Prime
Usajili wa Fei Toto… Zilongwa mbali, zitendwa mbali
ZILONGWA mbali zitendwa mbali ni msemo wa Kizaramo wenye maana ya 'maneno mbali na vitendo mbali' yaani yanayosemwa ni tofauti kabisa na yanayofanyika.
Hivi ndivyo ilivyo kwenye suala la uhamisho unaotajwa zaidi hapa nchini - wa Feisal Salum maarufu kama Fei Toto. Kila siku kuna habari mpya kumhusu mchezaji huyu wa Azam FC.
Kila mchambuzi wa michezo, kila mwandishi wa michezo, kila mwanamtandao wa michezo, kila gazeti la michezo na hata kila kipindi cha michezo habari kuu ni uhamisho wa Fei Toto.
Hakuna anayejadili kuhusu Fei Toto kuendelea kubaki Azam...kila mtu anajadili kuhama kwake kutoka Azam. Leo wanasema Fei Toto ameshamalizana na Yanga, kesho watasema ameshamalizana na Simba...wanamzungusha hapohapo kila siku.
Angalau zamani kulikuwa na stori za Kaizer Chiefs kwa sababu ya Nasreddine Nabi ambaye ni kama baba yake. Na pia kukawa na stori ya Wydad kwa sababu ya Rhulani Mokoena aliyewahi kunukuliwa akisema anampenda sana Fei Toto.
Lakini sasa stori za Kaizer Chiefs na Wydad hazipo tena - ni Yanga na Simba, basi. Watu walewale ambao leo watajadili Fei Toto ameshamalizana na Yanga, kesho watakuja na habari nyingine kwamba ameshamalizana na Simba.
Mbaya zaidi hawazisemi habari hizi kama tetesi bali wanazisema kama taarifa zilizokamilika...na watu wanawaamini.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna klabu yoyote katika zinazotajwa ambayo imeshawahi kupeleka ofa Azam kwa ajili ya Fei Toto.
Taarifa za ndani kutoka Azam wenye mchezaji, na Simba na Yanga wanaohusishwa zinasema hakuna mawasiliano yoyote baina yao. Hakuna klabu iliyowahi kutuma ofa Azam wala angalau kuulizia tu upatikanaje wake. Yaani kwa kifupi hakuna klabu iliyoonyesha nia na uthubutu wa angalau kuulizia bei.
Haya yote yanayosemwa mitandaoni hayana ukweli hata kidogo ndio hapo unapokuja ule msemo wa Kizaramo "zilongwa mbali na zitendwa mbali".
Japo katika ngazi za ndani Simba na Yanga wote wamekuwa wakimjadili mchezaji huyo na kuna uwezekano mkubwa sana kwamba wamekuwa wakiwasiliana naye, lakini hakuna aliyepiga hodi Chamazi. Kila mmoja kabaki na matamanio yake ndani nafsini - anakufa Kijerumani na tai shingoni.
Katika hali ya kawaida hakuna timu ya Tanzania inayoweza kumtoa Fei Toto pale Azam katika wakati huu akiwa na mkataba wake.
Kitu pekee wanachoweza kufanya ni kusubiri mkataba wake uishe wampate kama mchezaji huru na hiyo ni hadi msimu ujao. Na hii ni kwa sababu gharama za kumpata kwa sasa ni kubwa mno.
Mkataba wa Fei Toto na Azam una kipengele ambacho kimeshaweka bei ya mchezaji ambayo ni Dola 500,000 za Marekani. Hii ni zaidi ya Sh1.2 bilioni. Hakuna klabu Tanzania yenye uwezo wa kutoa fedha hizo kununua mchezaji mmoja.
Na hata kama itakuwepo itabidi iandae bajeti kubwa zaidi ya hiyo maana kuna pesa ya kumpa mchezaji mwenyewe (signing bonus) ambayo haipungui Sh500 milioni. Na hii ni kwa Yanga, lakini kwa Simba ambayo inahusishwa zaidi gharama ni kubwa zaidi.
Wakati Yanga wanamuuza Fei Toto kwenda Azam waliweka kipengele kwenye mkataba wa mauziano kinachotaka Yanga kupewa Sh1 bilioni endapo Azam itamuuza Fei Toto kwenda Simba.
Hii ina maana kwamba ili Simba wauziwe Fei Toto na Azam itabidi klabu hiyo wawape Yanga Sh1 bilioni. Sasa hebu fikiria Azam watamuuza Fei Toto kwa shilingi ngapi kwenda Simba ili wapate Sh1 bilioni ya kuwapa Yanga na wao wabaki na chenji.
Azam sio wajinga eti wamuuze kwa Sh1 bilioni kamili halafu yote wawape Yanga na wao wabaki patupu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa klabu hiyo, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi' hata kugawana sawa kwa sawa na Yanga hawapo tayari. Yaani labda wamuuze kwa Sh2 bilioni, halafu Sh1 bilioni wawape Yanga na wao wabaki na Sh1 bilioni -hawataki.
Wanataka wao wapate pesa nyingi zaidi ya Yanga kwa sababu ndio waliomuongezea thamani mchezaji huyo. Kwa hiyo labda Simba watoe ofa ya Sh2.5 bilioni, kwamba Azam wabaki na bilioni moja na nusu halafu Sh1 bilioni wawape Yanga. Simba wanaweza kutoa hiyo pesa? Ama kwa hakika zilongwa mbali, zitendwa mbali...!