ZORAN: Yanga inafungika subirini muone

Saturday August 06 2022
Zoran PIC
By Thobias Sebastian

ZIMEBAKIA siku chache kabla ya kuchezwa mechi ya ufunguzi wa msimu kati ya Simba dhidi ya Yanga, ambayo itapigwa Agosti 13, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Kocha Zoran Manojlovic Maki akisema wala hana presha kabisa na pambano hilo la dabi.

 Simba ilikuwa kambini Misri kwa muda wa wiki tatu kufanya maandalizi wakati watani zao Yanga walibaki Dar es Salaam, Kigamboni Avic Town.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Kocha Zoran ambaye amefunguka mambo mengi, huku akiweka bayana anavyoujua ushindani uliopo baina ya timu hiyo ya Msimbazi dhidi ya Yanga na Azam FC, lakini akisisitiza yeye ni mtu wa mechi kubwa.

Kocha huyo pia alifunguka juu ya maandalizi ya msimu mpya na namna kambi ya Ismailia ilivyomsaidia kuweka mambo mengi kiufundi na anakuja kumalizia kazi jijini Dar es Salaam akianzia na Simba Day kisha Ngao ya Jamii akisisitiza licha ya Yanga kuonekana kali, lakini bado inafungika.

ENDELEA NAYE...


Advertisement

MAANDALIZI YA MSIMU

Kocha wa Simba, Zoran Maki amesema katika maandalizi hayo ya msimu ujao wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamefanya kazi nzuri kulingana na vile vitu vya kiufundi walivyohitaji.

Zoran anasema walikuwa na mwanzo mgumu kutokana na ugeni wake ndani ya timu, ugeni wa wachezaji pamoja na ratiba ngumu ya mazoezi, ila baada ya muda kila kitu kimeenda sawa.

Anasema wamefanikiwa kucheza mechi za kirafiki na kuonyesha mwanga kwa timu yao hasa kwenye mechi hizo na wameweka malengo ya kufanya vizuri msimu ujao.

“Viongozi wamefanya kazi yao vizuri kwa kuileta timu mahala salama na sahihi na hata wachezaji wamepokea kile ambacho nilikuwa nahitaji.”


WATANO

Zoran anasema kuna wachezaji watano ambao hawakuwepo kutokana na majukumu ya Timu ya Taifa. Kuna kitu huenda kimepungua kwao lakini anaamini kabla ya kucheza mechi za ya mashindano watakuwa sawa.

“Baada ya kumaliza maandalizi huku Misri tutaungana nao na tutakuwa na wiki moja ya kufanya nao maandalizi kabla ya kucheza mechi na Yanga,” anasema Zoran na kuongeza:

“Hadi mchezaji anaitwa kwenye Timu ya taifa naamini atakuwa na kitu fulani kwa maana hiyo tukiungana nao nitawaelekeza vile tulivyofanya huko na wataweza kuelewa kwa haraka kwani kocha wetu wa viungo aliwapa ratiba ya kufanya mazoezi hukohuko Tanzania.”

Wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha Stars ni Aishi Manula, Mohammed Hussein, Mzamiru Yassin, Kennedy Juma na Kibu Denis.

Katika hatua nyingine Zoran anasema kuna wachezaji wawili wapya wamechelewa kufika kambini nao ataungana nao Dar es Salaam na kuona hali yao ya utimamu wa mwili kama ataweza kuwatumia katika mechi na Yanga.


FALSAFA YAKE

Hapa Ismailia Mwanaspoti lilishuhudia Zoran akipenda soka la kasi, kushambulia kwa haraka, hataki mchezaji kutembea na kupoteza mpira kwa urahisi.

Zoran anasema anataka kuona Simba inabadilika na kucheza katika falsafa yake soka la kushambulia muda wote tena kwa haraka huku wakicheza mpira wa kuvutia.

Anasema katika aina ya soka ambalo analihitaji na kufundisha katika mazoezi huku Ismailia atakuwa anatumia mifumo ya 4-3-3 na 4-2-3-1 ingawa muda mwingine atakuwa akibadilika kulingana na mechi itakavyokuwa.

“Kuna mechi nyingine inaweza isiwe ngumu kutokana na wapinzani walivyo, kutokana na falsafa yangu siku hiyo naweza kuanza na kiungo mmoja tu wa ukabaji kwa maana ya 4-1-3-2, ili kuishi katika malengo ya kushambulia muda mwingi kwani ni miongoni mwa njia ya kujilinda,” anasema.

“Unajua Simba ni timu kubwa inahitaji kushinda mechi nyingi kwa hiyo kucheza kwa kujilinda zaidi ni hatari tutawapa wapinzani nafasi ya kuja langoni kwetu ndio maana nimebadilisha aina ya uchezaji.

