Wabongo wapewa mchongo wa Messi Hispania

Muktasari:
- Kambi za majira ya kiangazi ni mafunzo maalumu kwa vijana ambazo hufanyika kila mwaka wakati wa likizo za shule sehemu mbalimbali hasa Ulaya na Amerika. hizi hujulikana kama 'summer football camps'.
KATIKA ulimwengu wa soka, historia ya mastaa wakubwa haianzii katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Haianzii katika klabu kubwa kama Barcelona, Manchester United, Real Madrid au Bayern Munich, bali huanzia katika misingi ya chini zaidi, kama viwanja vya mazoezi, akademi ndogo na kambi za majira ya kiangazi.
Kambi za majira ya kiangazi ni mafunzo maalumu kwa vijana ambazo hufanyika kila mwaka wakati wa likizo za shule sehemu mbalimbali hasa Ulaya na Amerika. hizi hujulikana kama 'summer football camps'.
Lionel Messi, Andrés Iniesta, Gerard Piqué, Sergio Busquets, Mason Mount na Kingsley Coman ni baadhi ya waliopita katika kambi hizi za majira ya kiangazi kabla ya kuwa mastaa wakubwa duniani.
Kambi hizi, hutoa taaluma mbalimbali ikiwamo kufundisha nidhamu ya soka, kucheza mechi za kirafiki na kujifunza lugha mpya pamoja na kuwekwa karibu na klabu kubwa. Hiyo ni moja ya fursa za maisha ya soka kama ilivyokuwa kwa nyota hao na sasa fursa hiyo imeifikia Tanzania.
Kwa mara ya kwanza, vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 12 hadi 21 wamepewa nafasi ya kushiriki katika kambi ya kimataifa ya majira ya kiangazi ya soka itakayofanyika jijini Valencia, Hispania kuanzia mwezi Juni hadi Agosti 2025.

MAFUNZO YA HALI YA JUU
Huko, watapata mafunzo ya soka ya kiwango cha juu kutoka kwa makocha waliobobea Ulaya. Makocha hawa wana leseni za juu kabisa za UEFA PRO. Kambi hii ni sehemu salama na daraja la kufikia ndoto za vijana wengi na kufikia mafanikio.
Maisha watakayoishi huko ni ya kitaaluma ya soka. Watapata mafunzo ya kiufundi, kushiriki mechi za kirafiki na kufanyiwa majaribio mbele ya wakufunzi na wawakilishi kutoka klabu mbalimbali za soka za Kihispania.
Pia, watapata nafasi ya kujifunza lugha ya kihispania, kupata uzoefu wa maisha na kuunganishwa na vijana wengine kutoka nchi mbalimbali.
Huduma zote muhimu kama malazi ya kisasa, chakula cha kiafya, usafiri binafsi ndani ya jiji la Valencia na huduma ya afya zitatolewa kwa viwango vya kimataifa.
KWA NINI TANZANIA?
Mtanzania anayeishi Hispania, Hemed Tawah amefichua sababu za Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yaliyofikiwa na fursa hii, ni kutokana na mwamko wa soka na kufanya vizuri kwa klabu kubwa kama Yanga na Simba.
"Kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo kwa Afrika yanatazamwa, yote hiyo ni kutokana na kufanya vizuri kwa klabu za Tanzania kimataifa hasa Simba na Yanga."
"Hivyo nilipofuatwa kwa jambo hili, nilifurahi sana na kuwa tayari kushiriki mpango huu. Naamini utafungua njia kwa vijana wengi wa Kitanzania wenye ndoto kubwa, hatua moja inaweza kuanzisha nyingine."
Kwa mujibu wa Tawah kwa yeyote ambaye ataguswa na kuhitaji kuwa sehemu ya kambi hiyo milango ipo wazi katika tovuti ya spanishprofootball.

UNAKUWA KAMA MESSI, MOUNT
Kama ilivyoelezwa kwa mastaa wakubwa waliotikisa ulimwengu wa soka ni kutokana na matokeo ya kambi hizi za majira ya kiangazi. Messi amepita katika kambi ya Barcelona (Akademi ya Barça). Mount, kiungo wa Manchester United na timu ya taifa ya England, aliibuka katika kituo cha mafunzo cha vijana cha (Chelsea Foundation Youth Program), huku Kingsley Coman akianzia katika akademi ya PSG
Kambi ya IMG iliyo Marekani inayokusanya vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani iliwahi kulea vipaji kama Landon Donovan na Freddy Adu wa Marekani.
Kwa mafanikio ya nyota hao katika soka, inaonyesha uwezo wa kambi hizi za majira ya kiangazi na sasa Tanzania inakaribishwa kuwa sehemu ya nchi zitakazonufaika na fursa hii.
Vijana kutoka sehemu mbalimbali Tanzania iwe Mwanza, Iringa, Kigoma au Zanzibar watapata kile walichopata Messi na Pique wakiwa na umri mdogo, kwani lengo kubwa la kambi ya Hispania ni kukuza vipaji vya Afrika na hasa Afrika Mashariki.