Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna nini Tuzo za NBC?

MSIMU wa soka wa mwaka 2025/26 umemalizika kwa mechi ya fainali ya Kombe la CRDB lililochukuliwa na Simba SC huku ubingwa wa Tanzania Bara uikirejea Jangwani kwa Yanga SC.

Kwa kawaida kisindikizio cha kumalizika kwa msimu ni sherehe ya kutuza au kuenzi wachezaji, makocha, timu na wadau wengine walioonyesha kiwango kizuri, mchango wao katika mchezo na mambo mengine.

Si sherehe ya lazima kuifanya lakini ni muhimu sana kwa kuwa huonyesha wachezaji, mashabiki, makocha na wadau wengine waliofanya vizuri msimu ulioisha ni kina nani na hivyo inakuwa ni kama kuwaelekeza wanatakiwa wafanye nini wafikie mafanikio hayo.

Sehemu nyingine, taasisi ambazo hujihusisha na mchezo huo kama vyombo vya habari, huendesha shughuli hiyo ya kuenzi waliofanya vizuri. Hata tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia (Ballon d’Or) haikuanzishwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), lakini baadaye chombo hicho kikaungana na gazeti kuendesha tuzo hiyo.

Huu unaelekea kuwa msimu wa pili bila ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Bodi ya Ligi (TPLB) kuendesha tuzo hizo baada ya mwaka juzi kuzisogeza mbele hadi mwanzoni mwa msimu unaofuata.

Siyo TFF wala TPLB ambayo ilitoa taarifa kuhusu kutofanyika kwa tuzo za mwaka jana. Na hata mwaka juzi walitoa taarifa baada ya wadau kuanza kuuliza kunani.

Na hadi sasa, vyombo hivyo viwili havijatoa taarifa ya kufanyika au kutofanyika kwa tuzo hza mwaka huu baada ya Ligi Kuu, inayodhaminiwa na NBC, kuhitimishwa yakriban wiki mbili zilizopita.

Haieleweki kama tatizo ni mamlaka hizo mbili za soka nchini au ni wadhamini, lakini kikubwa ni tuzo hizo ni bidhaa ya TFF na hivyo hata kama wadhamini wana matatizo ni jukumu la TFF kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika kuenzi waliofanya vizuri ili kuendelea kuitunza bidhaa yake na kuipa thamani.

Kutofanyika kwa tuzo hizo kunaweza kuibua hisia chanya au hasi kwa kuwa watu wanaweza kudhani waandaaji hawataki kuendesha sherehe za msimu husika kwa sababu wanaona wachezaji waliowalenga kutwaa tuzo hizo hawakufanya vizuri na hivyo kuwatangaza ni kuwapendelea.

Zinaweza kuwa fikra za kijinga lakini zikilinganishwa na hali halisi zinaongezewa nguvu na kuonekana za ukweli maana hali halisi inaonyesha waliodhaniwa wangeshinda wamechemsha.

Pia zinashusha thamani kwa waandaaji. Mtazamo wa wadhamini au wanaotaka kuwa wadhamini kwa waandaaji unakuwa hasi kwa kuwa wanaona watu wanaotaka kuwakabidhi fedha ili waendeshe shughuli hiyo hawatabiriki.

Moja ya sifa za uadilifu ni kutabirika. Kwamba mtu anajua fulani huwa anahakikisha jambo lake linafanyika, hata kama mazingira ni magumu. Lakini mtu akishajenga fikra kuwa fulani anaweza afanye au asifanye jambo lake, hataweza kufanya biashara naye kwa kuwa hatabiriki.

Hili ni jambo ambalo TFF ilitakiwa ihakikishe inalifanya. Inajenga fikra za kuaminika kwa wadau wake kwamba ikitangaza itafanya jambo, basi ni lazima lifanyike.

Pale inaposhindikana kabisa, basi juhudi kubwa hufanyika kuwataarifu wadau kuwa hakutakuwa na jambo hilo kwa sababu itakazoziweka bayana ili kujenga Imani kwao kwamba kulikuwa na nia ya dhati lakini mazingira yalikuwa magumu kulitekeleza.

Hata hivyo, siku hizi si lazima taasisi ifanye yenyewe kila jambo ndiyo maana unakuta Fifa hukodisha kampuni kama za masoko kufanya kazi zake badala ya wafanyakazi wake. Hivyo si vibaya kama TFF na Bodi ya Ligi wakaona umuhimu wa kukabidhi baadhi ya bidhaa zake kwa kampuni binafsi ili ziweke weledi wake na kazi ya shirikisho iwe ni kuhakikisha kuwa utendaji ulifanyika kwa kadiri ya misingi ya TFF na mpira wa miguu.

Ni wakati wa kuanza kufanya kazi kisasa zaidi badala ya kukumbatia kila kitu, hata kile ambacho shirikisho halina ujuzi wa kutosha. Kampuni za uandaaji na uendeshaji matukio ziko nyingi na zinafanikisha shughuli za taasisi kubwa nchini.

Hizi ni kampuni ambazo zinaweza hata kuongeza thamani ya tukio likawa kubwa zaidi na kuvutia kampuni nyingi kuongeza udhamini na hivyo tukio hilo kubeba taswira inayostahili.