Usishangae haya yakitokea dirisha dogo

DIRISHA Dogo la usajili kwa msimu huu litafunguliwa Desemba 15 na kufungwa Januari 15 mwakani ambapo timu zitapata fursa ya kuimarisha vikosi vyao kusajili nyota wachache wa kurekebisha maeneo ambayo yameonyesha udhaifu.

Upo usajili ambao unategemewa kufanyika katika kipindi hicho cha usajili wa dirisha dogo lakini pia kuna yale ambayo huenda hayategemewi kutokea lakini mambo yakaja kinyume kulingana na hulka na mienendo ya soka letu.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya mambo ambayo mashabiki wa soka pengine wanapaswa kujiandaa nayo kisaikolojia kuona yakitokea katika dirisha dogo la usajili msimu huu japo katika hali ya kawaida hayaonekani yanaweza kutokea.


Okwi, Chama kurejea

Emmanuel Okwi kwa sasa anachezea Kiyovu ya Rwanda akiwa na mkataba wa mwaka mmoja wakati Clatous Chama anaitumikia RS Berkane ya Morocco kwa mkataba wa miaka miwili.

Hawa wote walitamba vilivyo wakiwa na kikosi cha Simba hadi pale walipoamua kuondoka lakini inawezekana dirisha dogo la usajili likawarudisha katika mojawapo kat ya klabu tatu kubwa nchini, Simba, Yanga au Azam.

Mkataba wa Okwi na Kiyovu unamruhusu kuondoka ikiwa atapata timu hivyo anaweza kuitumia fursa hiyo kuja Tanzania wakati Chama inadaiwa amekuwa hana furaha na maisha ya Morocco hivyo anataka kuvunja mkataba aweze kurejea nchini.


Yanga kusajili wageni wawili

Yanga ina nafasi mbili imesalia nazo za usajili wa wachezaji wa kigeni kwani katika dirisha kubwa la usajili ilisajili wageni 10 lakini kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaruhusu usajili wa wachezaji 12 wa kigeni huku wanaopaswa kutumika kwa mchezo mmoja ni wanane tu.

Haitokuwa jambo la kushangaza kwa Yanga ikiongeza vifaa viwili vingine vya kigeni ili kujazia nafasi ambazo imebakia nazo na huenda miongoni mwa hao akawa wa nafasi ya ushambuliaji.


Mastraika kugeuka dili

Tatizo la ubutu wa safu za ushambuliaji za timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara huenda likageuka neema kwa wachezaji wanaocheza katika nafasi ya ushambuliaji ambao bila shaka watasakwa kwa udi na uvumba na timu mbalimbali ili waimarishe safu zao za ushambuliaji.

Katika raundi tano za mwanzo, timu ambazo zimeonyesha ubutu uliokithiri katika safu zao za ushambuliaji ni KMC, Tanzania Prisons, Coastal Union na Mtibwa Sugar ambazo kila moja imefunga bao moja tu huku timu ya Geita Gold yenyewe ikifumania nyavu mara mbili tu.


DTB kuzoa mafaza Ligi Kuu

DTB FC ndio habari ya mjini katika Ligi ya Championship (zamani Daraja la Kwanza) kutokana na matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata yakichangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango bora kinachoonyeshwa na kundi kubwa la nyota wa timu hiyo waliowahi kuchezea timu tofauti za Ligi Kuu.

Kutokana na jeuri ya fedha ambayo DTB FC wanayo pamoja na mazingira mazuri ambayo imeyaandaa kwa ajili ya wachezaji wake, haitakuwa jambo la kushangaza kuona katika dirisha dogo la usajili ikinasa nyota wa timu za Ligi Kuu.


Mbeya Kwanza kuporwa mastaa

Ushindani ambao umekuwa ukionyeshwa na Mbeya Kwanza umezua gumzo kwa wadau na mashabiki wa soka nchini ambao wanahisi timu hiyo inaweza kufanya kile cha ndugu zao Mbeya City katika msimu wa 2013/2014 walipokuwa mwiba kwa timu nyingi za Ligi Kuu zikiwemo Simba na Yanga.

Lakini kama uongozi wa Mbeya Kwanza usipojipanga hasa kiuchumi, inaweza kuwapoteza baadhi ya wachezaji wake muhimu ambao wanaweza kufuata malisho mazuri zaidi.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Chrispin Ngushi ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga na kupiga pasi za mwisho.


Wawa kutupiwa virago

Tangu beki Pascal Wawa aliporuhusu bao la kizembe katika mechi ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mashabiki na wapenzi wa Simba wengi hawaonekani kumfurahia kwa sasa.

Haishangazi kuona benchi la ufundi la timu hiyo likimpiga benchi kwa sasa pengine kwa nia njema ya kumuepusha na presha na vitisho kutoka kwa mashabiki ambavyo vinaweza kuathiri ufanisi wake uwanjani.

Kwa hali ilivyo, beki huyo anaweza kujikuta anafunguliwa mlango wa kutokea katika dirisha dogo lijalo la usajili kwani tayari uhusiano wake na wengi ndani ya klabu hauko sawa.


Wadau wafunguka

Mratibu wa DTB FC, Muhibu Kanu alithibitisha kwamba wako kwenye mpango wa kuimarisha kikosi chao kwa kusajili baadhi ya nyota wa Ligi Kuu.

“Timu hadi sasa ipo katika muelekeo mzuri na kama mnavyoona tunaongoza msimamo wa ligi huku tukiwa hatujapoteza mchezo wowote na hii inathibitisha kwamba wachezaji wetu wana viwango vizuri na uzoefu wao umeendelea kutusaidia.

“Katika dirisha dogo tutaongeza baadhi ya wachezaji nyota wa timu za Ligi Kuu ambao tunaamini wataongeza nguvu kwa waliopo ili tuweze kutimiza malengo yetu ya kupanda daraja. Hawa waliopo ni wazuri lakini nao wanatakiwa kuongezewa nguvu na kuwafanya wapinzani wasitukariri,” alisema Kanu.

Mwenyekiti wa Mbeya Kwanza, Mohamed Mashango alisema kuwa timu ambayo inamhitaji mchezaji wake yeyote inapaswa kufuata taratibu.

“Wachezaji wetu wote wana mikataba ya kuitumikia timu hii lakini hatuwezi kuwazuia iwapo wanapata malisho mazuri zaidi. Kama kuna timu inahitaji mchezaji wetu, ilete maombi rasmi mezani na kama itafikia dau tunalotaka tutawauzia,” alisema Mashango.