Utatu tishio Ligi kuu bara

Wednesday January 12 2022
Utatu pic
By Daudi Elibahati

RAHA ya mechi ni bao asikwambie mtu. Yaani yale mambo ya soka safi, pira biriani, ufundi na burudani nyinginezo wakati wa mchezo zote ni mbwembwe tu, mwisho wa picha mashabiki wataka kuona mpira uko wavuni.

Imezoeleka kuona Simba, Yanga na Azam FC kuzungumzwa sana nyota wao wanapowaadhibu makipa, lakini ukweli ni kwamba nje ya vigogo hao, zipo timu ambazo ni hatari kwa kuchana nyavu za wapinzani.

Kama ilivyo ada Mwanaspoti haliachi kitu katika kuhakikisha msomaji unaburudika na kila kitu kinachoendelea msimu huu na hapa leo linakuletea pacha kali zaidi zinazotikisa hadi sasa kwenye kucheka na nyavu.

Kuimba kupokezana, walisema wahenga, kwani ile Mbeya City iliyoponea chupuchupu kushuka daraja sio hii tunayoishuhudia msimu huu ambayo imekuwa ya moto na yenye kuvutia macho ya mashabiki nchini kuitazama.

Hii ni orodha inayohusisha pacha kali za timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa (2021/22).


Advertisement

YANGA

Ndani ya kikosi cha Yanga kuna nyota watatu wanaotamba kwa kufunga mabao mengi zaidi na vile timu hiyo ina utajiri wa mashabiki basi wanaongelewa kila sehemu.

Ndani ya kikosi hicho anayeongoza kwa mabao mengi (mabao 5) ni Fiston Mayale, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (mabao 4) na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ (mabao 3), wachezaji hao wamefunga zaidi ya nusu (mabao 12) kati ya yale yanayomilikiwa na timu hiyo yenye mabao 20 kwenye Ligi Kuu kufikia sasa msimu huu.

Mastaa wengine waliofunga mabao matatu ndani ya kikosi hicho ni Jesus Moloko, huku Khalid Aucho anayecheza kiungo mkabaji anamiliki mabao mawili.


SIMBA

Safu ya ushambuliaji ya Simba, inayoundwa na Meddie Kagere, Kibu Denis na Larry Bwalya imetengeneza mabao tisa, ambayo ni zaidi ya nusu yanayomilikiwa na timu hiyo (mabao 14).

Wakati huohuo, nahodha wao, John Bocco ambaye ndiye alikuwa kinara wa mabao ligi ya msimu uliopita (16) hadi sasa bado hajafungua akaunti ya mabao.

Mbali na wachezaji hao wengineo kadhaa kwenye kikosi cha Simba wamefunga bao moja moja wakiwemo Peter Banda, Mzamiru Yassin, Bwalya, Joash Onyango, Pape Ousmane Sakho, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Sadio Kanoute na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili wakiwa na pointi 24.


MBEYA CITY

Mbeya City msimu huu wamekuwa wa motoo hadi raha. Kufikia sasa, pacha yao yao ya ushambuliaji inayoundwa na Juma Liuzio (mabao 4), Richard Ng’ondya (mabao 4) na Paul Nonga (mabao 3), inatisha ikiwa tayari imefunga jumla ya mabao 11, huku mabao yanayomilikiwa na timu yakiwa ni 15. Yaani timu nzima ukiondoa watatu hao, imefunga mabao manne tu.

Mchango wao wa mabao unaiweka Mbeya City nafasi ya tano, ikiwa imekusanya pointi 16.


NAMUNGO FC

Japokuwa Namungo FC haijaanza vizuri msimu huu, mchango wa washambuliaji wao watatu Shiza Kichuya, Reliants Lusajo na Blaise Bigirimana unaonekana.

Lusajo ana mabao 5, Kichuya (2) na Bigirimana (bao 1), hivyo wamechangia jumla ya mabao nane kati ya 11 yanayomilikiwa na timu hiyo.


POLISI TANZANIA

Polisi Tanzania imeanza kwa kishindo msimu huu, ambapo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 17.

Safu yake ya ushambuliaji inaundwa na Vitalis Mayanga, Adam Adam na Tariq Simba, ambayo wamekuwa na mchango mkukwa kwenye katika timu hiyo.

Mayanga amefunga (mabao 5), Simba (bao 1) na Adam (bao 1), hivyo pacha hiyo imetengeneza jumla ya mabao saba kati ya 11 yanayomilikiwa na timu.


GEITA GOLD

Unapotaja kikosi cha Geita Gold hutoacha kumtaja mshambuliaji George Mpole ambaye anaongoza kwa mabao matano kwenye timu yake, akifuatia na Danny Lyanga anayemiliki mabao mawili huku Juma Mahadhi akiwa na moja alilolifunga dhidi ya Simba.

Pacha hiyo imetengeneza jumla ya mabao nane kati ya mabao 13 yanayomilikiwa na timu hiyo hivyo kuvuka zaidi ya nusu.


WASIKIE WADAU

Kocha wa Fountain Gate, Juma Masoud anasema: “Huenda msimu huu ukawa ni mzuri zaidi kwa wazawa maana ukiangalia unaona kabisa wamefanya vizuri mpaka sasa hivyo wana deni kwa Watanzania la kutuaminisha kuwa wanaweza zaidi ya wageni.”

Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma anasema licha ya wazawa kuuanza vyema msimu huu ila hawapaswi kubweteka bali kuongeza jitihada.

Advertisement