Uchawi wa Simba ndio huu
Muktasari:
- Mabosi hao chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji waliamua kusafisha kikosi kwa kuwatema wale walioonekana kuwa na umri mkubwa na waliokuwa wanamaliza mikataba yao na wengine ambao walioshindwa kuonyesha makali.
SIMBA ina misimu mitatu mfululizo bila kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho, jambo lililowafanya mabosi wa klabu hiyo kukuna vichwa na kusuka upya michongo yao kuanzia kikosi hadi benchi la ufundi.
Mabosi hao chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji waliamua kusafisha kikosi kwa kuwatema wale walioonekana kuwa na umri mkubwa na waliokuwa wanamaliza mikataba yao na wengine ambao walioshindwa kuonyesha makali.
Kisha fasta wakaleta majembe mapya wakiwamo wachezaji 15, wakiwamo tisa wa kigeni ambao ni Joshua Mutale, Steven Mukwala, Charles Ahoua, Augustine Okejepha, Valentin Nouma, Chamou Karabou, Moussa Camara, Leonel Ateba na Debora Mavambo, huku wazawa wakiwa sita akiwamo Awesu Awesu, Omar Omar, Abdulrazak Hamza, Valentino Mashaka, Yusuf Kagoma na Kelvin Kijili.
Lakini wakati huo Mo Dewji na wenzake wakalitengeneza benchi jipya la ufundi, likiwa chini ya Msauzi Fadlu Davids ambaye akishirikiana na wenzake kambini jijini Ismailia, Misri waliitengeneza timu kibabe na fasta wakarudi nchini na muda mchache maajabu yameanza kuonekana kwa timu hiyo kufanya vizuri.
Licha ya kuanza na kupigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kutema taji hilo, lakini Simba imeonyesha kuimarika zaidi katika mechi tatu zilizofuata za mashindano ikiwamo ile ya kusaka mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union iliyoichapa 1-0.
Ikashinda pia mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara kwa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United na kuichapa Fountain Gate kwa mabao 4-0 na kuifanya iongoze msimamo kwa pointi sita na mabao saba huku ikiwa haijaruihusu bao lolote hadi sasa ikiwa ni mara ya kwanza tangu 2017 kucheza mechi mbili za ligi na kuvuna idadi kubwa ya mabao na yenyewe kutohusu bao.
Licha ya kucheza soka tamu, lakini Simba imeonekana kuwa na stamina pamoja na pumzi za kutosha uwanjani, sambamba na kuwanyima raha mabeki wa upinzani kutokana na kushambulia kwa akili mwanzo mwisho ikielezwa hiyo yote imetokana na kuwa na uchawi mpya wa Kisauzi.
Mwanaspoti linakuletea siri ya ‘uchawi’ huo mzima wa Simba kuanza kwa kasi msimu huu, ikiwa ni ukubwa wa benchi lenye vichwa vya watu makini chini ya Fadlu ambaye amerejesha matumaini ya mashabiki wa klabu hiyo katika kumaliza ubabe wa Yanga iliyokumbatia mataji kwa misimu mitatu mfululizo.
Kama hujui benchi hilo la ufundi lina watu 14 kutoka mataifa tofauti waliopania kushirikiana an wachezaji kuiwezesha Simba kunyakua taji la 23 msimu huu, kwani ndio dhamira kuu ya uongozi wa Simba mbali na kuhakikisha inafika mbali katika michuano ya kimataifa ikianzia raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho.
Fadlu Davids - Kocha Mkuu
Huyu ndiye bosi wa benchi la ufundi la Simba, amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea kwa mabingwa wa soka wa Morocco, Raja Club Athletic maarufu Raja Casablanca alipokuwa kama kocha msaidizi. Raia huyo wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 43, amechukua mikoba ya Mualgeria Abdelhak Benchikha.
Mbali na Raja Casablanca, Fadlu pia amewahi kupitia timu mbalimbali akiwa kocha msaidizi pia akifanikiwa kuwa kocha mkuu. Timu hizo ni Maritzburg United, Orlando Pirates, Chippa United na Bloemfontein Celtic zote za Afrika Kusini na Lokomotiv Moscow ya Urusi. Ni kocha anayesifiwa kwa kupenda kushambulia kwa kasi na kujilinda kwa pamoja sambamba na kupenda zaidi damu changa na bahati nzuri asilimia kubwa ya Simba ya sasa imejaa vijana wengi.
