Prime
CHAN ilishafika, lakini mashabiki wamepoa

ZAIDI ya asilimia 80 ya mashabiki walioingia Uwanja wa Al Bayt nchini Qatar kuangalia mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 walikuwa ni wananchi wa Morocco.
Unaweza kusema idadi hiyo ilikuwa kubwa kwa sababu Morocco ilikuwa taifa la kwanza la Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia, lakini ukiangalia maandalizi na ushawishi uliokuwepo kutoka mwanzo, utagundua kuwa mafanikio hayo yaliongeza tu chachu kidogo katika kingi kilichokuwa kimeshawekwa sawa.
Mashabiki 55,000 kati ya 69,000 walioingia Uwanja wa Al Bayt kuangalia mechi hiyo dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi, Ufaransa, walikuwa ni mashabiki wa Morocco - wengi wakiwa ni wale waliokata tiketi za ndege kutoka nchini Morocco na wengine ni wale waliolowea ughaibuni huku baadhi wakitoka nchi za Kiarabu.
Morocco walionyesha mapenzi ya hali ya juu kwa mchezo wa mpira wa miguu na zaidi timu yao ya taifa ambayo ililazimika kuvuka viunzi kama kuishinda Ubelgiji, iliyokuwa nambari mbili kwa ubora duniani, katika mechi ya makundi, kuishinda Hispania kwa penati katika 16 bora na kuishinda Ureno iliyoongozwa na Christiano Ronaldo katika mechi ya robo fainali.
Uwingi wa mashabiki wa Morocco nchini Qatar haukutokana na mafanikio ya kusonga mbele hadi nusu fainali pekee, bali utamaduni uliojengwa na vikundi maarufu vya uhamasishaji vya Ultra ambavyo hufanya kazi kubwa ya kujaza viwanja kwenye mechi za ligi.

Lakini pia uongozi wa jumuiya za mashabiki ambao ulifanya kazi kubwa ya uhamasishaji na maandalizi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia za Qatar, zikikaribisha mashabiki wote kutoka Mashariki ya Kati, Morocco na barani Ulaya kwenda Qatar ambako wanakuchukulia kama nyumbani kwa pili.
“Kama jamii, tumekuwa sehemu ya Kombe la Dunia tangu Qatar ipewe haki za kuwa mwenyeji mwaka 2010. Kwanza, kama mashabiki wwaliopewa heshima ya kuwa na mashindano haya ndani ya sehemu ya yetu duniani na pia kama jamii, tuliojitolea na kuchangia utamaduni wetu katika matukio kama Klabu Bingwa ya Dunia na Kombe la Waarabu,” alisema Hassan Obaid, rais wa jumuiya za makundi ya mashabiki.
Obaid na Wamorocco wenzake walifanya kazi karibu na kamati maalumu ya ugavi na urithi (Supreme Committee of Delevery and Legacy) wakati wa kuelekea fainali za Kombe la Dunia za Qatar kuandaa matamasha ya kitamaduni na kushiriki katika matukio mengine mengi kama ufunguzi wa viwanja na mashindano kuwaanda mashabiki kwa fainali hizo.
Mambo hayo na mengine mengi husaidia kuwafanya wananchi wa Morocco kuwa tayari kwa matukio ya mpira wa miguu na sasa taifa hilo limekuwa kwa kasi kutoka kupenda michezo mingine na kuwa lenye wendawazimu wa mpira wa miguu.

