Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

#WC2018: Usishangae wasipocheza

Muktasari:

  • Ufaransa itakipiga na Uruguay mapema kabla ya Brazil kuvaana na Ubelgiji leo, huku kesho kutakuwa na mechi nyingine mbili, England itacheza na Sweden na Russia itakipiga na Croatia.

RAUNDI ya 16 bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 imeshapita na kusahaulika kabisa.
Kwa sasa habari zote ni kwenye mchakamchaka wa robo fainali, ambapo mechi zake zitapigwa leo Ijumaa na kesho Jumamosi.
Ufaransa itakipiga na Uruguay mapema kabla ya Brazil kuvaana na Ubelgiji leo, huku kesho kutakuwa na mechi nyingine mbili, England itacheza na Sweden na Russia itakipiga na Croatia.
Lakini katika kuelekea mechi hizo muhimu kabisa kuna masupastaa watano wanaweza kukosa, watatu kati yao ni hatihati kutokana na kuwa na majeraha, lakini wawili hawachezi kabisa kwa sababu ya kukabiliwa na adhabu iliyotokana na kuonyeshwa kadi mbili za njano.

5. Casemiro- Brazil
Huko kwenye kikosi cha Brazil, Kocha Tite anakuna kichwa kwa sasa kutafuta namna nzuri kabisa ya kuikabili Ubelgiji kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia 2018.
Shida inayomkabili Tite ni kiungo wake wa kukaba chaguo la kwanza, Casemiro hatakuwapo kwenye mechi hiyo. Kiungo huyo anayekipiga kwenye klabu ya Real Madrid anakabiliwa na adhabu baada ya kuonyesha kadi ya pili ya njano katika mechi ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mexico kwenye hatua ya 16 bora.
Jambo hilo linamfanya akose mechi hiyo ya leo Ijumaa dhidi ya wababe hao wa Ulaya. Jambo hilo linampa nafasi Fernadinho kuanzishwa kwenye mechi hiyo kwa sababu ndiye mtu anayefiti kwenye buti zake.

4. Blaise Matuidi- Ufaransa
Kocha Mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps atahitaji kuja na mpango mbadala kwa sababu kiungo wake mchapakazi Blaise Matuidi atakuwa na adhabu ya kufungiwa kucheza mechi ya robo fainali dhidi ya Uruguay itakayopigwa leo Ijumaa.
Kiungo huyo alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwenye mechi ya ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Argentina kwenye hatua ya 16 bora.
Kutokana na hilo, viungo sasa Corentin Tolisso na Stephen N’Zonzi ndiyo watakaokuwa na nafasi ya kuchezeshwa kwenye mechi hiyo kwa sababu Matuidi ana adhabu na hatacheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia huko Russia.

3.Jamie Vardy- England
Kocha wa England, Gareth Southgate alifichua kwanini Jamie Vardy hakupiga penalti kwenye mechi ya ushindi wa mikwaju 4-3 dhidi ya Colombia Jumanne iliyopita.  
Fowadi huyo wa Leicester City alipata maumivu ya misuli ya korodani wakati wa mchezo huo na sera ya kocha huyo ni kwamba mchezaji majeruhi haruhusiwi kupiga penalti.  Vardy ndiye mpigaji wa penalti zote za Leicester City.  Imeelezwa anaweza kuwekwa benchi kwenye mechi ya robo fainali dhidi ya Sweden itakayofanyika kesho Jumamosi labda kama tu atapona kwa haraka.
Kyle Walker na Ashley Young nao watafanyiwa uchunguzi kutambua ufiti wao kabla ya mechi hiyo.

2.Luis Suarez- Uruguay
Mashabiki wa Uruguay wapo kwenye presha kubwa juu ya mechi ya robo fainali dhidi ya Ufaransa itakayofanyika leo Ijumaa kutokana na orodha ya majeruhi ya wachezaji muhimu inayowaandama katika kikosi hicho. Luis Suarez ameumia mguu wake wa kulia mazoezini Jumanne iliyopita.  Straika huyo wa Barcelona alionekana akipatiwa matibabu kwa muda mrefu sana kwenye uwanja huo wa mazoezi kabla ya kuchukulia na kuondoka na hakurudi tena.
Uruguay kwa sasa jasho linawatoka kwa sababu patna wake wa uwanjani Suarez, Edinson Cavani naye ni majeruhi.

1.Edinson Cavani- Uruguay
Shujaa wa Uruguay kwenye mechi za raundi ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, Edinson Cavani yupo kwenye hatihati kubwa ya kuwapo kwenye mechi ya robo fainali itakayofanyika leo Ijumaa dhidi ya Ufaransa.  Straika huyo alifunga mabao mawili walipoitupa nje Ureno na kutinga hatua ya nane bora.
Lakini Cavani amepata maumivu ya misuli ya kigimbi na kushindwa kufanya mazoezi tangu Jumamosi.
Kocha Oscar Tabarez ana wasiwasi kama fowadi huyo wa PSG atakuwa fiti kiwango cha kutosha kuwakabili Les Bleus wikiendi hii.

Bonyeza HAPA kupakua jarida letu la Kombe la Dunia.