Zoran: Simba imeiva kinoma, apata video za Yanga

KOCHA wa Simba, Zoran Maki amesema kwa muda wa wiki mbili walizofanya maandalizi hapa Ismailia Misri kuna mabadiliko makubwa katika kikosi chake tofauti na msimu uliopita au alivyokikuta wakati anaanza kazi.

Zoran alisema baada ya kumaliza maandalizi yao huku Misri watakuwa na mechi ya kimataifa ya kirafiki siku ya Simba Day, na anaamini wataonyesha kiwango bora pamoja na kufanya vizuri.

Alisema baada ya hapo watakuwa na muda mwingine mfupi wa kufanya maandalizi ya kutosha dhidi ya mchezo mkubwa Tanzania dhidi ya Yanga.

“Katika kufahamu umuhimu wa mchezo na Yanga nimetenga muda wa kutosha kuangalia baadhi ya mechi zao za msimu uliopita ikiwemo zile nne zote ambazo walicheza na sisi,” alisema Zoran na kuongeza;

“Ninazo taarifa zao na nafahamu vitu vingi kutoka kwao vya msimu uliyopita baada ya kuangalia mechi kupitia runinga pamoja na vile ambavyo wapo msimu huu.

“Naenda kufanya nini? Hilo tusubiri hadi siku ya mechi kwani hizo ni kama silaha zetu Simba tu, naandaa ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kuchukua taji la kwanza kama malengo yetu yalivyo msimu huu.”

Katika hatua nyingine Zoran alisema kuna mabadiliko tofauti na alivyoanza kazi kwenye mazoezi ya kambi yao hapa Misri kwani alinza na mazoezi mengi magumu ili kutengeneza miili ya wachezaji kuwa katika ushindani.

Alisema katika eneo hilo amefanikiwa na ratiba iliyopo sasa ni mazoezi mengi ya mbinu na kufungua miili ya wachezaji ili kila mmoja kutamani kucheza mpira katika malengo anayohitaji.

“Niwapongeze wachezaji wangu kila mmoja amejitoa kwa nafasi yake kufanya vile ambavyo nahitaji hadi sasa, wengi wanauelewa hadi nimevutiwa na kufanya nao kazi ni jambo zuri kuona tunaishi na kufanya kazi kama vile ambavyo inahitajika,” alisema Maki na kuongeza;

“Tumebakiwa na wiki moja ya mazoezi hapa Misri tutafanya ya mbinu zaidi na masahihisho ya kile ambacho kitakuwa hakijafanywa vizuri ili tukirejea Dar es Salaam tuwe tayari kwa mashindano ya ndani na nje ya nchi,”

“Ndani ya hii wiki tunaweza kucheza mechi mbili za kirafiki ikiwemo hii ya Jumatatu na baada ya hapo tutaanza taratibu za kurudi Tanzania kwa ajili ya kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki siku ya Simba Day.

“Mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi siku hiyo ili kuishuhudia timu yao yenye mabadiliko makubwa katika maeneo mengi tofauti na ilivyokuwa msimu uliyopita.

“Naamini mashabiki wetu wote ambao watakuja uwanjani watafurahi kuona timu yao ikiwa na mabadiliko kwani tutacheza na moja ya timu iliyofanya vizuri huko kwao.”