Mavitu binafsi ya mafowadi wanaotamba Ulaya kwa sasa

Sunday April 04 2021
MAVATU PIC

LONDON, ENGLAND

HAKIJAWAHI kutokea na hakika kitu kinachoitwa mwanasoka aliyekamilika.

Sio Lionel Messi wala Cristiano Ronaldo wanaotajwa kuwa bora zaidi ndani ya uwanja, huwa hakuna aliyekamilika kila mtu ana ubora wake.

Na hata mastaa wanaotamba kwa sasa Kylian Mbappe, Erling Haaland na Robert Lewandowski nao hakuna aliyekamilika.

Wote wana ubora wao na udhaifu wanapokuwa ndani ya uwanja.

Lakini, mastaa hao wana mambo yao ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa ustadi mkubwa na kuonekana kuwa mahiri kabisa ndani ya uwanja na bora zaidi ya wengine.

Advertisement

Je, unataka kufahamu ubora wa kila fowadi anayetamba kwenye soka la Ulaya kwa sasa? Kwa baadhi yao hawa hapa ndio kiboko yao, kila mmoja akitamba na mambo yake ndani ya uwanja yanayomfanya kuwa bora zaidi.


Akili: Lionel Messi

Supastaa Lionel Messi ni ngumu sana kumuweka kwenye eneo moja ambalo amekuwa akilifanya kwa usahihi mkubwa ndani ya uwanja, lakini mkali huyo kwa uhodari wake wa kile anachokifanya uwanjani, unaweza kukijumlisha katika jambo moja tu - akili. Messi anatumia akili nyingi kufanya mambo yake ndani ya uwanja. Staa huyo anapokuwa na mpira anajua ni wakati gani wa kupiga pasi, kupiga chenga na kupiga mashuti.


Kichwa: Cristiano Ronaldo

Supastaa mwingine wa soka, Cristiano Ronaldo kama kuna kitu ambacho amekuwa akikifanya kwa uhodari mkubwa basi ni mipira ya vichwa. Staa huyo amefunga mabao yasiyopungua 65 kwa kichwa, ikiwa ni karibuni asimilia 10 ya mabao yake yote aliyofunga kwenye mchezo wa soka. Ronaldo ana ubora wake fulani kwenye kuruka juu. Amekuwa akifanya hivyo kuliko wachezaji wengine wote na kuwapata shida mabeki kumkaba wanapokabiliana naye kwenye mipira ya juu. Olivier Giroud na Harry Kane wanafunga sana mabao ya vichwa, lakini sio kwa uhodari wa Ronaldo.


Mguu wa kulia: Kevin De Bruyne

Kama utatakiwa kutaja mastaa matata kabisa waliopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, huwezi kumuweka kando kiungo mshambuliaji wa Manchester City, Kevin De Bruyne. Staa huyo wa Kibelgiji amekuwa akifanya mambo makubwa kwelikweli ndani ya uwanja, lakini kama kuna kitu kinachomfanya kuwa wa kipekee ni uhodari wake wa mguu wa kulia. Wachezaji wengi wanatumia mguu wa kulia kwenye kucheza, lakini De Bruyne anaonekana kufahamu matumizi sahihi ya mguu wake unapokuwa na mpira. Kwa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu England, De Bruyne alipiga asisti 20 kwa kutumia mguu huo. Wapo mastaa wengine wanaofanya vizuri kwa kutumia mguu huo Toni Kroos na Cristiano Ronaldo, lakini De Bruyne ni balaa kubwa.


Mguu wa kushoto: Mohamed Salah

Staa wa Liverpool, Mohamed Salah kwa sasa ndiye mchezaji anayeonekana kuutumia vyema zaidi mguu wake wa kushoto kitu ambacho hapo awali ilionekana kuwa Gareth Bale ni balaa zaidi. Mo Salah amebeba Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England kwa misimu miwili mfululizo, lakini alifanya hivyo kwa kupitia idadi kubwa ya mabao yake ambayo alifunga kwa mguu wa kushoto. Makipa wa timu pinzani wanakuwa salama pindi mpira unapokuwa kwenye mguu wa kulia wa Mo Salah, lakini habari haiwezi kuwa njema kwao supastaa huyo wa Misri anapoweka mpira kwenye mguu wake wa kushoto.


Kasi: Kylian Mbappe

Wanasema mwendokasi unaua. Basi hicho ndicho kitu ambacho Kylian Mbappe amekuwa akikitumia kuwamaliza wapinzani wake ndani ya uwanja.

Kama kuna kitu ambacho mabeki wa timu pinzani wanakuna kichwa na kuwaza sana wafanyaje wanapokabiliana na Mbappe basi ni kasi ya mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ujerumani. Kuna watu wanatania kwamba hadi sasa, Gerard Pique wa Barcelona bado anamkimbiza Mbappe hajampata. Staa mwingine ambaye amekuwa akisifiwa kwa kasi kwa sasa ni Marcus Rashford, lakini unaambiwa kama kuna mtu ambaye amekuwa akitumia kigezo hicho kiwaadhibu wenzake basi ni Mbappe.


Nguvu: Erling Haaland

Mjadala wa Mbappe na Erling Haaland nani zaidi huenda ukadumu kwa muda mrefu sana kwenye kizazi hiki cha sasa. Lakini, wawili hao kila mmoja ana umahiri wake, wakati Mbappe akitisha kwa kasi, Haaland ni mshambuliaji mwenye nguvu nyingi, mabeki wanapata shida sana kumdhibiti. Straika huyo wa Borussia Dortmund, Haaland amekuwa moto kabisa tangu alipokuwa huko Molde na sasa baada ya kutua tu Ujerumani, mabeki kwenye Bundesliga wanakumbana na wakali mgumu kwelikweli kwenye kumdhibiti kutokana na straika huyo kuwazidi nguvu ndani ya uwanja na kupachika mabao kama anavyotaka.


Miondoko: Robert Lewandowski

Kama kuna mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kwenda na mashambulizi, uelekeo wa mpira kuwa kwenye eneo sahihi kwa wakati sahihi basi ni straika Robert Lewandowski. Mastaa Sergio Aguero na Edinson Cavani ni mahodari kwenye hilo, lakini Lewandowski ni hodari zaidi yao na jambo hilo amekuwa akilitumia kuwazidi ujanja mabeki wa timu pinzani na kufunga mabao kama anavyopenda. Kwa wakati huu, Lewandowski ndite mshambuliaji wa kati bora zaidi huku ubora wake wa ndani ya uwanja ukimpa nafasi ya kuwa mmoja wa wachezaji watakaowania tuzo ya Ballon d’Or.

Lewandowski amekuwa akiwapumbaza mabeki wa timu pinzani kwa miondoko yake ndani ya uwanja.

Advertisement