UJANJA KUWAHI: Mastaa wa maana unaoweza kuwanasa bure Juni 2026
Muktasari:
- Badala yake, kuna timu nyingi zinaelekeza macho kwenye soko la wachezaji wa bure na uwezekano wa kuweka msingi wa kumsajili mchezaji muhimu bila kulipa ada yoyote ya uhamisho.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA la usajili la Januari limekuwa kipindi cha matumizi madogo katika soka la kisasa, huku klabu kubwa zikihifadhi pesa kwa matumizi makubwa zaidi majira ya joto.
Badala yake, kuna timu nyingi zinaelekeza macho kwenye soko la wachezaji wa bure na uwezekano wa kuweka msingi wa kumsajili mchezaji muhimu bila kulipa ada yoyote ya uhamisho.
Kwa sasa, kuna majina makubwa kadhaa ambayo yanaweza kupatikana bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi yajayo.
Ingawa hakutakuwa na shughuli nyingi za haraka mwezi huu, nyuma ya pazia, wakurugenzi wa michezo na wataalamu wa usajili watakuwa wakifuatilia fursa za soko la baadaye.
Kwa uwezekano mkubwa, macho yao yataelekezwa kwa wachezaji ambao mikataba yao imesalia na miezi sita pekee kufika ukingoni.
Baada ya kubaki kwenye klabu zao majira ya joto yaliyopita huku nafasi ya kuingiza ada kubwa ya uhamisho ikipotea, nyota kadhaa wanaotamaniwa wameingia kwenye hatua za mwisho za mikataba yao, hivyo watapatikana bure kabisa kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2026.
Je, ni mastaa gani zinazoweza kuwaokota bure na kuwapeleka kwenye timu wakati wa dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu?
Ibrahima Konate (Liverpool)
Liverpool inaonekana kutokuwa na hofu kubwa tena ya kumpoteza Ibrahima Konate bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, hasa kutokana na kushuka kwa kiwango cha beki huyo wakati wa mwanzo dhaifu wa msimu wa 2025-26 katika jitihada zao za kutetea taji.
Baada ya kuwa nguzo muhimu katika ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa amefanya makosa kadhaa makubwa msimu huu yaliyochangia matatizo ya jumla ya mabingwa hao. Atakuwa huru mwisho wa msimu na timu zitapata fursa ya kumbeba bure kabisa.
Bernardo Silva (Man City)
Bernardo Silva amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka Manchester City kwa miaka kadhaa, huku Barcelona na Benfica zikitajwa mara kwa mara.
Sasa, huenda wakati wake umefika anapoingia kwenye miezi ya mwisho ya mkataba wake huko Etihad.
Akiwa mmoja wa wachezaji walioaminiwa sana na Pep Guardiola, Silva mwenye umri wa miaka 31 si chaguo la uhakika tena kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ujio wa wachezaji vijana wengi wa kushambulia.
Bado ana mengi ya kuchangia, hasa katika ligi zisizo na kasi kubwa zinazothamini zaidi ufundi wa mpira.
Antonio Rudiger (Real Madrid)
Kuna maswali mengi kuhusu mustakabali wa Antonio Rudiger huko Real Madrid chini ya kocha Xabi Alonso.
Ilidaiwa majira ya kiangazi yaliyopita kuwa klabu haina mpango wa kumwongezea mkataba, kutokana na wasiwasi wa kiwango chake na afya ya muda mrefu.
Hofu hizo zilionekana kuthibitishwa alipoumia misuli ya paja na kukaa nje miezi mitatu kuanzia Septemba.
Hata hivyo, ameanza mechi tano mfululizo za La Liga tangu arejee, ingawa ripoti zinaonyesha kuwa Alonso hampi nafasi ya muda mrefu na mwisho wa msimu atapatikana bure.
John Stones (Man City)
John Stones amekuwa mtumishi mwaminifu wa Manchester City kwa karibu muongo mmoja, lakini majeraha yamekuwa yakimsumbua muda mrefu.
