Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kaze mwanasheria anayedatishwa na vibe la mashabiki Yanga #2

JANA tulianza mfululizo wa makala iliyotokana na mahojiano maalumu na Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze ambaye alifichua namna alivyofuatwa mara mbili na Simba ili ajiunge nao na safari yake nzima Jangwani na jinsi alivyokutana na presha ya Kariakoo Derby.

Leo tunaendelea na makala za kocha huyo raia wa Burundi kama alivyohojiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaama na amefichua kitaaluma yeye ni nwanasheria, pia kuanika habari za kupangiwa kikosi, kwa Yanga hajawahi kukutana nayo. Ebu endelea naye...!

VIBE LA MASHABIKI

Kaze anasema pamoja na kufundisha soka katika nchi kadhaa tofauti, lakini hajawahi kuona vibe la mashabiki kama alililokutana nalo Tanzania hasa ndani ya Yanga na kumpa sapraizi ya aina yake.

Anasema hajawahi kuona mzuka wa mashabiki wa soka ndani ya Burundi na hata Canada alikoishia kwa muda mrefu.

“Sikuamini, lakini ni jambo lililonifurahisha kuona namna watu wanapata furaha ya soka nchini Tanzania hasa kwenye hizi klabu kubwa za Simba na Yanga,” anasema Kaze na kuongeza, tofauti na nchi alizowahi kuishi na kufundisha soka, kwa Yanga mashabiki wana shauku na matarajio makubwa kwa timu yao.

“Kitu kilichonifurahisha ni kuona namna watu wanapata furaha na timu yao ikishinda hata kocha unaona kazi unayofanya na kuna watu wanafurahi.

Kaze tangu ametua Yanga anasema amekuwa anaumizwa na namna watu wanavyochambua matokeo kuliko mchakato wa perfomance (timu ilivyocheza).

“Kuna baadhi ya mashabiki wanataka vitu vipatikane hapo hapo, katika soka kuna vitu viwili, kwanza ni wakati unapata matokeo unapaswa kujiuliza baada ya matokeo nini kinafuata?

“Lakini kwa Tanzania yakipatikana matokeo tu hakuna kingine zaidi, watu wanaridhika na wanaamini wachezaji wote wako vizuri na kama hayapatikani wanaanza kutafuta ni nani ambaye anacheza chini ya kiwango au kocha yuko hivi.

Anasema anapenda sana timu inapokosa matokeo wote kuwa kitu kimoja na kuangalia tatizo ni nini, kwani uenda hata wakati wanafunga timu haikuwa vizuri lakini kwa kuwa alikuwa inapata matokeo mashabiki wanasahau.

“Sio mashabiki tu, hata wachezaji wapo baadhi anajua akifunga bao ndio amecheza vizuri lakini haiko hivyo, unaweza kufunga bao lakini hauko kwenye kiwango bora,” anasema.

Anasema mara nyingi makocha ndiyo hubebeshwa mzigo pale timu inapokuwa haifanyi vizuri.

“Sidhani kama ni suluhisho, nakumbuka hata hapa Tanzania miaka ya nyuma kulikuwa na mtindo huo, lakini nitolee mfano Liverpool, iliajiri kocha akawapa plani ya miaka mitano.

“Wamepitia changamoto, lakini leo hii Liver ni timu ambayo inawania ubingwa, nafikiri hizi za kutimua timua makocha ndani ya muda mfupi kunasababishwa na kukosa subira na kutoelewa mchakato wa soka kwa kupita step kwa step.

“Lakini timua timua haiwezi kusaidia hata kidogo, ndiyo sababu unakuta timu zetu nyingi hazina mwongozo ambao unaonekana.

Alimtolea mfano Pitso Mosimane akibainisha amekuwa Kocha wa Mamelodi Sundowns kwa miaka mitano, Ibenge pia kwene klabu ya AS Vita lakini waliendelea kuwapa nafasi wakiamini katika soka kuna ‘process’

KUPANGIWA KIKOSI

Zipo tetesi nyingi katika soka la Tanzania makocha wengi wamekuwa wakipangiwa vikosi vyao na mabosi wa klabu na baadhi ya makocha wa kigeni na hata wazawa wamekuwahi kukaririwa kukiri, Kaze alipiulizwa kana amewahi kukumbana na jambo hilo anajibu.

“Sijawahi kutana na jambo hili kote nilikowahi kufundisha na hata Yanga, ila kama limewahi kutokea basi viongozi wala hawana makosa, aliyekubali kupangiwa timu ndiye ana upungufu.”