Darian Wilken - Kocha Msaidizi
Wakati Fadlu anatambulishwa ndani ya Simba, alikuwa na wenzake wanne mmojawapo ni Darian ambaye naye ni raia wa Afrika Kusini. Ndani ya kikosi cha Simba, Darian ndiye kocha msaidizi wa kwanza, hufanya kazi kwa ukaribu na kocha mkuu ili kusaidia kuboresha ujuzi wa wachezaji.
Msauzi huyu ametoka na Fadlu pale Raja Casablanca akiwa pia amewahi kupita timu za Maritzburg United, Orlando Pirates na Amazulu. Inavyoonekana ni mtu wa karibu sana na Fadlu kwani wamekuwa pamoja katika takribani timu tano sasa.
Mara kadhaa Darian amekuwa bize kuwafuatilia wapinzani wanachokifanya katika ‘warm up’ kabla ya mechi na hiyo inaelezwa imekuwa silaha ya Fadlu kufahamu namna wapinzani wao wataianza mechi kwa mtindo gani.
Seleman Matola - Kocha Msaidizi
Huyu ni mzawa, amekuwa ndani ya Simba kwa muda mrefu, pia ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo. Yeye ni kocha msaidizi wa pili baada ya Darian.
Matola amekuwa akisimamia mazoezi kabla ya mechi huku akifanya kazi kwa ukaribu na msaidizi mwenzake kwa kushirikiana na kocha mkuu. Wakati Darian akiwa bize kuwafuatilia wapinzani, Matola anabaki na wachezaji wake kuwaimarisha kabla ya mechi sambamba na Fadlu.
Wayne Sandilands - Kocha wa Makipa
Huyu ni kipa wa zamani wa Supersport United, Platinum Stars, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates zote za Afrika Kusini. Naye amekuja sambamba na Fadlu katika kuimarisha benchi la ufundi. Wayne ni raia wa Afrika Kusini akiwa na jukumu kubwa la kuwanoa makipa wa Simba.
Kocha huyu mjanja sana, anapowafundisha makipa wake kwenye uwanja wa mazoezi anaenda kuangalia mienendo yao wakati wa mechi. Katika kufanikisha hili amekuwa akiweka kamera nyuma ya goli lao inayorekodi matukio muda wote, kisha baada mchezo anafahamu namna ambavyo kipa wake amekifanya siku hiyo ili kumpa mbinu bora zaidi za kuimarisha kiwango chake. Naye alikuja sambamba na Fadlu.
Riedoh Berdien - Kocha wa viungo
Wakati kocha msaidizi akiwa na jukumu la kusimamia mazoezi ya wachezaji, kwa upande wa kocha wa viungo kazi yake ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa na hali nzuri kimwili na uwezo bora wa kufanya kazi. Wakati mwingine anashiriki katika kupanga aina ya vyakula ambavyo vinaweza kumsaidia mchezaji kutopata madhara anapofanya mazoezi na kuimarisha uwezo wake.
Riedoh si mgeni katika ardhi ya Tanzania kwani awali alikuwa akifanya majukumu yake ndani ya kikosi cha Yanga. Ni raia wa Afrika Kusini akiwa amekuja sambamba na Fadlu.
Mueez Kajee - Mchambuzi
Msauzi mwingine ndani ya benchi la ufundi la Simba akiwa amekuja sambamba na Fadlu. Jukumu lake ni kusaidia timu kuboresha utendaji wao kupitia uchambuzi wa video za mechi ili kumpa mwanga kocha mkuu namna ya kufanya kikosi kiwe bora zaidi lakini pia kufanya tathimini viwango vya wachezaji. Pia katika uchambuzi wake wa video za wapinzani anaangalia mifumo na jinsi wanavyocheza ili kumrahisishia kazi kocha mkuu katika ufundishaji wake.
Culvin Mavhunga - GPS Tracking
Awali, alikuwa na majukumu ya kuwa mchambuzi wa video ndani ya Simba, lakini baada ya ujio wa Mueez Kajee, Mavhunga amepewa majukumu mapya ambayo hivi sasa atakuwa GPS Tracking. Huyu ni raia wa Zimbabwe akiwa na timu hiyo tangu msimu uliopita.
