Kitayosce tatizo lilianzia hapa!

MASHABIKI wa soka wanajadili kile kilichojiri juzi usiku katika Uwanja wa Azam Complex, baada ya Kitayosce iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kufanya kituko cha mwaka kwa kushuka uwanjani na wachezaji wanane dhidi ya Azam kisha wawili ‘kujivunja’ na kuifanya mechi ivunjwe dakika ya 15.

Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuwa Tabora United, iliingia na wachezaji hao na kucheza dakika 15 tu kabla ya mchezo huo kuvunjwa ikiwa imeshafungwa mabao 4-0, nyota wa zamani wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akifunga ‘hat trick’ ya mapema zaidi katika ligi akitumia dakika 10 tu.

Fei alifunga bao la kwanza dakika ya tatu, ya tisa na 13, huku bao jingine likiwekwa kimiani na Prince Dube aliyefunga dakika ya tano ya mchezo huo kisha pambano kuvunjwa baada ya kusubiriwa kwa dakika 15 za kurejea kwa wachezaji wawili waliotolewa uwanjani kupatiwa matibabu.

Licha ya Kocha Msaidizi wa Kitayosce, Henry Mkanwa na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda kufafanua kilichojiri usiku ule, lakini maswali ni mengi kwa mashabiki kuanzia mtaani hadi kwenye mitandao ya kijamii lawama zikielekezwa kwa TFF/TPLB na Kitayosce kwa ujumla.

Hata hivyo, Mwanaspoti jana liliwasaka viongozi wa Kitayosce na wale wa Bodi pamoja na wadau kadhaa waliotoa ufafanuzi juu ya kilichosababisha aibu hiyo kwa Ligi Kuu inayotajwa kama ni ya tano barani Afrika kwa ubora, huku mabosi wa klabu hiyo wakikiri wamejifunza kutokana na makosa.


TATIZO NINI?

Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Thabit Kandoro alisema walipata ugumu na kuwa na presha baada ya kujua itawatumia wanane tu dhidi ya Azam na kukiri kuna makosa yamefanyika na kwa sasa wamejifunza na watafanya mambo mengine kwa umakini.

Kandoro alisema sakata lilianza kutokana na taarifa ya kufungiwa kusajili na Fifa baada ya kushtakiwa kwa kutomalizana na mchezaji aliyekuwa anawadai na kusema hilo lililokwamisha vibali vya kazi vya wachezaji tegemeo ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake mkoani Tabora.

“Unajua ingekuwa vigumu kulipia vibali wakati timu imefungiwa, ukichanganya na ugeni wa ligi mambo yanakuwa mengi hadi mechi hiyo inachezwa haikuwa rahisi nyuma ya pazia,” alisema na kuongeza;

“Presha ilikuwa kubwa sana kuanzia kwa viongozi hadi wachezaji, lakini ilibidi tupambane na mazingira magumu, kwani hatukuwa na namna ya kuliepuka hilo, hivyo ilitubidi  kuwapa moyo wachezaji ambao kati yao hawajamaliza wiki kufanya mazoezi na timu.

“Hakuna kitu kigumu mchezaji anaingia uwanjani ana presha kubwa, pamoja na hayo yote walifanya kazi yao walivyoweza, walicheza na Azam FC yenye wachezaji wazuri, hivyo walikabiliana na majukumu mazito.”

Alisema lilikuwa jambo gumu kwa makocha, lakini iliwabidi wawatumie wachezaji waliopo na kufafanua; “Makocha walikuwa na wakati mgumu kupanga mfumo, pamoja na hayo yote walionyesha ujasiri ndani ya muda ambao timu imecheza ilikuwa inajaribu kushambulia na kuzuia.”

Alisema mechi yao inayofuata dhidi ya Singida Fountain Gate kila kitu kitakuwa sawa na mchezo huo wanautarajia utakuwa na ushindani mkali.

Alipoulizwa juu ya ruksa ya kutumia wachezaji wa timu B alijibu kwa kifupi; “Tuna timu ya vijana na kikosi kizima cha B kilibaki Tabora, tulisafiri wachezaji 20 tu kuja Dar, wazawa wakiwa 10 na wageni 10, lakini hata hao wazawa mmoja aliumwa ghafla. Ni mambo mengi nadhani tuishie kukubali changamoto na imetufunza na siwezi kulizungumza sana hilo,” alisema Kandoro mkurugenzi wa mashindano wa zamani wa Yanga.