“Kwa kocha unayejitambua unatakiwa uheshimu kazi yako, ukimwona kocha anakubali kupangiwa timu maana yake ana kasoro kubwa na haiheshimu kazi yake, binafsi hilo halijanikuta na silitarajii,” anasema Kaze na kudai tangu atue Yanga amekuwa akifanya kazi kwa uhuru mkubwa akishirikiana na wasaidizi wake, bila kuingiliwa na wanapewa sapoti kubwa na viongozi na wanayanga kwa jumla.

KUMBE MWANASHERIA

Familia ya Kaze hasa wazazi wake hawakuwahi kuwa na fikra kocha huyo angekuja kuwa mwanasoka, kwani walimkazania kusoma zaidi na kumtumainia afanye kazi nyingine tofauti.

“Walitaka nisome, kweli nilisoma na nilipohitimu sekondari niliendelea na elimu ya juu, nikichukua masomo ya sheria,” anasimulia Kaze.

Anasema wakati huo alikuwa na mapenzi na soka, kwenye sheria alikwenda kwa shinikizo la wazazi wake.

“Wazazi wengi wa Kiafrika wakati huo walikuwa wanaamini mtoto wake akiwa daktari au mwanasheria ndiyo faraja, hata kwangu ilikuwa hivyo,” anasimulia.

Anasema kutokana na mapenzi yake na mpira alijiunga na timu ya Prince Louis na akiwa na miaka miwili ndani ya timu hiyo, ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini Burundi.

“Bado familia haikunielewa, kwa miaka mitatu niligombana nao wakishinikiza nitoke kwenye mpira nirudi kwenye fani yangu ya sheria, lakini sikuwa napenda kuwa mwanasheria.

Anasema baadae alipata majeraha yaliyomweka nje ya uwanja na kurudi kusoma na kuhitimu digrii ya sheria, lakini haikuwa fani aliyokuwa akiipenda wakati huo ilikuwa mwaka 2015.

“Nikiwa nimeacha soka kutokana na majeraha, kocha wetu aliitwa kuwa kocha msaidizi kwenye timu ya taifa, nikaambiwa kwa kuwa sasa sichezi basi nichukue jukumu la kusaidia kusimamia mazoezi.

“Mwanzo nilikataa, nikasema mimi nawezaje kuwafundisha wachezaji ambao wengine wamenishinda kipaji na walikuwa wakiniweka benchi, ila nikajipa muda na kusema naweza kuwa kocha mzuri kwao kama nitaamua.”

Anasema alipanga kuwapa mazoezi ambayo watayafurahia na kama wataona yanawafaa basi watamuamini na baadae kumheshimu kama kocha aliyepewa jukumu la kusimamia mazoezi wakati huo, japo hakuwa na vyeti vya ukocha.

“Nilianza hivyo ukocha, nilitumia muda wangu wa ziada kusoma sana kwani wakati ule makocha wa Kiafrika walikuwa wanapenda wachezaji wakimbie sana, mimi nikawa nabadilika kila siku na ninawaeleza faida ya mazoezi ninayoyatoa kila siku.”

Anasema muda mwingi aliwapa mazoezi ya mpira na ilikuwa hata wakitaka kufanya fitness wanafanya na mpira hadi kocha aliporejea lakini tayari wachezaji wenzake walishajenga heshima kwake.”

“Kiongozi wa timu alinishauri, akaniambia Kaze wewe ni kocha mzuri, nenda kasome, nikiwa kwenye mchakato huo, timu yetu ya taifa ilifuzu fainali za Afrika na kocha kuondoka tena, mimi ndiye nikapewa jukumu la kusimamia timu kwa mara nyingine kama kocha msaidizi.

Anasema baadae alienda kusoma, walikuwa makocha 30 wa Burundi ambao walipa ofa ya masomo Ujerumani lakini familia yake haikuwa ikiamini hiyo taaluma ya ukocha, japo walimkubalia kwa shingo upande.

“Iliona nguvu ninayotumia kwenye mpira, wakaamua baadae kunisapoti japo anasema hakuwahi kufanya kazi ya sheria hata mara moja baada ya kuhitimu masomo yake.

BURUNDI SOKA HALILIPI

Makocha na wachezaji wengi wa Burundi wamekuwa wakija nchini kusaka timu za kucheza au kufundisha, jambo ambalo Kaze anasema ni kutokana na hali ngumu ya maisha ya soka nchini humo.

“Ligi ya kule ni ndogo, japo ina muundo mzuri lakini haina mapato kama ilivyo Tanzania, kule unawezacheza mwaka mzima bila kupokea mshahara kipindi chote.

“Lakini unaona watu wanajituma, makocha wa Burundi wanapenda kujifunza na wana matamanio ya kufika mbali na ndicho kinawasaidia hata wachezaji pia,” anasema.

Itaendelea kesho

IMEANDIKWA NA IMANI MAKONGORO, MWANAHIBA RICHARD NA THOMAS NG’ITU