Zoran: Simba sasa imeiva, apitia mikanda ya Mayele

ZIKIWA zimebaki siku 10 kabla ya Simba na Yanga kukutana kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi wa Ngao ya Jamii, Agosti 13 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kocha wa Simba, Zoran Maki amekisuka kikosi chake, kisha akasema sasa kipo tayari kwa ajili ya mashindano.

Simba ambayo ipo mjini hapa ilipoweka kambi ya wiki tatu sasa, imekuwa ikijifua na kujiweka fiti katika mambo mbalimbali ya uwanjani ikiwamo utimamu wa miili.

Zoran amesema katika utimamu wa miili wachezaji wapo sawa na upande wa mbinu wamepokea vizuri maelekezo na kwamba, ameliona hilo hata katika mechi nne za kirafiki walizocheza na kama kuna marekebisho machache, basi ni yale madogo ambayo watayajenga wakiwa Dar.

Amesema kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kuhakikisha wachezaji wanaonyesha mchezo bora katika kilele cha Siku ya Simba (Simba Day), Jumatatu ijayo, kwani mbali ya kushinda anataka kuwaona mastaa hao wanacheza soka la kuvutia na la haraka muda wote.

“Baada ya hapo tutakuwa na siku chache kufanya maandalizi mengine kabla ya kucheza mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Yanga na jinsi ambavyo tumefanya maandalizi, naamini tunakwenda kushinda na kuanza msimu vizuri tukiwa na taji la kwanza,” alisema Zoran.

“Mechi yoyote ya dabi katika nchi zote nilizopita ni ngumu, lakini maandalizi tuliyofanya huku Misri, wachezaji walivyoimarika tofauti na nilivyowakuta, usajili wa wachezaji wapya pamoja na ubora wa kikosi naamini tunakwenda kushinda.

“Nimepata bahati kuwaona Yanga kupitia runinga ikiwemo mechi zote za msimu uliopita kuna vitu navifahamu kutoka kwao. Kama timu tutakwenda kuvifanyia kazi ili kuwa na kiwango bora katika mchezo huo na kushinda taji la kwanza tofauti na msimu uliopita.

“Baada ya hapo sasa nguvu tunaziweka katika ligi kwa jinsi ambavyo naiona Simba hii yenye mabadiliko tofauti na msimu uliopita kuna dalili za kwenda kutawala kutokana na ubora wa kikosi ulivyo.”

Katika hatua nyingine Zoran alisema Simba inahitaji kuonyesha ubora katika ligi pamoja na mashindano mengine ya ndani na kuwa uzuri wa timu wakati huu kuna wachezaji walio kwenye viwango bora.

“Kuna shida nyingi katika msimu uliopita zilikuwa changamoto kwa Simba kushindwa kufanya vizuri, hata mechi za nyumbani, hilo msimu huu sioni likipata nafasi kutokana na maandalizi yetu,” alisema.


MASHINDANO YA CAF

Katika hatua nyingine, Zoran alisema malengo ya muda mrefu ya Simba ni kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na bado wanaishi katika ndoto hizo na kwamba, anaamini siku moja watafanikiwa.

Alisema kwa sasa katika michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu wanataka kufuzu hatua ya makundi, kisha baada ya hapo wataangalia wamepangwa na timu gani ili kuweka mipango mingine mathubuti ya kuvuka.

Zoran alisema wanaweza kujikuta katika kundi lenye timu kubwa Afrika na hilo litawapa nafasi ya kupiga hesabu nzuri za kuwa bora dhidi ya wapinzani wao ili kupata nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.

“Kuna nyakati tunaweza kujikuta kwenye kundi lenye timu sio za kutisha na ikawa rahisi kusonga hatua inayofuata pengine kabla ya kucheza mechi za mwisho,” alisema Zoran. “Wakati tunataka kuona kwanza tunafuzu hatua ya makundi, kisha kuweka sasa yale malengo ya kucheza nusu fainali hadi fainali yenyewe.”