wao wa jadi wa jiji moja.
Iniesta alionyesha fulana yake ya ndani iliyoandikwa ‘Dani Jarque siempre con nosotros’ ikimaanisha kwamba ‘Dani Jarque siku zote utakuwa nasi’. Dani Jarque alikuwa nahodha wa Espanyol ambaye alifariki kwa shambulio la moyo mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia.
Baada ya hapo Iniesta aliipeleka fulana hiyo katika klabu ya Espanyol ili iwekwe katika makumbusho yao. Utu wake uliwaingia mashabiki wa Espanyol na mpaka leo katika mechi hii ya watani wa jadi Iniesta huwa anashangiliwa. Huyo ndiye Iniesta.
Lakini pia Iniesta ni miongoni mwa wachezaji wachache kando ya Ronaldinho na Lionel Messi ambao wamewahi kushangiliwa na mashabiki wa wapinzani wao katika soka la Hispania, Real Madrid. Ilikuwa ni Novemba 2015.
Iniesta alionyesha soka la kiwango akafunga bao moja murua katika ushindi wa mabao 4-0 wa Barcelona ugenini. Wakati anatolewa mashabiki wa Madrid walishindwa kuvumilia. Walijikuta wakisimama na kupiga makofi kwa Iniesta. Jioni ile walikuwa wamekiona moja kati ya kipaji cha ajabu kuwahi kutokea.Huyu ndiye Iniesta katika sura nyingine.