SIO ZENGWE: Uamuzi wa Omary Kaya ndio uwajibikaji unaotakiwa sasa

Muktasari:
- Kama ilivyotarajiwa, Azam FC ilimtimua kocha mkuu, Yousouph Dabo na benchi lake lote la ufundi baada ya timu hiyo kushindwa kufurukuta mbele ya APR ya Rwanda katika mechi za raundi ya kwanza ya michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
WIKI tuliyoimaliza tulishuhudia makocha wengine wawili wakiondolewa katika klabu zao baada ya matokeo mabaya kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.
Kama ilivyotarajiwa, Azam FC ilimtimua kocha mkuu, Yousouph Dabo na benchi lake lote la ufundi baada ya timu hiyo kushindwa kufurukuta mbele ya APR ya Rwanda katika mechi za raundi ya kwanza ya michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Azam ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, na wiki moja baadaye ikakubali kichapo cha mabao 2-0 jijini Kigali na hivyo kuaga mashindano hayo kwa jumla ya mabao 2-1.
Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Azam kushiriki mashindano hayo makubwa Afrika kwa ngazi ya klabu. Mara ya kwanza ilishiriki baada ya kutwaa ubingwa wa Bara mwaka 2014 na safari hii ilipata tiketi kwa kushika nafasi ya pili. Kutokana na Tanzania kuwa katika nchi 12 bora Afrika, ina nafasi ya kupeleka timu mbili katika Ligi ya Mabingwa na nyingine mbili Kombe la Shirikisho.

Kati ya timu sita zilizowakilisha Bara na Zanzibar kwenye mashindano ya klabu Afrika, ni Yanga na Simba tu ndio zimesalia. Timu nyingine zilizoshiriki ni Coastal Union, Uhamiaji ya Zanzibar na JKU (Zanzibar).
Kocha mwingine aliyekumbwa na kimbunga cha timuatimua ni Mwinyi Zahera. Namungo ilimtupia virago baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za mwanzo za Ligi Kuu kwenye uwanja wake wa nyumbani, kikiwepo kipigo cha mabao 2-0 walichopewa na Singida Fountain Gate katikati ya wiki iliyopita.
Hayo yamekuja wiki moja baada ya Coastal Union kumtimua kocha wake David Ouma kutoka Kenya. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Coastal kupata kipigo cha mabao 3-0 mbele ya Bravos do Maquis katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho. Coastal imetolewa kwenye mashindano hayo kwa jumla ya mabao 3-0.
Ouma ndiye anahusishwa na mafanikio ya Coastal kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.
Mijadala mingi imejikita juu ya kutimuliwa kwa makocha hao na rekodi zao kwenye klabu hizo kabla ya kutimuliwa, na baadhi kuhoji kwa nini viongozi nao hawatimuliwi?

Lakini katika hilo yuko shujaa mmoja, Omary Kaya, ambaye alijitoa muhanga baada ya matokeo mabaya ya Namungo na kuamua kuwasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake wa mtendaji mkuu wa klabu, kuonyesha kuwajibika kama kiongozi.
Ni kweli! Ni nadra sana kwa kiongozi kuwajibika kwa matokeo ya uwanjani. Viongozi hutumia nguvu nyingi kuonyesha kuwa wamefanya jitihada kubwa na kuwapa makocha kila kitu, lakini wataalamu hao hawakuwapa matokeo yanayolingana na jitihada za uongozi.
Wapo pia ambao huhamishia shutuma au lawama kwa wachezaji kwamba walisaliti au kuhujumu katika mechi muhimu ndio maana timu ikashindwa kupata mafanikio.
Ni rahisi sana kwa viongozi kusikilizwa hoja zao, hasa zinapobebwa na wapambe wao na kuzieneza kwa mashabiki ili ionekane mwenye tatizo ni kocha au mchezaji.

Hilo halikuwa hivyo kwa kiongozi huyo kijana ambaye aliwahi kushika nafasi nyeti kama hiyo kwenye klabu ya Yanga wakati ikiwa imempoteza mdhamini na mwenyekiti wake wa zamani, Yusuf Manji na hivyo klabu kuendeshwa kwa misaada ya wanachama.
Uamuzi wa Kaya umeonyesha ukomavu na uthubutu wa kuchukua uamuzi kama huo wa kuwajibika kwa matokeo mabovu, hata kama hakuhusika moja kwa moja kama kocha anayeandaa timu, au mchezaji anayetekeleza maelekezo ya mwalimu uwanjani.
Uamuzi wa Kaya kuachia ngazi ni jibu tosha kwa wale walioanza kuhoji sababu za viongozi pia kutowajibika na kuwawajibisha makocha pekee. Uamuzi huo pia ni mfano kwa viongozi wengine kwamba si lazima ushiriki moja kwa moja katika matokeo mabaya, bali kuonyesha kwa namna moja au nyingine unaweza kuwa sababu ya timu kutofanya vizuri kutokana na nafasi yako.
Huu ni utamaduni ambao haujawahi kuzoeleka, si tu katika mpira wa miguu, bali hata nyanja nyingine hapa Tanzania. Ni lazima na ni muhimu kuwa na watu wa aina ya Kaaya ili kujenga utamaduni wa uwajibikaji ambao utarejesha nidhamu ya kazi na umakini ambao unaweza kuinua kiwango cha uendeshaji wetu wa klabu za soka na kuzalisha matokeo mazuri uwanjani.

Omary Kaya anastahili kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine wote wa mpira wa miguu na michezo mingine kama riadha, ngumi, judo na kuogelea ambayo mwaka huu ilifanya vibaya kwenye Michezo ya Olimpiki 2024 jijini Paris, lakini si makocha wala viongozi walioguswa na kuamua kuwajibika.
Hata wale wanaoandaa tuzo za wanamichezo bora wa mwaka, hawana budi kufikiria tuzo ya heshima kwa kiongozi anayejiwajibisha kama Kaaya kwa lengo la kuchochea uwajibikaji.