Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zagallo angefanya jambo Simba v Berkane

Muktasari:

  • Kipindi cha pili kilipoanza Simba iliyokuwa ikiongoza 1-0 na kupania kupata bao la pili ili iwe sare na Berkane ya Morocco ilikuwa na matumaini ya kutimiza ndoto ya kubeba kombe na Tanzania kuweka historia.

BAADA ya Simba kutofanikiwa kulibeba Kombe la Shirikisho la Afrika kutokana na kwenda sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar nilikumbuka hekima ya aliyekuwa kocha wa Brazil katika miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Mario Zagallo.

Kipindi cha pili kilipoanza Simba iliyokuwa ikiongoza 1-0 na kupania kupata bao la pili ili iwe sare na Berkane ya Morocco ilikuwa na matumaini ya kutimiza ndoto ya kubeba kombe na Tanzania kuweka historia.

Lakini mambo yalikwenda mrama na matumaini kuhama baada ya Yusuph Kagoma kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 50 na Simba kuwa na mchezaji mmoja pungufu.

Nilimkumbuka kocha Mario Zagallo kwa sababu katika michezo kama hii ya kimataifa alifanya uamuzi mgumu pale alipokuwa na wachezaji waliopewa kadi ya njano katika kipindi cha kwanza.

Kwake ilikuwa kawida katika kipindi cha pili kuwaweka pembeni hata wachezaji watatu waliopewa kadi ya njano katika kipindi cha kwanza.

Alifanya hivyo kwa kuhofia akitokea mmoja wao kugongwa njano ya pili na kutwangwa nyekundu kikosi kingelikuwa na kazi pevu ya kucheza wakiwa pungufu.

Kila alipoulizwa kwa nini aliamua hivyo, jawabu yake ilikuwa bora ujinyoe kichwa mwenyewe kwa kiwembe kuliko kunyolewa na mwengine kwa kigae.

Zagallo aliyefariki dunia Januari mwaka jana akiwa na umri wa miaka 92, ni mmoja wa makocha waliosifika kuanzia katikati ya miaka ya miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Aliipatia Brazil heshima ya kuwa timu bora ya kandanda duniani, kwanza kama mchezaji na baadaye kocha.

Katika miaka ya mwisho ya maisha yake kila alipofika uwanjani watu walisimama na kumwambia "Ahsante… Tunaheshimu mchango wako."

Zagallo ambaye mara chache alizungumzia masuala yasiyohusu kandanda  alikasirishwa na kauli za kuwadhalilisha wahamiaji wa Marekani zilizotolewa na Rais Donald Trump katika uongozi wake wa awamu ya kwanza.

Alisema Trump ni mtu asiyejijua kwani hata yeye ni mtoto wa wahamiaji na ukweli ni kwamba wahamiaji wamechangia sana maendeleo ya Marekani.

Zagallo alisema na yeye aliyezaliwa Brazil ni mtoto wa wahamiaji kutoka Lebanon na alifurahi kuipatia nchi hiyo heshima katika soka, kwanza akiwa mchezaji na baaadaye mwalimu.

Zagallo alipewa tuzo za kitaifa na kimataifa na masanamu yake akilisakata kabumbu au kocha yapo yametapakaa Brazil.

Mario Jorge Lobo Zagallo alilaumiwa na baadaye kusifiwa kwa kuleta mageuzi makubwa yaliyofanya mchezo wa kandanda kuvutia.

Wakati alipokuwa mwalimu wa kikosi cha Brazil cha kina Pele, Jairzinho, Tostao na Relino alikuwa mtu wa kwanza kushinda Kombe la Dunia kama mchezaji (1958 na 1962) na kama kocha wa nchi hiyo 1970 na mshauri na kocha msaidizi 1994.

Mara zote nne Brazil ilipobeba Kombe la Dunia ulihusika mguu, mkono au kichwa cha Zagallo, akiwa mchezaji au kocha.

Vile vile aliifikisha timu ya nchi za Ghuba (UAE) katika fainali za Kombe la Dunia za 1990.

Zagallo aliyezaliwa katika mji wa Maceio, Brazil, wazazi wake wakiwa na asili ya Lebanon, alianza safari ya kandanda Marekani 1948, akiwa na umri wa miaka 17.

Alichezea klabu mbalimbali mpaka 1958 aliporudi Brazil na kujiunga na Flamengo na baadaye Botafogo.

Akiwa winga wa kushoto alikuwa hatabiriki uwanjani kama ilivyokuwa tabia yake nje ya uwanja.

Tafauti na mawinga wa zama zake, Zagallo alirudi nyuma mara nyingi kulinda goli lao liliposhambuliwa na kupachikwa jina la 'winga mlinzi'.

Wakati ule haikuwa rahisi kuvuma kwa vile alikuwa na wachezaji waliotikisa dunia kama Pele, Garrincha, Didi, Santos, Castilho, Bellini, Gilmar Didi, Vava na Zito.

Zagallo aling'ara katika fainali za Kombe la Dunia za 1958 na za 1962.

Aliichezea Brazil mara 36 kutoka mwaka 1958 hadi 1964 na kukabidhiwa timu ya Brazil 1970 baada ya kocha Joao Saldanha kuachia ngazi kwa kulaumiwa kuwaingiza wachezaji walioonekana hawakustahili kuwamo katika kikosi hicho.