BODI YA LIGI

Ofisa Habari wa Bodi la Ligi, Karim Boimanda alieleza hoja ya kwamba kuruhisiwa kucheza mechi hiyo kisha kuvunjwa baada ya dakika 15 kama imechafua sifa ya ligi na kusema, Kitayosce ndio imechafua picha ya ligi hiyo, ila walichokifanya wao ni kusimamia kanuni na kuipa thamani zaidi.

“Timu hiyo kabla haijafungiwa juzi, Agosti 15 ilikuwa na mwezi mmoja na nusu tangu ipande, wakati huo ilikuwa imesajili wachezaji watano tu, ukiondoa watatu ambao leseni zao zilikuja uwanjani, mbaya zaidi hawakuwa na barua ya viongozi kuomba kuahirishwa kwa mchezo huo,” alisema Boimanda na kuongeza;

“Bodi la Ligi hatukuwa na kanuni ya kuiambia timu mwenyeji wa mchezo ambayo ni Azam kuwa tunaahirisha mchezo huo, wakati Kitayosce ilikuwa inataka kucheza na nikumbushe klabu za Ligi Kuu, leseni ni lazima sio jambo la huruma wala hekima kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaiokoa zaidi ligi yetu na si vinginevyo.

“Mfano kwa Kitayosce kuvunja kanuni hiyo TFF na Bodi la Ligi ingekuwa na uwezo wa kuiondoa timu hiyo Ligi Kuu kwa kukosa sifa, nasisitiza maamuzi ya mchezo kuchezwa yapo kwenye kanuni na haziwezi kuvunjwa, nadhani wanahabari wawaulize zaidi viongozi wa Tabora ndio wenye kujua walikosea wapi na sio bodi ambayo imefanya kinachotakiwa kufanyika.”


WASIKIE AZAM

Kulikuwa na hofu kwamba kuvunjwa kwa pambano hilo huenda kungewazingua mashabiki walioingia uwanjani kushuhudia mchezo huo, kama ambayo hofu huenda mashabiki wakawa wamedhulumiwa viingilio kwa mechi kuisha ndani ya muda mchache, lakini klabu ya Azam, inayomiliki Uwanja wa Azam Complex, imefafanua.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam, Zakaria Thabit ‘Zakazi’ alisema; “Tangu msimu uliopita mechi zote za nyumbani zikipigwa kwenye uwanja huu hatuweki viingilio, hivyo hakukuwa na tatizo lolote baada ya mchezo huo kuvunjika.

“Baada ya mchezo kuvunjika wachezaji waliocheza walifanya mazoezi kwa dakika  takribani 30 ambao hawakucheza kabisa walifanya kwa dakika 45 na alfariji ya leo timu inasafiri kwenda Ethiopia kwa ajili ya michuano ya CAF.”


RAGE  HUYU HAPA

Akizungumzia sakata hilo, mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Rage alisema, tatizo la mchezo huo liko kwa klabu yenyewe kushindwa kutafsiri na kujua vyema kanuni.

“Naziomba klabu ziheshimu kanuni, ndio maana TFF ilitangaza kabla ya Ngao ya Jamii na kuzitaja timu ambazo hazijakamilisha lakini nyingine ndio kama zilipuuza, usajili wa sasa unafanyika kwa njia ya mtandao watu wabadilike,” alisema Rage na kuwataka viongozi wa klabu kubadilika na wazisome kanuni.

“Mimi mwenyewe nilikuwa uwanjani sikuelewa kwa nini wameingia wachezaji wanane, nikawauliza wakaniambia usajili haujakamilisha hao wanane ndio tayari, nikawaambia wanitafute niwasadie mchezo ujao yasiwakute kama hayo.”

Aidha Rage ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Tabora Mjini alisema sakata hilo halina athari kwa soka letu kwa madai ya kuporomoka katika ubora wa ligi akidai ubora huo unaletwa na klabu hasa Simba na Yanga mashabiki wao ndio wamelibeba taifa kutokana na wingi wao uwanjani.