Utatokaje kwa mfano!

Sunday April 04 2021
AGUEROO PIV

LONDON, ENGLAND

KUONDOKA kwa Sergio Aguero huko Etihad Stadium kunazifikisha mwisho nyakati matata kabisa huko kwenye klabu ya Manchester City.

Baada ya habari za kwamba mwisho wa msimu huu Aguero ataachana na Man City kumeibuka mjadala wa daraja gani hasa supastaa huyo wa Argentina anapaswa kuwekwa kwenye orodha ya mastraika bora kabisa kwenye Ligi Kuu England.

Nje ya jambo hilo, Aguero atahesabika kama mmoja wa wachezaji wa kigeni mahiri kabisa waliopata kutokea kwenye ligi hiyo ya kibabe kabisa Ulaya. Aguero ni mmoja wa wachezaji mahiri kabisa watakaobaki kwenye kumbukumbu za Ligi Kuu England kwamba walikuwa hatari kwa kufunga mabao kwenye ligi hiyo.

Lakini, kuondoka kwake kunaibua mjadala mwingine wa kutafuta mastaa moto kabisa wa kutoka Amerika Kusini waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu England na kutengeneza kikosi kimoja matata kabisa.

Hii timu ya wakali wa Amerika Kusini waliocheza kwenye Ligi Kuu England kama wangecheza katika zama moja na kutengeneza timu yao na kushiriki kwenye michuano hiyo ni dhahiri hakuna wa kuwazuia kwenye kubeba ubingwa. Hili chama ubingwa lazima!

Advertisement

Tena hapo mastaa kama Carlos Tevez, Juan Sebastian Veron, Ederson, Diego Forlan, Edinson Cavani, Denilson na wakali wengine kibao akiwamo Kleberson, wakianzia kwenye benchi.

Kipa: Alisson Becker

Kipa Alisson Becker ni mchezaji wa pili kwenye kikosi hiki mwenye idadi ndogo ya mechi alizocheza kwenye Ligi Kuu England, akicheza mechi 93. Lakini, ndani ya muda mfupi wa maisha yake kwenye kikosi cha Liverpool ameonyesha kiwango bora kabisa na hivyo kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi hiki mbele ya Mbrazili mwenzake, Ederson, anayekipiga Manchester City. Alisson aliisaidia Liverpool kubeba Ligi Kuu England msimu uliopita.

Beki wa kulia:

Pablo Zabaleta

Pablo Zabaleta alicheza karibu kila mechi na kumfanya akipige kwenye michezo 303 ya Ligi Kuu England na hivyo kuwa Muargentina aliyecheza mechi nyingi zaidi akiwa na vikosi vya Manchester City na West Ham United. Uwezo wake wa kukaba na kushambulia ulimfanya kuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Man City chini ya makocha Roberto Mancini na Manuel Pellegrini huku umahiri wake wa kucheza bila ya kukata tamaa ukimpa hadhi kubwa uwanjani.

Beki wa kushoto: Gabriel Heinze

Hakuna ushindani mkali sana kwa mabeki wa kushoto kutoka Amerika Kusini waliowahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England kwa mafanikio. Kutokana na hilo, Gabriel Heinze anapata nafasi na kuwapiku Maynor Figueroa na Mauricio Taricco kwenye beki ya kushoto. Heinze alicheza mechi 52 za ligi kwenye kikosi cha Manchester United kati ya 2004 na 2007 na mara chache alicheza kama beki wa kati, lakini kushoto ndiko alikotamba zaidi.

Beki wa kati: Javier Masche-rano

Javier Mascherano hakuwahi kucheza beki wa kati kwenye timu yoyote West Ham au Liverpool kwa muda wake aliokuwa kwenye Ligi Kuu England, lakini alikwenda kucheza nafasi hiyo alipohamia Barcelona na kuwa pacha wa Gerard Pique uwanjani. Staa huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, hana tatizo anapocheza beki ya kati na jambo hilo ndilo linalomfanya kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hiki cha Waamerika Kusini.