Alifanya mabadiliko ya wachezaji na wimbo wake mkubwa kwa wachezaji ulikuwa: Usijali kupachikwa bao, lililo muhimu ni kwa kila bao mnalofungwa mnalipiza kwa kufunga mawili.

Aliwafundisha wachezaji kujipanga kama kete za chesi na kuiwezesha Brazil kushinda michezo yote sita katika fainali za Kombe la Dunia za 1970 zilizofanyika Mexico ikifunga jumla ya mabao 19.

Aliwapanga Pele, Gerson, Tostao, Jairzinho na Rivelino kama makamanda na wengine akawaita wapiganaji.

Yeye ndiye aliyebuni mfumo wa 5-3-2 na kuwafanya wachezaji kugeuka mara kwa mara kucheza 3-5-2 na baadaye kurudia 5-3-2. Mabadiliko yalifanyikia aliposimama na kumnyooshea kidole nahodha.

Alipoacha kuifundisha Brazil, alifundisha klabu na timu za nchi mbalimbli, ikiwa ni pamoja na Klabu ya Al Hilal ya Misri, timu za Kuwait na Saudi Arabia.

Namna Zagallo alivyowajenga mabeki kuwa hatari wanapopanda mbele kushambulia kama ilivyoonekana kwa Cafu, Leonardo na Roberto Carlos, ni mfanikio yanayopigiwa mfano mpaka leo.

Alipofanya mageuzi ya mabeki watafute mabao, makocha wengi walimuona amechanganyikiwa na vyombo vya habari vya Brazil vilitaka apimwe kama akili yake ilikuwa sawa.

Lakini alisisitiza hivyo ndivyo alivyotaka na kuwaambia wachezaji wakifungwa yeye angewajibika kulaumiwa na wakishinda pongezi zilikuwa sio zake bali zao.

"Katika maisha sio vizuri kula chakula kimoja au kutembelea eneo moja kila siku. Kitu usichoweza kubadili ni wazazi tu," alisema alipotetea mageuzi katika kandanda.

Mafanikio yake yalichangia nchi nyingi kufuata mtindo wa mabeki kutafuta magoli.

Zagallo alikuwa mwalimu wa soka ambaye hakujali lawama na alikataa kuingiliwa katika kupanga timu.

Wakati mmoja aliposhinikizwa kupangiwa timu na wanasiasa, vyombo vya habari na mashabiki, Zagallo alisema: "Kama nilivyokuwa sina haki kumpangia Rais baraza la mawaziri naye hastahili kunipangia wachezaji. Lakini ninapoona viongozi au wahariri wa michezo wananipangia timu sishangai na ikiwa haitokuwa hivyo basi Brazil itakuwa imebadilika kwa mapenzi yake kwa kandanda".

Zagallo aliwakuna wengi aliposema: "Brazil ina watu milioni 150 na kila mmoja, hata vikongwe vilivyopo kitandani ni makocha wa timu ya taifa. Kila mmoja hupanga timu yake, lakini inayoteremka uwanjani ni ya Mario Zagallo."

Alisema hata mapadri, pamoja na kuongoza kanisa wanataka kuongoza kandanda. Ni raha iliyoje, lakini kama kocha dhamana ya kupanga timu ilikuwa yake na makocha hao wengine watapatao milioni 150 ni wasaidizi wake na halazimiki kufuata ushauri wao.    

Tangu akiwa mchezaji na baadaye mwalimu, Zagallo amekuwa akisema hafurahishwi na matokeo ya timu kutoka sare.

Alitaka lazima timu zinapopambana moja iwe imeshinda na moja imeshindwa kwa sababu mchezo wa kutoka sare unapoteza ladha ya kandanda.

Wakati ambao Zagallo aliuzungumzia kwa furaha ni wachezaji wake walivyocheza samba kule Mexico 1970 na kubeba Kombe la Dunia kwa kuichakaza Italia 4-1 katika fainali.

Lakini alisononeka alipoikumbuka Julai 23, 2001 Brazil ilipotolewa katika robo fainali na Honduras na hakufikiria katika maisha yake nchi ndogo kama Honduras ingeliiadhibu Brazil.

Vile vile alisikitishwa alipofukuzwa kuwa kocha wa Brazil mwezi Julai, 1998 baada ya kuwa mwalimu katika michezo 148 ambapo ilishinda mara 107, ikaenda sare mara 29 na kufungwa mara 12.

Mchezo wake wa mwisho kama mwalimu Brazil ilipofungwa 3-0 na Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia.

Mpangilio wa kikosi wa mwaka 2010 wa vyombo vva habari maarufu duniani ulikuwa kama hivi: Kocha ni Mario Zagalo (Brazil) na wachezaji ni Puskas (Hungary), Pele (Brazil), Eusebio (Ureno), Cruyff (Uholanzi), Platini (Ufaransa), Beckenbauer (Ujerumani), Maradona (Argentina), Maldini (Italia), Bobby Moore (Uingereza), Carlos Alberto (Brazil) na Yashin (Urusi).

Nimeelezea habari za kocha huyu kama somo kwa makocha wetu kumuiga Zagallo kwa kuwatoa wachezaji waliopata kadi za njano ili kuepusha kubakia na wachezaji pungufu dakika za mwisho za mchezo.