Kundi la wachezaji niliokuwa nao wengi wanafiti katika kile ambacho nahitaji ingawa kuna wengine wachache tu naendelea kuwaelekeza na baada ya muda watabadilika kuwa sawa kama wenzao.”


YANGA INAFUNGIKA

Zoran anasema baada ya kumaliza maandalizi watarudi Tanzania watacheza mechi moja ya kirafiki kisha ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

“Malengo ya kwanza ni kuondoa rekodi mbaya ya kupoteza mechi ya ufunguzi wa msimu,” anasema Zoran na kuongeza:

“Bahati nzuri msimu huu tunafungua tena msimu kwa kucheza na wapinzani walewale tumedhamiria kushinda ili kuchukua taji la kwanza kama malengo yetu yalivyo msimu huu na baada ya hapo tutaanza kujipanga kwa ajili ya Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 17.

“Tumeafanya maandalizi ya kutosha dhidi ya Yanga. Nimeangalia baadhi ya mechi zao na kufahamu udhaifu wao na kuna vingine tunavifanyia kazi ili kuhakikisha tunashinda mechi hiyo ngumu moja ya dabi kubwa Afrika.

“Kuhusu Ligi ya Tanzania ni ngumu na tunatakiwa kuanza kwa nguvu ili kumaliza vizuri kwani hii ni kama marathoni, kuhusu Kombe la Shirikisho (ASFC) nalo tutaandaa mipango yake kulingana na mechi zitakavyokuwa ili kuhakikisha tunafika fainali na kulibeba kombe hilo.”


LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Kuhusu Ligi ya mabingwa Afrika ambayo Simba itaanzia hatua ya kwanza na kama ikishinda michezo miwili ya hapo nyumbani na ugenini itakwenda hatua ya makundi, Zoran anasema jambo la kwanza ni kuhakikisha timu inakwenda makundi na baada ya hapo kuandaa mpango mzuri kulingana na wapinzani wao kwenye kundi.

Anasema baada ya kuwaona wapinzani kwenye kundi hapo kutakuwa na mipango mizuri ya kwenda robo fainali kulingana na ubora wa timu ambazo watakutana nazo.

“Tunakwenda kushindana katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba ifike mbali zaidi pengine hatua ya nusu fainali ambayo kwa hivi karibuni bado hatujaifikia,” anasema Zoran.

“Malengo ya timu ni nusu fainali lakini kuna yale ya muda mrefu kutwaa taji hilo. Tutafanya maandalizi ya kutosha kuona hilo linawezekana.

“Kikosi changu kina wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kushindana katika mashindano haya na kuweka rekodi kubwa ya kufika mbali zaidi.”


WACHEZAJI WAPYA

Simba itakamilisha usajili msimu huu kwa kuleta mashine nyingine mbili mpya nchini ila kabla ya hapo ilikuwa imewatambulisha nyota wapya sita ambao wote wapo hapa kambini Ismalia.

Wachezaji wapya waliotambulishwa, Moses Phiri, Augustine Okrah, Habibu Kyombo, Victor Akpan, Nassoro Kapama wanaondelea na mazoezi na Mohamed Ouattara aliyeomba ruhusa kwa ajili ya mambo yake ya kifamilia.

Zoran anasema kuhusu wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho Phiri na Okrah wameonyesha ni wachezaji wazuri katika maandalizi haya hasa linapokuja suala la kushambulia wanaweza kufunga, wasumbufu kwa mabeki na wanaweza kutengeneza nafasi za kufunga.

“Kama Phiri na Okrah watakwenda kucheza hivi katika mashindano ni aina ya wachezaji hatari na kuchungwa muda wote wanapokuwa uwanjani.

“Outtara namfahamu vizuri ni beki mwenye uwezo wa hali ya juu tangu nikiwa naye Wydad Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan.

“Ouattara atakwenda kutoa ushindani wa kutosha kwa Joash Onyango na Inonga Henock wale ambao watakuwa imara nitawatumia kulingana na mechi husika.

“Akpan, Kapama na Kyombo kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akinivutia kutokana na uwezo wanaonyesha kwenye kila zoezi au jukumu ambalo nawapatia.”


KWA NINI SIMBA

Zoran anasema aliamua kufanya maamuzi ya kujiunga na Simba kuachana na ofa nyingine kutokana na malengo ya timu hii pamoja na kucheza Ligi ya mabingwa Afrika mara kwa mara.

Anasema amefundisha Angola, Casablanca, Al Hilal ya Sudan, Nigeria huko kote alicheza Ligi ya mabingwa Afrika na alifika hatua za mbali kwenye mashindano hayo kama nusu fainali.