Baada ya kurejea uwanjani msimu huu, alikuwa akipata nafasi chache kabla ya kupata jeraha la paja Desemba.
Lakini, staa huyo mkataba wake huko Etihad utafika tamati mwishoni mwa msimu, hivyo dirisha la kiangazi kama hatakuwa amesaini mkataba mpya, basi ataondoka bure.
Leon Goretzka (Bayern Munich)
Baada ya kuonekana kama angeondoka, Leon Goretzka amerejea kwenye kikosi cha kwanza chini ya kocha Vincent Kompany.
Hata hivyo, mustakabali wake bado una mashaka anapoingia miezi ya mwisho ya mkataba wake, huku Bayern Munich ikianza kumtafuta mrithi wake.
Ripoti zinaonyesha klabu imeamua kutompa mkataba mpya licha ya kurejea kwa kiwango kizuri.
Manchester United imetajwa mara kwa mara inataka saini yake na huenda ikaipata bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Serge Gnabry (Bayern Munich)
Serge Gnabry mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akipanda na kushuka kutokana na majeraha.
Hata hivyo, alianza msimu mpya kwa kiwango bora, akichangia mabao tisa katika mechi 12 za Bundesliga.
Hilo limemfanya kurejea kwenye mipango ya klabu, na sasa anaripotiwa kupewa ofa ya mkataba mpya wa miaka miwili baada ya huu wa sasa kufika ukingoni mwa msimu huu.
Na kama hakuwa na dili jipya mezani, hivyo Gnabry atakuwa huru kunaswa bure mwisho wa msimu.
Mike Maignan (AC Milan)
Hali ya mkataba wa Mike Maignan inaibua maswali mengi. Ingawa aliripotiwa kukubaliana kwa maneno kuongeza mkataba mapema 2025, bado hakuna taarifa rasmi.
Inadaiwa kuwa mabadiliko ya uongozi na wasiwasi wa kiwango chake yamesababisha kuchelewa.
Alikuwa karibu kujiunga na Chelsea kabla ya Kombe la Dunia la Klabu, lakini makubaliano hayakufikiwa.
Sasa anaweza kuanza mazungumzo na klabu za nje, huku Chelsea ikitajwa kurejea tena.
Ruben Neves (Al-Hilal)
Ruben Neves aliondoka Wolves akiwa kileleni na kujiunga na Al-Hilal mwaka 2023. Baada ya misimu miwili mizuri, sasa yuko kwenye miezi ya mwisho ya mkataba wake baada ya kukataa kuongeza mkataba wenye mshahara mkubwa.
Anatajwa kuwa tayari kupunguza mshahara ili kurejea Ulaya, huku Manchester United na Porto zikitajwa kama sehemu ambazo anaweza kwenda kujiunga kwa uhamisho wa bure kabisa.
Marc Guehi (Crystal Palace)
Baada ya drama za mwisho za dirisha la majira ya joto, Marc Guehi alibaki Crystal Palace.
Liverpool ilikuwa karibu kumsajili baada ya makubaliano ya ada ya Pauni 35 milioni, lakini Palace walifuta dili dakika za mwisho kwa kukosa mbadala.
Liverpool bado inaonekana kuwa mbele, lakini Bayern Munich pia wameanza mazungumzo, jambo linaloweza kuwalazimisha Liverpool kulipa ada Januari, la ataondoka bure kabisa dirisha la majira ya kiangazi.
Dayot Upamecano (Bayern Munich)
Upamecano ameimarika sana chini ya Kompany na ameunda ushirikiano imara na Jonathan Tah.
Ingawa mkataba wake una miezi sita tu, anaripotiwa kuwa kwenye mazungumzo ya juu ya kuongeza mkataba hadi 2030.
Isipokuwa mabadiliko ya ghafla, ataendelea kubaki Bayern. Hata hivyo, kwenye soka chochote kinaweza kutokea na kama hakutakuwa na dili jipya ubaoni, basi beki huyo wa kati anaweza kufungua milango ya kuondoka Allianz Arena bure kabisa wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.