MAONI: TFF isiruhusu tena aibu hii TPL

JUZI Agosti 16 usiku kulikuwa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kati ya Azam FC na Tabora United (zamani Kitayosce) ambao ulianza kuchezwa saa moja usiku katika Uwanja wa Azam Complex.

Lakini katika mazingira ya kutatanisha Tabora United iliingia uwanjani ikiwa na wachezaji wanane tu  badala ya kikosi kamili cha wachezaji 12.  Na ndani ya dakika 15, tayari ilishafungwa mabao 4-0 na wachezaji wake wawili wakaumia na mchezo ukaishia hapo kwasababu za kanuni za soka.

Kabla ya mchezo huo kulikuwa na kesi ilkiyoihusu timu hiyo kufungiwa na FIFA kufanya usajili mpya.

Na hata TFF asubuhi ya siku ya mchezo huo lilitoa taarifa kuhusu kuwepo kwa zuio hilo la Tabora United kutowachezesha wachezaji wapya waliokuwa wamesajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya kushiriki msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu.

Kutokana na zuio hilo, TFF haikufanya jambo lolote kunusuru aibu hiyo zaidi ya kuitaka timu hiyo yenye masikani yake Tabora kuwachezesha wachezaji wake wanane waliokuwa na timu hiyo tangu ilipokuwa ikishiriki Championship.

Tunasema TFF haikufanya lolote kunusuru mchezo huo kwasababu kama mzazi wa soka hapa nchini ingeweza kuuharisha na kuipa muda Tabora United kurekebisha kasoro zake baada ya kumalizana na  FIFA.

Kuna mifano mingi ambayo TFF na Bodi ya Ligi zilishirikiana kuahirisha michezo kutokana na sababu mbalimbali.

Mwaka 2021, Simba ilishindwa kucheza dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba ikiwa imeshafika jijini Bukoba kutokana na wachezaji wake kuumwa ugonjwa wa mafua. TFF ilikubali kuusogeza mbele mchezo huo.

Kama haitoshi mchezo mwingine wa Ligi Kuu wa Mei 8, 2021 kati ya Simba na Yanga uliokuwa ufanyike katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam nao ulisogezwa mbele baada ya kutokea mgongano wa muda kati ya saa 11 iliyopangwa awali na saa moja usiku iliyopangwa baadaye.

Kwanini TFF imeshindwa kuokoa hadhi ya Ligi Kuu ambayo tunajinasibu nayo kwa kudai inashika nafasi ya tano kwenye ubora barani Afrika? Katika hili lawama za kwanza lazima zitue TFF, itakuwaje kama mtu aliyekuwa akisubiri mchezo huo baada ya kulipia king’amuzi chake halafu anaona utumbo ule?

 Hivi TFF iliwafikiria wadhamini wa Ligi Kuu ambao walipaswa kuonekana kwenye runinga ya Azam kwa dakika 90?  Hawakuwaza baada ya aibu hii, Azam TV ambao nao ni wadhamini wa Ligi Kuu watakuwa na kipindi kingine cha kuonyesha kwenye runinga yao?

Waliwafikiria wale waliolipa ving’amuzi vyao kwa ajili ya mchezo huo na waliolipa viingilio vyao uwanjani? 

TFF ilifikiria kama aibu hii imevuka mipaka ya nchi kutokana na ubora wa ligi kushika nafasi ya tano barani Afrika iliyokuwa ikijivunia, isiziogope baadhi ya timu na kuamua tofauti na ikubali kutenda haki kwa heshima ya taifa.  Pamoja na uzembe wa viongozi wa Tabora United, ilitakiwa TFF isimame kama mzazi sio kufikiria kuikomoa zaidi timu hiyo.