Kitayosce yaanza Ligi kwa aibu

Dar es Salaam. Wageni wa Ligi Kuu Bara, Kitayosce kutoka Tabora jana ilianza ligi kwa aibu kwa kuingiza uwanjani wachezaji wanane tu katika mechi yao dhidi ya Azam FC iliyochezwa kwa dakika 15 kabla ya kuvunjwa kutokana na wachezaji wawili kujivunja wakati timu ikiwa imeshafungwa mabao 4-0.

Mechi hiyo ilipigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa ni tukio la kwanza kwa miaka ya karibuni kushuhudiwa timu ikiingia uwanjani ikiwa na idadi ya wachezaji kama hiyo kisha wawili kuanguka wenyewe na kutolewa na kwa mujibu wa kanuni 17 ibara 30 na 31.

Inaelezwa timu hiyo ni wachezaji hao wanane tu waliopata vibali na wengine kati ya 30 walionao kukwama, licha ya viongozi kupambana kutatua tatizo kutokana na hali iliyojitokeza kwa taarifa ya kufungiwa kusajili kutokana na kesi iliyopo Fifa ambayo hata hivyo adhabu hiyo ilifutwa jana mchana.

"Tulifungiwa kusajili ndio maana, lakini tulifanya mazoezi kama kawaida ya kujiandaa na mchezo huo, wachezaji wamepambana.Tulilazimika kuingia na wachezaji hao wanane, lakini hawakuwa fiti kwani, na wale waliokuwa tayari kwa mchezo walizuiwa ila nadhani viongozi wamepambana na mechi zijazo hili halitakuwepo tena," alisema kocha msaidizi wa timu hiyo Henry Mkanwa.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda alisema ibara ya 30 inasema timu inaweza kucheza ikiwa na wachezaji wasiozidi 11 na wasiopungua saba na ikiwa chini ya hapo mechi inamalizwa na timu iliyoshinda inapewa ushindi.

"Ibara ya 31 inasema ikitokea wachezaji wasiopungua saba, wakapungua mechi itavunjwa na timu iliyokamilika itapewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu, ila ikiwa imefunga zaidi ya mabao hayo yatabaki kama yalivyo na kwa vile Azam imeshinda 4-0, matokeo yanabaki hivyo hivyo," alisema Boimanda.

Licha ya Kitayosce kuonyesha wapo tayari kwa mchezaji, walijikuta wakipoteza kasi kutokana na kufungwa mabao manne ya haraka ndani ya dakika 13 tu, matatu yakiwekwa kimiani na nyota mpya wa Azam, Feisala Salum 'Fei Toto' aliyefunga mabao matatu na kuandika rekodi ya hat trick ya mapema katika misimu ya karibuni, huku jingine likifungwa na Prince Dube.

Fei Toto aliesajiliwa kutoka Yanga, alifunga mabao yake katika dakika ya 3,9 na 13, lingine lilifungwa na Prince Dube dakika ya tano.

Hata hivyo, dakika mbili baada ya Fei kukamilisha hat trick yake kipa wa timu hiyo aliumia hivyo hakukuwa na namna ya kuendelea baada ya kukosa mbadala wake.

Kabla ya kipa huyo kuumia wachezaji wa Kitayosce muda mwingi walionekana kufanya vikao kulingana na mchezo huo kuwalemea, huku wapinzani wao wakipata neema ya mabao.

Matokeo hayo ya jana yameifanya Azam ikae kileleni ikiishusha Mashujaa iliyoshinda mabao 2-0 mbele ya Kagera Sugar kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.