UCHAMBUZI: Simba Day ni ishara ya uadilifu wa Mzee Hassan Dalali

KESHO Jumapili, ni kilele cha Tamasha la Siku ya Simba (Simba Day) ambalo litafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika siku hiyo ya kilele, kutakuwa na shughuli mbalimbali ambazo zitafanyika nje na ndani ya uwanja huo ambazo zitahitimishwa kwa mchezo wa kirafiki utakaozikutanisha timu za Simba na mabingwa wa DR Congo, TP Mazembe

Awali kilele cha tamasha la Simba Day kilikuwa kikifanyika kila ifikapo Agosti 8, siku ambayo pia Tanzania huadhimisha sikukuu ya wakulima na wafugaji ya Nanenane lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Uviko iliyojitokeza mwaka jana na kuchelewa kumalziika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu, safari hii tukio hilo litafanyika Jumapili, Septemba 19.

Maadhimisho ya tamasha la Simba Day, yanarudisha kumbukumbu za mashabiki, wanachama, wapenzi wa Simba na wadau wa mpira wa miguu nchini, miaka 12 iliyopita pale lilipoanzishwa na kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009 pindi Simba ilipokuwa chini ya uongozi wa Mzee Hassan Dalali aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Mzee Hassan Dalali aliasisi tamasha hilo akiamini litaunganisha pamoja wapenzi, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo na kumfanya kila mmoja ajione ni sehemu ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1936 lakini kwa upande mwingine kama fursa ya kutambulisha kikosi ambacho timu inakwenda kukitumia katika msimu unaofuata hasa wale wachezaji wapya waliosajiliwa

Wakati anapata wazo la kuanzisha tamasha hilo, Mzee Dalali hakuwa na uhakika wa fedha za kusimamia na kuendeshea lakini moyo wa uthubutu na ujasiri ulimuaminisha kuwa inawezekana jambo hilo katika siku za mwanzoni likakumbana na changamoto lakini zikivumiliwa linaweza kuwa kubwa na lenye hadhi ya kipekee.

Hisia chanya za Mzee Hassan Dalali bila shaka zilizaa matunda kwani hatimaye Simba Day imezidi kupata umaarufu mkubwa na imeshakuwa sehemu ya utamaduni wa klabu hiyo kiasi ambacho hakuna namna ambayo mwaka unaweza kupita bila kufanyika.

Kwa sasa Simba Day limekuwa zaidi ya tamasha la kuwaunganisha Wanasimba na wadau wa mpira wa miguu nchini bali pia limekuwa likiwaonyesha thamani na ukubwa wa klabu ya Simba, wachezaji wapya wanaosajiliwa na timu hiyo hasa wale wa kigeni,

Ni tamasha linaloongeza deni mbele ya mashabiki kwa wachezaji wa timu hiyo katika msimu mpya kwa kuwapa taswira halisi ya hitajio la mafanikio ambalo klabu hiyo imekuwa nalo ambalo hasa ni kutwaa mataji katika mashindano ambayo itashiriki pamoja na kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa.

Na jambo la kufurahisha zaidi, tamasha la Simba Day limekuwa chachu ya kuanzishwa kwa matukio mengine yanayofanana na hilo kwa klabu mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa hapa Tanzania tu kwa mfano, lipo Tamasha la Wiki ya Mwananchi ambalo ni la klabu ya Yanga lililoanzishwa mwaka juzi, kuna lile la Azam FC ambalo lilifanyika mwaka jana kwa mara ya kwanza ingawa sasa hivi halijafanyika na pia timu nyingine kama Biashara United, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Mbeya City nazo zimefanya jambo kama hilo. Kule nchini Burundi nako, timu ya Aigle Noir nayo imeanzisha tamasha kama hilo baada ya kuona mvuto wa tamasha la Yanga la Wiki ya Mwananchi ambapo wao walikuja kucheza mechi ya kirafiki siku ya kilele chake mwaka jana

Pengine haya tusingeyashuhudia kwa ukubwa wake leo hii kama Mzee Hassan Dalali asingejilipua na kuanzisha tamasha la Simba Day miaka 12 iliyopita

Leo hii Mzee Dalali sio kiongozi wa Simba lakini kile alichokianzisha kimebaki kuwa alama na jambo kubwa ambalo linautangaza mpira wa miguu hapa Tanzania kwa kiasi kikubwa hadi kupelekea kuigwa na mataifa mengine.

Dalali hakuwa na choyo kama kundi kubwa la viongozi wa soka ambao pindi wanapokuwa madarakani huamua kujinufaisha wenyewe kwa rasilimali za klabu pasipo kufanya mambo yatakayoacha alama kwa kuhofia kwamba sifa watapewa wengine ama wao hawatokuwa madarakani kwa muda mrefu kwenye soka letu.

Tukio la Simba Day, linatufundisha kwamba inawezekana kuwa na viongozi wanaojali maslahi ya taasisi wanazoziongoza na sio matumbo yao binafsi kama alivyo Mzee Dalali.