Hayo yalikuwa yakisemwa miaka michache kabla ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022. Kwetu tuna chini ya siku 30 kabla ya kuandaa fainali kubwa barani Afrika za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) tunazoandaa kwa pamoja nan chi za Kenya na Uganda.
Tanzania, ambayo inaweza kuwa ndio inaongoza kwa mashabiki wake kuwa na unazi mkubwa wa mpira wa miguu, tumepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi itakayofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 2, wakati tutakapoikaribisha Burkina Fasso.
Kamati ya Mandalizi imeonekana kufanya kazi kubwa ya kufuatilia kila kinachotakiwa, ikiwa ni pamoja na viwanja vitakavyotumika kwa mechi, viwanja vya mazoezi na mambo mengine muhimu. Lakini, ukiacha vyombo vya habari, ni mashabiki wachache wanaoweza kuwa wanajua kinachoandaliwa na kukisubiri kwa hamu kama ile waliyokuwa nayuo Wamorocco waliposikia nchi jirani ya Qatar ingeandaa fainali za 2022.

Hakuna matukio yoyote yanayowaandaa Watanzania kujiandaa kwa mashindano hayo ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Fainali za Mataifa (AFCON) ambazo pia tutaziandaa kwa pamoja na majirani hao wawili mwaka 2027.
Nguvu kubwa ilihitajika kuandaa mashabiki, hasa kutokana na ukweli kwamba fainali hizi zi kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Afcon 2027 kwa kuwa uzoefu mkubwa na elimu itapatikana kabla yam waka 2027. Kwa maana hiypo, nguvu kubwa ilitakiwa ianzie sasa ili yale mapungufu yawe machache kabla yam waka 2027.
Lakini nguvu kubwa inahitajika kwa CHAN kwa kuwa mashindano haya hayajiuzi kama zilivyo fainali za Afcon. Mashindano haya yanashirikisha wachezaji ambao wanashiriki ligi za ndani ya nchi na hivyo si wale maarufu barani Afrika au duniani.
Hutegemei kuona nyota kama Victor Omsihen wa Nigeria, Mohamed Salah (Misri), Sadio Mane (Senegal), Ashraf Hakimi (Morocco), Ademola Lookman (Nigeria), Serhou Guirassy (Guinea), Inaki Williams (Ghana) na Riyadh Mahrez (Morocco).
Hao na wenzao wangekuwa wanakujan CHAN wala kusingehitajika nguvu za ziada kuwahamasisha mashabiki kwa kuwa wameshajijengea majina kote duniani na hivyo wangefuatwa sit u na mashabiki wan chi zao, bali na wengine wengi duniani wanaoshabikia klabu zao.

Ni kwa jinsi hiyo, wenyeji, hasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitakiwa liwe limeshajenga mtandao wa mashabiki kwa ajili ya kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya fainali hizo za pili za michuano ya Afrika baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17.
Hawa pia inabidi wawe wameshajua hata uzuri wa timu yao na hasa wachezaji tegemeo ili waanze kukaa vichwani mwao na kwenye mazungumzo na mijadala kuhusu fainali hizo. Lakini hadi sasa hakuna uhakika wa kikosi kama cha Taifa Stars, na hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo ndiyo hutengeneza mashabiki wengi.
Timu inatarajiwa kwenda Misri kuweka kambi ya wiki tatu, lakini kimasoko ilitakiwa iwe hapa nchini ambako TFF ingekuwa na programu kadhaa za kutengeneza mapenzi na mashabiki wake, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi za kirafiki nyumbani kuwapa thamani hata wadhamini.
Kutegemea kikundi cha watu wachache wanaokuja na ngoma uwanjani na kudansi wakati wote wa mechi, hakuwezi kuwahamasisha mashabiki kufurika viwanjani kuishuhudia timu yao na nyingine zitakazoonyesha mchezo mzuri.
Kunahitajika uhamasishaji mkubwa kwa mashabiki ili waone ukubwa wa kilicho mbele yetu na umuhimu wake kabla ya mashindano hayo kuanza.
Shamrashamra za CHAN zilitakiwa ziwe zimeanza mapema sana, lakini zimechelewa sana. Hata hivyo, kwa kuwa bado tuna wiki takriban tatu, hatuna budi kuanza sasa na naamini vyombo vya habari vitakuwa tayari kutoa ushirikiano ili kujenga mazingira mazuri kwa fainali hizo kuwa na mafanikio ndani nan je ya uwanja.