Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa sababu tano Sillah kusaini Yanga

SILLAH Pict

KUELEKEA msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, mabingwa watetezi Yanga wanadaiwa kuanza kufanya maboresho ya kikosi kwa kusaka nyota wenye uwezo wa kuongeza ushindani ili kuleta matokeo chanya katika mashindano mbalimbali.


Miongoni mwa majina yanayotajwa ni la kiungo mshambuliaji aliyekuwa akikipiga Azam FC, Gibril Sillah (26), ambaye tayari keshamalizana na matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam baada ya mkataba wake kwisha na ameshaaga.


Kiwango cha mchezaji huyo msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kilikuwa moto na kilikuwa kikivutia macho ya mashabiki na wadau wa soka nchini. Nyuma ya hilo, kwa sasa tetesi nyingi zinaeleza nyota huyo tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia Wananchi ambao wametetea ubingwa wa ligi na Kombe la Shirikisho (FA).

Mgambia huyo aliyeitumikia Azam kwa misimu miwili kuanzia msimu 2023-25, alimaliza mkataba akiwa ameifungia mabao 19 yakiwamo 11 ya msimu huu na manane ya ule uliopita. Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya sababu ambazo pengine viongozi wa Yanga huenda wakawavutiwa na winga huyo aliyejizolea umaarufu nchini akiwa na Azam na hivyo kuamua kumshusha Jangwani.

SIL 01

1. PENGO LA MZIZE

Sababu ya kwanza ni kwamba Sillah huenda akaangaliwa kama mbadala sahihi wa kuziba pengo la Clement Mzize ambaye inadaiwa klabu hiyo imeshapokea ofa kutoka klabu kubwa za Afrika na hivyo msimu ujao anaweza kuuzwa nje ya Tanzania.

Kama nyota huyo ataondoka Jangwani basi Yanga itakabiliwa na uwezekano wa kumpoteza mshambuliaji chipukizi ambaye amekuwa tegemeo kwenye safu ya ushambuliaji akifunga mabao 14 msimu ulioisha wa Ligi Kuu. Sillah anaweza kuchukua nafasi hiyo kwa ufanisi kutokana na uelewa wake wa Ligi Kuu Bara na pia uwezo wake wa kucheza kama kiungo mshambuliaji au winga - maeneo ambayo Mzize amekuwa akiyatumikia ndani ya Yanga.

SIL 02

2. KUHIMILI PRESHA YA MECHI KUBWA

Kwenye mechi zote alizocheza dhidi ya Simba na Yanga, nyota huyo ameziadhibu timu hizo akicheza kwa kiwango bora.

Zilipocheza Simba na Azam msimu huu ambapo dakika 90 zilimalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2, Sillah alifunga bao la mapema kabla ya Elie Mpanzu wa Simba kusawazisha kwenye mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Mkapa.

Mbali na Simba, pia mchezaji huyo aliifunga Yanga mara tatu ndani ya misimu miwili aliyoitumikia Azam, na hilo linadhihirisha kuwa ana uwezo wa kuhimili mechi zenye ushindani hasa wa Simba na Yanga, hivyo iwapo Yanga itabahatika kumnasa anaweza kwenda kuendeleza pale alipoishia bila wasiwasi yoyote.

SIL 03

3. KIRAKA

Sillah siyo mchezaji anayecheza eneo moja, bali anaweza kucheza kama winga, kiungo mshambuliaji au hata mshambuliaji anayesimama pale mbele katikati. Asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga wana uwezo wa kucheza nafasi tofauti, jambo ambalo limekuwa na msaada kwa timu hiyo. Nyota kama Duke Abuya ana uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo na hata winga, ilhali Mzize mbali na kucheza akiwa mshambuliaji amekuwa akitokea pembeni kama winga.

Yanga inahitaji wachezaji wa aina hiyo wanaoweza kubadilika kulingana na mfumo wa kocha unaotokana na majukumu makubwa kikosini anayowapangia. Haitashangaza kwamba kuwa na mchezaji wa kariba ya Sillah ndani ya kikosi hicho kunaweza kuongeza wigo wa wachezaji wanaoweza kutumika katika maeneo tofauti wakati wowote kulingana na mahitaji ya mechi husika.

SIL 04

4. AINA YA UCHEZAJI

Nyota huyo amedhihirisha kwamba ni miongoni mwa mastaa ambao Ligi Kuu Bara imebarikiwa kuwa nao wenye kasi, ubunifu, pasi bora za mwisho na uwezo wa kumalizia kile alichokitengeneza ikiwa ni miongoni mwa vitu vinavyombeba.

Sillah ana kasi, 'dribolingi' nzuri na uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mwisho (key passes).

Katika baadhi ya mechi za Azam, mchezaji huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha mashambulizi ya haraka kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya mambo hayo, jambo ambalo mifumo mingi ya makocha waliopita Yanga miaka ya karibuni wamekuwa wakitaka ili kuongeza tija mbele ya wapinzani wao.

SIL 05

5. KIMATAIFA

Licha ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu 2022/23, lakini Yanga imekuwa haina mwendelezo mzuri sana kimataifa kama ilivyo kwa watani zao, Simba ambao wamekuwa wakifanya mambo flani hata kama timu yao haina watu bora.

Lakini, kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba Yanga inataka kujiimarisha na kuimarisha kikosi kwa ajili ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na wachezaji wanaotajwa ni wale wenye uzoefu na ubora wa kimataifa.

Sillah amecheza mechi kubwa za ndani na kimataifa akiwa na Raja Casablanca ya Morocco, hivyo anaweza kuwa msaada katika kuongeza ubora kwenye mashindano hayo, ikizingatiwa ubora wa timu hiyo enzi akiichezea nchini humo.

Hata hivyo, kwa miaka ya karibuni Yanga imekuwa ikiuza wachezaji kwenda nje wakiwamo Aziz KI na Fiston Mayele, hivyo kwa umri alionao Sillah ni wazi ana muda mrefu wa kucheza Jangwani akiendelea kuonyesha kiwango bora, huku akibeba nembo ya timu hiyo kimataifa.

Jambo jingine alilonalo ni kiu ya ushindi ambayo imekuwa ikionekana kila mara anapokuwa uwanjani, na hasa pale chama lake linapokuwa nyuma au likipambana kupata ushindi.