Prime
Simba, Yanga kazi ipo CAF

KUMEKUCHA Afrika. Ndio, unaambiwa hadi kufikia Julai 31 mwaka huu, zitafahamika timu zote zitakazoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu ujao wa 2025-2026, lakini hadi sasa vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga wameungana na mabingwa saba.
Al Ahly na Pyramids (Misri), RS Berkane na AS FAR (Morocco), Esperance (Tunisia), Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates za Afrika Kusini ni kati ya vigogo saba waliofuzu Ligi ya Mabingwa wakiwa ni kati ya timu zilizowahi kubeba ubingwa wa michuano hiyo na ile ya Kombe la Shirikisho.
Makocha wapya waliotambulishwa wikiendi hii, Florent Ibenge wa Azam na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars wenyewe wapo sambamba na mabingwa wengine wa Afrika katika Kombe la Shirikisho, licha ya orodha kamili ya timu zote zitakazocheza CAF itafahamika mwishoni mwa mwezi.
Simba na Yanga ndio wawakilishi nchi katika Ligi ya Mabingwa, kukiwa na vigogo saba waliowahi kubeba taji hilo na lile la Kombe la Shirikisho wakati wanaendelea kusikilizia orodha ya mwisho kabla ya kupangwa katika poti kwa ajili ya kuanza msimu mpya wa michuano hiyo ya Afrika.
Al Ahly na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa sasa Pyramids za Misri ni kati ya timu zilizokata tiketi ya michuano hiyo inayotarajiwa kuanza hatua ya awali Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lililotangaza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga, Simba na Mlandege zitashiriki na Kombe la Shirikisho Afrika linalozihusu Azam, Singida BS na KMKM, itaanza Septemba 2025 kufuatia uwepo wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu.
USAJILI WACHEZAJI
Kipindi cha kwanza cha usajili kwa hatua ya awali kinaanza Agosti 1-31, 2025. Kipindi cha pili cha usajili kwa hatua ya pili kinaanza Septemba 1-30, 2025.
Kipindi cha usajili kwa hatua ya makundi kinaanza Oktoba 1-31, 2025. Kipindi cha usajili kwa sehemu zilizosalia za hatua ya makundi na mechi za mtoano kitaanza Januari 1-31, 2026.
WAWAKILISHI WA TANZANIA
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania Bara itawakilishwa na mabingwa Yanga sambamba na Simba iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi, huku Mlandege ikiiwakilisha Zanzibar baada ya kutwaa ubingwa visiwani humo.

Upande wa Kombe la Shirikisho, Azam na Singida Black Stars zitaiwakilisha Tanzania Bara na KMKM ikiwa na uwakilishi wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa CAF, kati ya mashirikisho 54 ya soka yaliyo chini yao, 12 yenye renki za juu yanakuwa na wawakilishi wawili wawili katika kila mashindano ambapo Tanzania Bara ni mojawapo.
Katika mashirikisho hayo 12 bora, Tanzania Bara ni ya tano ikipanda kwa nafasi moja baada ya kufikisha pointi 82.5 sawa na Tunisia ikiicha nchi ya saba Angola yenye pointi 55.
Katika viwango vya CAF, Tanzania ni timu tatu pekee ndizo zilizokusanya pointi kwenye michuano hiyo ya klabu kufuatia kufika kwao angalau hatua ya makundi.

Timu hizo ni Simba iliyopo ya tano ikikusanya pointi 48, inafuatiwa na Yanga inayokamata nafasi ya 12 na pointi 34, kisha Namungo yenye pointi 0.5 ikiwa nafasi ya 75.
Azam licha ya kushiriki mashindano ya CAF mara kwa mara, haina pointi yoyote kwani haijawahi kucheza hatua ya makundi. Msimu ujao itakuwaje baada ya kuboresha benchi la ufundi kwa kumleta kocha Florent Ibenge mwenye wasifu mkubwa na uzoefu wa kutosha wa michuano ya CAF? Tusubiri tuone.
Yanga na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika, tunatarajia kuona mwendelezo uleule kama ilivyokuwa msimu wa 2023-2024, achana na uliopita 2024-2025 ambao Simba ilishiriki Kombe la Shirikisho baada ya kuikosa nafasi ya Ligi ya Mabingwa.
Katika msimu wa 2023-2024, Yanga ilianzia hatua ya awali, Simba ikianzia hatua ya pili na zote zikafanya vizuri zikafika hadi robo fainali.
Msimu uliomalizika 2024-2025, Simba ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho, wakati Yanga ikiishia makundi Ligi ya Mabingwa.

Kwa kuendelea kufanya vizuri Simba na nafasi yao kwenye viwango vya CAF, haitashangaza kuona msimu ujao ikianzia tena hatua ya pili, huku wawakilishi wengine wa Tanzania katika mashindano husika wakianzia hatua ya awali.
Kwa misimu ya hivi karibuni, tumeshuhudia CAF ikizipanga timu za ukanda mmoja kukutana hatua hizi za awali kuitafuta hatua ya makundi hali inayofanya timu za CECAFA kucheza zenyewe tofauti na hapo awali ambapo hatua za mwanzoni tu timu ya ukanda wa UNAF inakutana na ya kutoka UNIFFAC.
ZILIZOFUZU
Hadi kufikia sasa, Ligi ya Mabingwa Afrika timu zilizofuzu ni Yanga na Simba (Tanzania), Al Ahly na Pyramids (Misri), RS Berkane na AS FAR (Morocco), Esperance na US Monastir (Tunisia), Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates (Afrika Kusini), Mlandege (Zanzibar) na Rahimo (Burkina Faso).
Nyingine ni FC Nouadhibou (Mauritania), Petro Luanda (Angola), Remo Stars (Nigeria), Vipers (Uganda), Mangasport (Gabon), Fassell (Liberia), Lioli (Lesotho), Aigle Noir (Burundi), Power Dynamos (Zambia), ASC Jaraaf (Senegal), Kenya Police (Kenya), Aigles du Congo na FC Lupopo (DR Congo).
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, zilizofuzu mpaka sasa ni Azam na Singida Black Stars (Tanzania), KMKM (Zanzibar), Kwara United na Abia Warriors (Nigeria), Nairobi United (Kenya), AS Maniema (DR Congo), Étoile du Sahel na Stade Tunisien (Tunisia), Wydad AC na Olympique de Safi (Morocco), Zamalek na Al Masry (Misri), USM Alger na CR Belouizdad (Algeria), Primeiro de Agosto na Kabuscorp (Angola), San Pedro na AFAD (Ivory Coast), Kaizer Chiefs na Stellenbosch (Afrika Kusini), ZESCO United (Zambia), Djoliba AC (Mali), Asante Kotoko (Ghana), Jwaneng Galaxy (Botswana), AS Otoho d’Oyo (Congo), Coton FC (Cameroon), Ferroviário de Maputo (Msumbiji), FC 15 de Agosto (Guinea), Flambeau (Burundi), Rayon Sports (Rwanda), Sidama Bunna (Ethiopia), Royal Leopards (Eswatini), Bantu FC (Lesotho), Kator FC (Sudan Kusini), AS Port (Djibout), Black Man Warrior (Liberia), Dekedaha (Somalia), Gbohloé-su des Lacs (Togo), Elect Sport (Chad), Bhantal FC (Siera Leone), Foresters FC (Seychelles), Djabal FC (Comoros), AS Police (Mali) na NEC (Uganda).