Msimu huu Simba wameamua kuwa ‘siriazi’ sana kwani wachezaji wanapokuwa mazoezini au kwenye mechi, kuna vifaa maalum wanavaa ambapo Mavhunga ana jukumu la kufuatilia mienendo ya wachezaji uwajibikaji wao uwanjani kwa kutumia vifaa maalum, ikiwemo mikimbio na nguvu iliyotumika, kujua utimamu wao wa mwili.
Durell Butler - Mtaalamu wa Recovery
Huyu ameongezwa ndani ya timu hivi karibuni akiwa ni chaguo la kocha Fadlu. Naye ni raia wa Afrika Kusini akiwa na jukumu la kuwasaidia wachezaji kurudi katika utimamu wa mwili hasa kwa wale wanaotoka katika kuuguza majeraha. Lakini pia amekuwa akishirikiana na kocha wa viungo kuandaa program za mazoezi kwani majukumu yao kwa namna moja ama nyingine yanafanana.
Edwin Kagabo - Daktari
Katika kitengo cha tiba, huyu ni kama bosi wao akiwa na jukumu la kuwatibia wachezaji wanapopata majeraha. Yeye amekuwa ndani ya Simba kwa muda mrefu tangu mwaka 2022 akifanya majukumu hayo. Ni mzawa.
Hamis Kimweri - Mchua Misuli
Anaingia kwenye kitengo cha tiba ndani ya Simba akiwa na jukumu la kuiweka sawa misuli ya wachezaji inapopata changamoto, lakini pia hata wakati mwingine anamchua mchezaji misuli yake ili kuzuia asipate madhara katika utendaji wake wa kazi. Naye ni mzawa.
Wycliffe Omom - Mtaalamu wa Tiba ya Viungo (Physiotherapist)
Ni raia wa Kenya, yupo Simba tangu msimu uliopita akiwa na jukumu la kusimamia mienendo majeruhi ndani ya timu. Mchezaji akitoka kupatiwa matibabu, kwanza anakabidhiwa kwake kumuweka sawa kabla ya mambo mengine kuendelea katika uwanja wa mazoezi.
Hamis Mtambo - Mtunza Vifaa
Zaidi ya misimu saba yupo ndani ya Simba akifanya majukumu ya kutunza vifaa vya mazoezi kama mipira, koni na bips kuhakikisha kila kitu kinakuwa katika mpangilio wake. Naye ni mzawa.
Patrick Rweyemamu - Meneja
Aliwahi kuwa kwenye majukumu hayo hapo awali kabla ya kupelekwa kwenye program za soka la vijana na sasa amerejeshwa akiendelea na majukumu yake ya kiutawala. Unaweza kusema ndiye kiunganishi cha benchi la ufundi, wachezaji na uongozi wa klabu.
Meneja wa timu pia ana jukumu la kuweka sawa safari za timu. Ni mzawa.
Abass Ally - Mratibu
Majukumu yake anayafanya kwa ukaribu sana na meneja wa timu katika kuhakikisha mambo ya ndani na nje ya uwanja yanakwenda vizuri. Majukumu yake mara nyingi yanahusisha kuratibu shughuli za timu kama safari na kuwa kiunganishi cha benchi la ufundi, wachezaji na viongozi. Mara nyingi amekuwa akitumika kufika mapema katika kituo cha mechi kabla ya timu haijawasili ili kwenda kuweka mipango sawa ya timu kufikia. Ni mzawa pia.
MSIKIE PAWASA
Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, amesema anavyoliona benchi la ufundi la timu hiyo, anaamini kuna kitu kinakwenda kutokea msimu huu.
“Simba wamepata benchi zuri la ufundi likiongozwa na kocha Fadlu, ni kocha mzuri ambaye anahitaji apewe muda kuifanya kazi yake.
“Katika timu yoyote ile ambayo ni kama inaanza upya ili ije kukaa sawa vile inavyotakiwa inatakiwa kuchukua wiki kumi mpaka 12 kwa maana hiyo Simba inapitia kipindi hicho ili kutengeneza muunganiko unaowahusu wachezaji ambao asilimia kubwa kila mmoja ametoka katika timu akiwa na falsa ya mwalimu mwingine na sasa amekutana na mwalimu mwingine.
“Imani yangu ni kwamba benchi la ufundi lililopo msimu huu linaweza kuifanya Simba kuwa na matokeo mazuri kama wakipewa muda wa kufanya hivyo,” alisema Pawasa ambaye alikuwepo katika kikosi cha Simba kilichoitoa Zamalek mwaka 2003 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kufuzu hatua ya makundi.