Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Chama anaweza kuiendesha Biashara United

Muktasari:

NAFAHAMU Simba imetumia zaidi ya Sh500 milioni kumbakisha Clatous Chama. Watani zao walijaribu kuwasumbua kidogo kwa kuitaka saini ya Chama. Nusura waipate kama si ujanja wa watu wa Simba. Wakambakisha.

NAFAHAMU Simba imetumia zaidi ya Sh500 milioni kumbakisha Clatous Chama. Watani zao walijaribu kuwasumbua kidogo kwa kuitaka saini ya Chama. Nusura waipate kama si ujanja wa watu wa Simba. Wakambakisha.

Haikuwa kazi nyepesi. Yanga walishaweka dau kubwa mezani kwa Chama. Kama Chama angeondoka Simba basi kungetokea mgogoro mkubwa kati ya viongozi na mashabiki. Unafahamu namna ambavyo mashabiki wa Simba wanavyompenda Chama.

Unafahamu namna ambavyo kama Chama angeenda kwa wapinzani wao lingekuwa pigo kubwa zaidi katika utani wao kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20. Hakuna mchezaji aliyefikia thamani ya Chama ambaye aliweza kuvuka boda kwa urahisi hivi.

Mwishowe aliyenufaika amekuwa Chama mwenyewe. Amepata pesa nyingi. Hauwezi kumlaumu. Amefanya kazi nzuri Simba lakini zaidi ni alitumia akili nzuri kuutiririsha mkataba wake mpaka miezi ya mwisho na kuwafanya Simba wahahe.

Wakati hayo yakiendelea timu za Ligi Kuu zimeanza mazoezi kwa ajili ya kumalizia ngwe ya mwisho ya ligi. Kule Mara wachezaji wa timu ya Biashara Mara wameingia mitini. Tuliambiwa wachezaji 10 walitoweka bila ya taarifa. Watano wamerudi, watano hawapokei Simu.

Nilikuwa namsikia kocha wao, Mkenya Francis Baraza akilalamika. Ukiona hivi sio bure. Wachezaji hawalipwi kwa wakati na wana malimbikizo mengi ya pesa wanazodai. Ni kitu cha kawaida kwa klabu za Ligi Kuu nchini.

Ukiachana na Simba, Yanga, Azam, Mtibwa, wengine huku chini wanaishi maisha ya dhiki zilizopitiliza. Ukienda katika kambi zao unajiuliza mara mbili kama hizi timu zinastahili kuwepo katika hadhi ya Ligi Kuu.

Pengo kati ya Chama na wachezaji hao ni kubwa. Kifupi ukichukua hizo Sh500 milioni, ukajumlisha na pesa za Vodacom ambao ni wadhamini wakuu wa Ligi, kisha ukajumlisha na pesa za Azam TV basi hata Chama anaweza kuiendesha timu kama Ndanda au Biashara Mara.

Pengo hili limekuwa kichekesho kikubwa. Ni pengo ambalo limezidumaza klabu zetu kubwa katika michuano ya kimataifa. Wakati fulani watu huwa wanasema Ligi yetu ni bora na ina ushindani. Hapana. Ni Ligi ya wenye pesa wachache dhidi ya maskini wengi.

Itazame Ligi Kuu ya Morocco. Kwa nini kina Wydad Casablanca, Raja, FAR Rabat na wengineo wamekuwa bora kila kukicha? Ni kwa sababu pengo sio kubwa kati ya walionacho na wasionacho. Hakuna mchezaji mwenye hadhi ya Chama pale Raja ambaye anaweza kuiendesha timu ya Ligi Kuu.

Timu za chini chini katika soka la Morocco zina viwanja vyenye hadhi kubwa. Zina kambi za kisasa. Mabasi ya kifahari. Kila huduma ya kifahari. Wanachoshindwa ni kununua wachezaji wa bei mbaya kama wa Raja na klabu nyingine kubwa.

Hata hivyo, wachezaji walionao bado wana uwezo mkubwa wa kushindana kwa sababu wameandaliwa mazingira ya kupambana. Katika nchi yoyote yenye uchumi mzuri lazima timu kubwa na ndogo zitakuwepo lakini nyingi zimelingana kwa huduma.

Misri pia ni hivyo hivyo. Hawa kina Al Ahly, Zamalek na Pyramids ni wakubwa kipesa, lakini wanapata wakati mgumu wakicheza na timu wanazochezea kina Himid Mao kwa sababu nao wana pesa nzuri ya kulea wachezaji.

Katika miezi ya karibuni Simba imehaha kusaka nyota wengi mahiri wa kigeni kwa ajili ya kujimarisha zaidi katika michuano ya kimataifa. Wakati mwingine unapata hisia Simba inaweza kuwa timu ya kwanza nchini kumnunua mchezaji mwenye thamani ya Dola 1 milioni.

Swali litarudi pale pale. Mchezaji huyu ataimarika vipi akiwa nchini? Ataimarika kwa kucheza na wachezaji wa Biashara Musoma ambao wamegoma kurudi kambini mpaka leo? Ataimarika kwa kucheza na wachezaji wa Coastal Union ambao wamewasili kucheza mechi Dar es salaam katika siku hiyo hiyo ya mechi?

Ligi yetu pia imesheheni timu za majeshi ambazo hazina bajeti hata ya kumnunua mchezaji mmoja kwa Sh20 milioni. Zinaishi kwa mazoea tu kwa sababu wachezaji wana usafiri wa kwenda mkoa mwingine kwa kupitia mabasi ya majeshi au kulala bure katika kambi za jeshi mikoani.

Kama hatutaua pengo kubwa lililopo baina ya Simba, Yanga, Azam dhidi ya wengineo nadhani tutakuwa tunajisumbua bure tu. Kama wadogo maskini wasipoimarika basi tutaua viwango vya wachezaji mahiri wa timu kubwa.

Wakati fulani watu wakisema Meddie Kagere ni Mzee huwa nawashangaa. Najua Kagere atafunga tu kwa sababu yuko fiti kuliko mabeki wa timu nyingi maskini. Hapati changamoto kubwa. Hata Amissi Tambwe alikuwa akifanya hivyo hivyo licha ya kuitwa Mzee.

Tusijidanganye ligi yetu ni bora. Haitaweza kuwa bora mpaka pale tutakapopunguza pengo la walionacho na wasionacho.

Hili pengo ni kubwa na ingawa litawafanya wachezaji wetu waonekane wafalme katika soka la ndani lakini watakuwa vibonde katika soka la kimataifa.

Imeandikwa na EDO KUMWEMBE