Beki wa kati: David Luiz

Hakuna mwanasoka wa kutoka Brazil anayependa kuwa beki na David Luiz hajawahi kuwa tofauti ya dhana hiyo. Mkali huyo amekuwa akifanya vyema kwenye beki ya kati, licha ya kwamba havutiwi kabisa na kucheza beki wa kati. Hata hivyo, kwenye Ligi Kuu England, Luiz ametamba kwenye vikosi vya Chelsea na Arsenal na kucheza mechi 212 na hivyo kuwa mmoja wa mastaa wa Amerika Kusini ambao wanafanya vizuri kwenye ligi hiyo ya kibabe.

Kiungo wa kati:

Gilberto Silva

Haina mjadala, Gilberto Silva ni kiungo bora wa kati anayejua kukaba kutoka Amerika aliyepata kutokea kwenye Ligi Kuu England. Gilberto Silva alikuwa injini ya Arsenal akipachikwa jina la Ukuta Usioonekana, kutokana na uwezo wake wa kukaba na kufanya mambo kuwa mepesi kwa wachezaji wenzake. Gilverto Silva alicheza mechi 170 za Ligi Kuu England kwa kipindi cha miaka sita aliyoitumikia Arsenal kwenye mikikimikiki hiyo.

Kiungo wa kati: Fernandinho

Safu ya kiungo ya timu hii itakuwa ya kibabe kabisa, Wabrazili wawili matata. Fernandinho anafanya mambo yake moto kabisa akiwa na kikosi cha Manchester City na hivyo kuwa mmoja wa wakali wa kutoka Amerika Kusini ambao mambo yao ndani ya uwanja kwenye Ligi Kuu England si mchezo. Fernandes anaripotiwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa kucheza kimbinu na jambo hilo linamfanya kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hiki bila shida.

Kiungo mshambuliaji: Philippe Coutinho

Unaweza usielewe kwa sasa, lakini kulikuwa na sababu za msingi zilizoifanya Barcelona kulipa Pauni 142 milioni kunasa huduma ya Philippe Coutinho kutoka Liverpool mwaka 2018. Kiungo huyo mshambuliaji alikuwa moto kwelikweli alipokuwa akicheza kwenye Ligi Kuu England akitamba na miamba ya Anfield, huku akiacha alama zake kwa kufunga mabao matata kabisa kwenye ligi hiyo. Ubora wa Coutinho England unamfanya apate nafasi kirahisi.

Mshambuliaji:

Alexis Sanchez

Ingizo pekee hili kwenye kikosi hiki ambaye si Mbrazili wala Muargentina. Alexis Sanchez ni staa wa kimataifa wa Chile na kwenye Ligi Kuu England alicheza zaidi ya mechi 100 akitamba kwanza na Arsenal kabla ya kwenda kujiunga na Manchester United. Kwenye kikosi hiki Sanchez atashambulia kutokea upande wa kulia, huku rekodi zake zikiwa tamu kwenye soka la England, akifunga mabao 80 na kuasisti mara 45 alipokuwa Arsenal.

Mshambuliaji: Luis Suarez

Luis Suarez anapata nafasi mbele ya Carlos Tevez kwenye safu ya ushambuliaji kwa upande wa kushoto. Wawili hao wote wamefanya vizuri kwenye EPL, lakini moto wa Suarez ni balaa huko Liverpool, ambapo alifunga mabao 69 na kuasisti mara 39 kwenye mechi 110 alizocheza. Tevez muda wake aliotamba kwenye EPL ilikuwa alipocheza West Ham, Man United na Man City.

Mshambuliaji:

Sergio Aguero

Kinara wa mabao wa kigeni kwenye Ligi Kuu England. Nani mwingine kama si Sergio Aguero. Kwenye kikosi hiki, staa huyo wa Manchester City atacheza nafasi ya mshambuliaji wa kati. Aguero amefunga mabao 181 kwenye Ligi Kuu na kuzidiwa na wakali watatu tu, Andy Cole, Wayne Rooney na Alan Shearer, lakini yeye akiwa na wastani mzuri wa bao kwa dakika akiwazidi wakali kama Thierry Henry, Shearer na Ruud van Nistelrooy.

Advertisement