VPL 2020/21 ulikuwa msimu wa aina yake

Wednesday July 21 2021
vpl pic
By Ramadhan Elias

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) 2020/21 ulimalizika juzi Jumapili baada ya timu zote 18 kukamilisha mechi 34 za ligi hiyo kwa mfumo wa nyumbani na ugenini na kushuhudiwa timu nne zikishuka daraja moja kwa moja huku Simba ikiibuka bingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Zilichezwa jumla ya mechi 306 msimu huu ambapo mechi 217 zilimalizika kwa timu kupata ushindi huku mechi 89 zikimalizika kwa sare/suluhu na kushuhudiwa yakifungwa jumla ya mabao 610 na jumla ya pointi zilizopatikana kwa timu zote kuwa pointi 740.

Kiufupi ilikuwa ni ligi yenye ushindani mkubwa kwa timu zote ambapo kila timu ilijitahidi kutafuta matokeo chanya lakini waliochanga vyema karata ndio waliocheka.

Mwadui, Ihefu, Gwambina na JKT Tanzania zimeonyeshwa mkono wa kwaheri kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kumaliza katika nafasi nne za mwisho huku Coastal Union na Mtibwa Sugar zikisubiri kucheza mechi za mtoano na Pamba na Transit Camp ili kujua hatima yao kama ni kushuka ama kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao.


WACHEZAJI

Advertisement

Ni dhahiri kuwa Ligi hii ilikuwa bora na yakuvutia kutokana na uwezo na ubora wa wachezaji waliokuwepo.

Kila timu ilikuwa na nafasi ya kusajili wachezaji 10 wa kigeni ambapo baadhi ya timu zilitumia walau nusu ya nafasi hizo na wachezaji wengi wa kigeni waliweza kuleta ushindani sambamba na wazawa ambao walikuwa moto kwa msimu huu.

Pia wapo wachezaji wengi ambao msimu huu haukuwa mzuri kwao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeraha na ufinyu wa nafasi za kucheza na huenda msimu ujao wakatatua changamoto hizo.


MAKOCHA/ BENCHI LA UFUNDI

Huu ni miongoni mwa misimu iliyoshuhudiwa makocha wengi ndani ya msimu mmoja. zaidi ya makocha wakuu 25 wamefundisha kwenye ligi kuu msimu huu ambapo wapo waliotimuliwa ama kuachana na timu na wengine wamesalia katika vikosi vyao.

Wingi huo wa makocha, umetoa burudani kwa mashabiki na wadau wa soka kwani wameshuhudia ufundi na mbinu tofauti ambazo kila kocha alitumia zake jambo ambalo kuna wachezaji walinufaika na wengine ikala kwao.


WAAMUZI

Kabla ya kuwalaumu waamuzi waliosimamia mechi za Ligi Kuu kwa msimu huu, yapaswa kuwapongeza kwanza kwa kazi kubwa walioifanya na kushudia ligi inamalizika bila ya kuvunjika au kugomewa kwa mchezo wowote kisa uamuzi wa waamuzi.

Sambamba na pongezi hizo pia msimu huu unapaswa kuwa funzo kwao, kuna makosa mengi ya kimchezo yamefanyika, yapo yaliyoonwa mubashara kwa macho ya watazamaji na yapo mengine yalionekana kupitia teknolojia na sheria tofauti za soka jambo ambalo waamuzi wanahitaji kuyafanyia kazi kubwa ili yasijirudie katika misimu ijayo.


MASHABIKI NA WADAU

Msimu huu ulinogeshwa zaidi na mashabiki wa timu zote pamoja na wadau wengine wa soka waliojitokeza kusapoti ama kushangilia timu zao kwa namna tofauti.

Ubishi, utani, majigambo, kejeli na sifa ni miongoni mwa vitu vilivyofanywa na mashabiki na kuongeza ushindani katika ligi.

Kila timu ilihitaji kufanya vizuri ili kuwafurahisha wadau na mashabiki wake na kuwafanya watembee vifua mbele dhidi ya wapinzani wao.


MAMLAKA

Mamlaka za kusimamia soka nazo zilifanya kazi yao, hapa nazungumzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kila mamlaka kwa nafasi yake ilihakikisha ligi inachezwa na kumalizika kwa amani.

Kuna mambo tofauti yaliyotokea ambayo hayakuwa sahihi mfano baadhi ya ratiba kupanguliwa bila kuzingatia sheria na makosa mengine ambayo hayakuwapendeza wadau na mashabiki wa soka nchini hivyo yanatakiwa kufanyiwa kazi kwaajili ya msimu ujao.


VIONGOZI

Achana na Simba, Yanga, Azam na baadhi ya timu zenye uwezo kiuchumi wa kutunza timu, pongezi nyingine ni kwa viongozi wa timu waliopambana kwa hali na mali kuhakikisha timu zinaishi na zinacheza mechi.

Sio kama zamani lakini bado msimu huu haukuwa bora kiuchumi kwa baadhi ya timu, usafiri, malazi, vifaa na stahiki za wachezaji ilikuwa ngumu kuzipata kwa wakati lakini busara na upambanaji wa viongozi ulifanya ligi ikachezwa pamoja na ugumu huo.

Mwisho ni pongezi kwa Simba, Yanga, Azam na Biashara United kwa kumaliza katika nafasi nne za juu na kukata tiketi ya kuwakilisha nchi na kuonesha ubora wa VPL kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Pongezi nyingine za dhati ni kwa KMC, Polisi Tanzania, Tanzania Prisons Dodoma Jiji, Namungo, Mbeya City, Ruvu Shooting na Kagera Sugar kwa kuwa katika timu 12 zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao, wadau na mashabiki wa soka wanatarajia kupata ushindani zaidi kwa msimu kesho.

Nahodha wa Simba, John Bocco amekuwa mfungaji bora akifunga mabao 16 akiwapiku Prince Dube (14), Chris Mugalu (15) na Medie Kagere (13) huku Aishi Manula ambaye ni kipa wa Simba akiwa kipa bora kwa mara ya nne mfululizo akiwa ndani ya timu hiyo baada ya kumaliza msimu huu akiwa ana ‘clean sheet’ 18.

Advertisement