“Hayo mawili yalichangia kufanya maamuzi ya kuja kuifundisha timu hii nikiamini nitaishia katika ndogo zangu na nitaifikisha katika malengo makubwa kama kwenye timu nyingine nilizopita huko nyuma,” anasema Zoran.

“Huenda watu hawafahamu Simba kwa sasa ni moja kati ya timu kubwa Afrika ambayo makocha na wachezaji wakubwa wanatamani kuja kufanya kazi hapa.”


YANGA NA AZAM

Zoran anasema anafahamu Tanzania kuna timu tatu kubwa na kuna ushindani mkali katika mashindano ya ndani.

“Hata katika nchi nyingine nilizofundisha ushindani ulikuwa ni mkali kwa baadhi ya timu mbili au tatu na nilifafanya vizuri naamini hata hapa Simba itakuwa hivyo,” anasema Zoran

“Awali nilikueleza malengo ya Simba ni hatua kwa hatua. Tunaanza na Ngao ya Jamii kisha ligi, ASFC na baada ya hapo Ligi ya Mabingwa Afrika na kote huko tumepanga kufanya vizuri.

“Kwa hiyo licha ya ushindani kati ya Yanga na Azam naamini msimu huu utakuwa bora kutokana na aina ya maandalizi yetu na timu jinsi ulivyo.”


KABLA YA TANZANIA

Zoran anasema kabla ya kuja Tanzania alifahamu vitu vingi ikiwemo soka la hapa kwani alishawahi kuja na Al Hilal katika Tamasha la Wiki ya Simba.

Anasema Ligi ya Tanzania imekuwa na ushindani mkali na kuimarika kwa kasi jambo ambalo litazidi kuvutia watu wengi kwenye maeneo mbalimbali kuja kufanya kazi na kuwekeza.

“Nafahamu kuna changamoto ya viwanja kuna maeneo si mazuri katika kuchezea ila tutaweka mipango na mbinu sahihi kwa wachezaji wangu ili kufahamu tunaingia na mbinu gani ili kuweza kupata ushindi huko.

“Katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ni wakubwa kuliko Yanga kwani kwa kipindi cha hivi karibuni wametinga robo fainali si chini ya mara mbili katika mashindano haya ya CAF.

“Nafahamu Watanzania wanapenda sana mpira. Najua huwa wanajaa kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi za kimataifa Simba ikicheza pamoja na kilele cha Wiki ya Simba kama hii inayofanyika Agosti 8 au zile za Yanga na Simba.”


BENCHI LA UFUNDI

Zoran anasema baada ya kukubaliana na mabosi wa Simba kuanza kazi amefurahishwa kupewa nafasi ya kuleta wasaidizi wake wawili ambao anawafahamu.

Zoran anasema Sbai mbali ya kuwa kocha wa viungo anaweza kazi ya usaidizi anaujua uelewa wake ni mkubwa katika soka na amefanya naye kazi katika kila nchi.

“Ndani ya siku hizi chache nitamleta kocha mwingine wa makipa kutoka Algeria ambaye nafahamiana naye kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa pamoja kama ilivyokuwa kwa Sbai.

“Uwepo wa wasaidizi hao pamoja na Selemani Matola ambaye ni mwenyeji wetu hapa tutakuwa na benchi la ufundi zuri na lenye kushauriana vizuri.

“Baada ya wachezaji wapya wawili kufika, kocha wa makipa timu itakuwa imekamilika kwa ajili ya kwenda kwenye mashindano yote msimu ujao.”


NAFASI ZA KUFUNGA

Msimu uliopita Simba ilikuwa ni miongoni mwa timu iliyokosa mabao mengi katika kila mechi huku ikiwa na wastani mzuri wa kutengeneza nafasi za kufunga.

Zoran anasema ameliona hilo alimeshalifanyia kazi katika mazoezi ili kulipatia ufumbuzi na kudai muda mwingine kufunga ni kipaji alichozaliwa nacho mchezaji au ubora wake uwanjani.

“Katika wachezaji hao wawili wapya kabla ya dirisha kufungwa Simba itasajili mshambuliaji mzuri mwenye uwezo wa kufunga ili kuongeza ubora wa kikosi chetu kwenye mashindano msimu ujao.

“Wakati huohuo nina nahodha, Bocco pamoja na Kyombo naimani watafanya vizuri. Kwenye ile mechi tuliyoshinda mabao sita, tulikosa nafasi nyingi za kufunga ndio maana tumeamua kufanya haya mawili naimani kila kitu kitabadilika katika hili.”


ITAENDELEA TENA KESHO

Advertisement