UCHAMBUZI: Tumepigwa kibao, hakijageuka bado

Muktasari:

WIKIENDI hii, Liverpool na Manchester United zinapambana katika mechi ambayo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne iliyopita, United wanapewa nafasi zaidi kushinda.

WIKIENDI hii, Liverpool na Manchester United zinapambana katika mechi ambayo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne iliyopita, United wanapewa nafasi zaidi kushinda.

Katika miaka minne iliyopita, katika maeneo tofauti ndani ya uwanja, United ilikuwa na wachezaji wazuri lakini haikuwahi kuwa na timu nzuri ya kupambana na Liverpool kuwania mataji.

Kama Liverpool ingekuwa katika kiwango chake cha msimu uliopita na mmoja zaidi nyuma yake, sina shaka yoyote kwamba ingetwaa ubingwa wa England tena. Ile haikuwa Liverpool ya kawaida. Ule ulikuwa ni mtambo wa ushindi.

Sishangai kwamba kuna walioanza kuandika na kuamini kwamba huu ndio mwanzo wa United kuanza kutawala tena soka la England na Liverpool kurudi kule ilikokuwa kabla ya ujio wa Jurgen Klopp na wamiliki Wamarekani wa Fenway Sports Club (FSG).

Nyakati nyingine huwa nasikia hoja zikitolewa kuhusu kuporomoka kwa Liverpool na mara nyingi nacheka mpaka kuumiza mbavu. Liverpool inaanzaje kuporomoka wakati karibu kila kilichoisaidia kupanda juu kipo palepale.

Liverpool haijapata mafanikio yake kwa sababu ya kumnunua Virgil van Dijk na Alisson Becker kwa bei mbaya. Manchester City, United na Chelsea walitumia fedha nyingi zaidi kusajili kuliko wakazi hao wa Anfield.

Mafaniko ambayo Liverpool imeyapata katika miaka michache iliyopita yamejengwa katika misingi ya kusajili kwa akili, mshikamano kwenye timu na kiwango cha juu cha ufundishaji wa Klopp na timu yake nzima.

Watu wengi huwa wanaangalia tu kikosi kinachocheza uwanjani, lakini hawaangaliai mambo mengine muhimu yanayofanyika kwenye kikosi. Liverpool iliajiri mtaalamu wa lishe kutoka Bayern Munich, ikaleta mtaalamu wa saikolojia, ikaajiri bingwa wa kuandaa miili kwa wachezaji, imejenga uwanja mpya wa mazoezi unaokidhi matakwa ya kisasa ya kisayansi kwenye kuandaa wachezaji.

Msimu uliopita, watu wakashangaa wakati klabu ilipotangaza kuajiri mtaalamu anayesaidia kuhusu utaalamu wa mipira ya kurusha. Katika historia ya karibuni, hili ni eneo jipya katika soka ambalo kwa wengi halikuwa na maana yoyote.

Nini ambacho kinatufundisha kupitia mambo kama haya? Maana yake ni kwamba Liverpool inaamini zaidi katika sayansi na kufanya vitu vidogo vidogo vya kuwapa wachezaji wake faida kulinganisha na wapinzani wake.

Ni vigumu kuiona klabu ikiporomoka wakati ina mchanganyiko mzuri wa sayansi na uzoefu wa soka kama ulioanza kujazana pale Liverpool. Si watu wengi wanafahamu, lakini Michael Edwards husajili wachezaji kujiunga na timu baada ya kujiridhisha na takwimu muhimu kuwahusu.

Ukiwa unaamini katika sayansi na kuwa na timu inayojua mchezo, suala la kuporomoka halipo.

Lakini, nakubali kwamba Liverpool msimu huu haikuwa Liverpool ile tuliyoitarajia. Mfululizo wa nuksi, kushuka kwa viwango, kukosekana mashabiki viwanjani na mambo mengine madogo ya ndani na nje yamesababisha hali hii.

Badala ya kuzungumzia kugeuka kwa kibao, kwamba sasa ni zamu ya Chelsea au Man United kuizidi Liverpool, suala hapa ni kupigwa kibao kwa timu ya Klopp. Tumezabwa vibao vingi msimu huu.

Na inabaki hapo hapo kwamba ni vibao. Vya kupigwa na si kwamba upepo ndiyo unageuka.

Manchester United wanaweza kuwa na faida Jumapili hii, lakini katika picha kubwa ya mambo, Liverpool ina maisha marefu katika kiwango cha juu kuliko kuamini kwamba mwisho wa zama umefika.

Sayansi itawaambia kwanini kuna wachezaji wameshuka viwango. Sayansi itawaambia kina Klopp ni takwimu ipi ilikosekana zaidi msimu huu kuliko nyingine na watatafutwa watu wenye takwimu kubwa zaidi kwenye hilo eneo ili kuziba upungufu huo.

Mashabiki wanaotarajiwa kuanza kurejea uwanjani msimu ujao, wataamsha ile ari ya kawaida ya wachezaji. Ni kama itatoa hewa ya oksijeni kwa wachezaji ya kuwasaidia kupumua vizuri zaidi.

Kuna wachezaji wapya wataletwa. Kuna wachezaji wasiohitajika wataondolewa. Kuna wachezaji wanaohitajika kidogo, lakini itabidi wauzwe ili klabu ipate fedha za kununulia wengine wanaohitajika zaidi sasa kutokana na mapungufu yaliyopo.

Kwa mfano, na hili tutaliona zaidi katika mechi dhidi ya United, Liverpool ina tatizo kubwa la upungufu wa wachezaji warefu katika timu. Kuna wakati huwa nadhani Liverpool ndiyo inaongoza kwa kuwa na wachezaji ambao kwa wastani ni wafupi kuliko timu nyingine.

Hili ni eneo moja ambalo nadhani litaangaliwa vizuri na ndiyo sababu sishangai klabu kuhusishwa na usajili wa wachezaji kama Sander Berge na Ibrahima Konate. Wana urefu wa futi sita hao, kila mmoja na hilo ni eneo ambalo msimu huu lilituangusha pia.

Manchester United wanaweza kushinda Jumapili hii lakini ndiyo kwanza picha linaanza.

Ieandikwa na EZEKIELI KIMWAGA