UCHAMBUZI: Matumaini ya Wanasimba mikononi mwa Barbara

SIMBA wameondoka nchini kuelekea DR Congo ambako watacheza mechi yao ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, wameondoka wakiwa na matumaini kibao ya kuibuka na ushindi ugenini kesho Ijumaa.

Simba wamekwenda Congo wakiwa wanajua kabisa kwamba watakutana na timu ngumu ambayo imewahi kuwafunga bao 5-0 matokeo sidhani kama kumbukumbu wameifuta, hivyo awamu hii wamejipanga.

Wana Msimbazi wamekwenda DR Congo wakiwa na Afisa Mtendaji Mkuu mwanadada Barbara Gonzalez, miongoni mwa mabinti wanaofanya vizuri kwenye kazi zao hasa kuiongoza Simba kipindi hiki tangu achaguliwe.

Hivi sasa Barbara ni kama amebeba mioyo ya Wanasimba wengi wanaoamini ana uwezo wa kufanya jambo na likakamilika na kuwa zuri kwa asilimia kubwa hivyo hata huko Congo waanamini hawatapata matokeo mabovu chini ya mrembo huyo.

Imani ni jambo moja gumu sana na wakati mwingine linaumiza pale ambapo matarajio yanakuwa sivyo vile ulivyokuwa umejiwekea imani, hivyo Simba ikipata matokeo tofauti na ushindi mashabiki wao lazima waumie na pengine wakaanza kupoteza hata imani kwa viongozi wao. Simba wanaweza kufanya vizuri ugenini kutokana na kikosi chao kilivyoboreshwa, kina wachezaji wanaojituma na kujitoa ambao ndiyo wenye dhamana ya kuamua matokeo ndani ya uwanja yaweje ukiachana na vigisu za nje ya uwanja ambazo hudaiwa kufanya sehemu mbalimbali kunapokuwa na mechi ya mashindano.

Wachezaji wa Simba ndiyo wenye kuamua ni namna gani wambebe mrembo wao pekee Barbara ili aendelee kuaminiwa kwenye majukumu yake ambayo mengi amefanikiwa kutokana na juhudi zake ambapo awali wengi walionekana kutoamini utendaji kazi wake kwani hawakuwahi kumuona akiongoza soka.

Barbara anaonekana kukomaa sasa, ameibeba klabu kubwa kuliko yeye mwenye umri mdogo lakini anapambana kuona anawapa furaha Wanasimba na waendelee kuiamini Bodi ya Wakurugenzi kuwa haikukosea kumteua kwenye nafasi hiyo hivyo hata wachezaji na viongozi wengine wanapaswa kuwa naye bega kwa bega huko walio-kokwenda kupambana.

Simba ilipo basi hata Barbara yupo, hana uoga wala hofu wa matokeo yoyote na hata pale Simba inapopata matokeo ya tofauti anajitahidi kutoonyesha maumivu makali ya moyo wake nje kwa kuhofia kuwanyong’onyesha zaidi mashabiki wao anachokifanya ni kuamini kwamba Simba inaweza tu. Simba imesafiri mara kadhaa na wana tabia ya kutanguliza baadhi ya viongozi ili kwenda kuweka mazingira mazuri mara tu timu yao itakapofika huko ugenini lakini hili Barbara hajawaachia baadhi tu bali hata yeye wakati mwingine anakuwa mstari wa mbele kuongoza kundi hili kuweka mambo safi.

Hajamaliza mwaka katika uongozi wake lakini aliyoyafanya katika kipindi hiko kifupi yanaonekana na yamekuwa na faida tofauti na matarajio ya wengi ambapo wengi wao walikuwa na hofu ya utendaji kazi wake kwa mambo kama matatu makuu, umri, mwanamke na ukubwa wa Simba kwamba asingeweza.

Katika kipindi chake kifupi ameisaidia Simba kufika hatua hiyo ya michuano mikubwa Afrika pia haitakuwa ajabu kuona anaivusha kwenye hatua hiyo akishirikiana bega kwa bega na wachezaji wao na viongozi wengine.

Nidhamu ya timu, uongozi na utawala bora ndivyo vitu pekee vitakavyompa mchango mkubwa Barbara wa kupambana zaidi na kutowaangusha Wanasimba na bodi iliyomwamini, asikatishwe tamaa wala kutopewa ushirikiano, panapohitajika msaada basi kila mmoja atoe kwa kadri ya uwezo wake ikiwa na lengo moja ya kuipa mafanikio timu.

Barbara pambana mrembo umebeba mioyo ya Wanamsimbazi, wao wanachohitaji kutoka kwako ni furaha tu ya uwanjani hasa pale inapofanya vizuri na si vinginevyo, matumaini ya mioyo yao yote kwenye burudani ya soka umeyabeba wewe.

Wanaamini kabis akuwa mmepwangwa kundi lenye timu bora na zenye uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo lakini bado wanajua uyawavusha. Kila la kheri Simba huko DR Congo maana mechi ya nyumbani haina mashaka kabisa.