UCHAMBUZI: Raiola na bidhaa yake katika mfuko wa Rambo

Sunday April 04 2021
BIDHAA PIC
By Edo Kumwembe

ALHAMISI asubuhi, abiria wawili walishuka katika Uwanja wa Ndege wa EL Prat pale Barcelona. Walishuka katika ndege ya kukodi ambayo iliendelea kuwasubiri katika uwanja wa ndege. Wakaondoka zao kwenda mjini kufanya mazungumzo ya pesa.

Baadaye wakarudi katika uwanja huo, wakapanda ndege yao na kutokomea katika Jiji la Madrid. Wakaonekana katika Uwanja wa Ndege wa Barajas na kisha kutokomea ndani ya Jiji la Madrid kwa mazungumzo mengine yaliyohusu pesa.

Huyu mmoja ndiye mpiga pesa mzuri tunayemfahamu. Mino Raiola. Wakala wa staa mpya wa soka, Erling Haaland. Mwingine alikuwa ni baba wa Haaland, Alf Inge Haaland ambaye naye alikuwa staa wa soka siku za nyuma.

Pale Barcelona walienda kukutana na matajiri wa Barcelona kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kumuuza Erling Haaland kwenda Barcelona. Akili inajipa kwamba Barcelona inabidi wasuke upya kikosi chao. Luis Suarez aliondoka pale na hawajawahi kuziba pengo lake.

Real Madrid nao wanamtaka Haaland. Akienda pale lazima atasimama katikati na kufunga mabao mengi kwao. Haijalishi Karim Benzema atacheza katika nafasi ipi lakini ukweli ni kwamba wote tunafahamu kuwa Haaland ana uwezo wa kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu yoyote kubwa duniani.

Raiola yupo katika ubora wake wa hali ya juu kwa sasa. Zaidi ya mawakala wengine kama kina Jorge Mendes. Huyu Haaland ni mmoja kati ya wateja wake. Anao kina Romelu Lukaku, David de Gea, Moise Kean, Paul Pogba na wengineo. Lakini anajua kwamba kwa Haaland ndipo atapiga pesa ndefu katika dirisha hili.

Advertisement

Haaland ni lulu Ulaya. Ni bidhaa adimu Ulaya. Raiola ametumia akili nzuri kumuegesha pale Borussia Dortmund. Wakati akifunga mabao mengi kama mwehu akiwa na Red Bull Salzburg ya Austria, Raiola hakutaka kumpeleka moja kwa moja katika timu kubwa.

Alihitaji kufanya uhamisho mara mbili kwa ajili ya kupata pesa nyingi. Alijua kwamba Haaland lazima angeenda timu kubwa lakini kwanza akamuegesha Dortmund ambako angefunga zaidi na angekuwa lulu zaidi. Akachukua pesa ya Dortmund.

Haaland ana kipengele kinachomruhusu kuondoka Dortmund kwa dau la Pauni 65 milioni tu katika dirisha kubwa la majira ya joto mwakani. Lakini Raiola alijua kwamba Haaland hawezi kufika huko. Hata Dortmund walijua kwamba Haaland hawezi kufika huko na ndio maana wakakubali kipengele hiki huku wakijua kwamba atafunga mabao mengi na atatakiwa kabla ya muda huo kufika.

Endapo atatakiwa kabla ya muda huo kufika basi Dortmund itanufaika zaidi. Lakini mtu ambaye anaitwa Raiola atanufaika zaidi kwa sababu atasingizia kujipa kazi ya kuishawishi Dortmund kumuuza Haaland kabla ya muda.

Na sasa Raiola ameingia kazini. Juzi alikuwa Barcelona na baadaye akaenda Madrid. Usidhani zile picha zilipigwa kwa bahati mbaya. Hapana. Hakuna mwandishi wa habari ambaye ataota kuwa Raiola na baba yake Haaland watakuwepo uwanja wa ndege kesho.

Kinachofanyika ni Raiola kuandaa watu maalumu wa kazi hiyo kwa ajili ya kuvujisha habari hiyo.

Hii ni kuhakikisha kwamba timu zote zinazomtaka Haaland zinaongeza moto. Baada ya hiyo habari ni wazi kwamba Roman Abramovich ataongeza moto. Manchester City watapiga simu nyingi kwa Raiola na baba yake ambaye aliwahi kucheza hapo.

Hii ndio mbinu ya mawakala maarufu. Wanavujisha habari. Hata pale ambapo Raiola atakutana na Chelsea tutaambiwa. Akienda kukutana na City pia tutavujishiwa habari. Hii itafanya timu zitoane roho katika mbio za kuisaini saini ya Haaland.

Katika mbio hizi klabu ambayo itakuwa katika nafasi nzuri ya kumpata Haaland ni ile ambayo itampatia dau zuri zaidi Raiola na kisha baba yake Haaland. Hivi ndivyo ambavyo mawakala wa soka wanavyoishi. Wanaishi tu kama madalali wengine.

Kitu ambacho unapaswa kuweka akilini ni ukweli kwamba Raiola anaiona nafasi hiyo kuwa kubwa zaidi kwa sababu katika klabu yoyote ambayo Haaland atakwenda, basi atasaini mkataba mrefu wa miaka mitano. Kwanini asipate pesa sasa hivi?

Najua kwamba baada ya miaka miwili Raiola ataanza kusumbua tena. Kama mchezaji ataenda Chelsea, basi baada ya miaka miwili tu atataka kumha-misha kwenda Real Madrid au Barcelona. Umesahau kuwa ndicho ambacho anaifanyia Manchester United kwa Pogba?

Baada ya Pogba kusaini mkataba wa miaka mitano Old Trafford, huku akivunja rekodi ya uhamisho ya dunia mwaka 2016, Raiola alianza kazi ya kutaka kumhamisha baada ya miaka miwili tu. Mpaka leo Raiola amevunja madaraja yote ya uhusiano na Manchester United. Hata dili la Haaland kwenda Manchester United silioni kwa sababu wakala wake ni Raiola.

Raiola anatamba na bidhaa yake hii katika mfuko wa rambo. Hadi amuuze Haaland nadhani wakubwa watapata sana shida. Itakuwa kazi ngumu kwa klabu ambazo zitamuwania. Ni kweli kwamba klabu zipo tayari kutoa Pauni 150 milioni kuinasa saini ya Haaland kutoka Dortmund kwa sasa.

Hata hivyo sioni kama Raiola atakosa Pauni 20 milioni katika biashara hii. Lazima ata-weka mfu-koni. Mzee Haaland sijui ataweka mfukoni kiasi gani, lakini na yeye lazima ataipata faida ya kumzaa Erling.

Hawezi kukosa pauni 10 mfukoni.

Wazee siku hizi hawapo nyuma. Katika kila dili la mtoto lazima wawepo. Ni tofauti na ilivyokuwa zamani. Ni kama unavyomuona Mzee Neymar na mwanae.

Ni kama unavyomuona Mama Rabiot na mwanae Adrien. Wanaendana na kasi ya maisha.

Advertisement