Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI: Bernard Morrison, ‘Mtanzania’ aliyezaliwa Ghana

“BUSHA, busha,” alisema Bernard Morrison akimwambia mwandishi wa habari aliyehoji kuhusu staili yake ya kushangilia baada ya kufunga mabao mawili katika pambano kati ya Simba dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika Uwanja wa Taifa.

Alichukua mpira akauweka ndani ya bukta na kushangilia huku akitanua miguu yake. Kabla ya hapo mashabiki wa Yanga walikuwa wamedai kwamba Morrison alikuwa anaumwa ugonjwa huo. Maisha yake Simba yalikuwa hayaendi sawa kutokana na ugonjwa wa ngiri.

Morrison alikuwa akiwajibu mashabiki wa Yanga. Huwa inatokea kwa wachezaji wa Ulaya kujibu mapigo wakati wa kushangilia kutokana na maneno fulani yaliyosemwa dhidi yao. Hata hivyo usingetegemea Morrison kufanya hivyo.

Kila nikimtazama Morrison nagundua kwamba ana ‘Utanzania’ fulani hivi katika damu yake licha ya kwamba amezaliwa Ghana. Amezijua timu zetu mapema. Amejua ushabiki wake na yeye anatumia kipaji chake kukaa katikati ya ushabiki huo.

Amejua siasa za soka la Tanzania pengine kuliko wachezaji wa kigeni waliokuja kabla yake. Na sasa ameamua kuwa mchezaji ambaye ni shabiki. Anajua jinsi ya kuwakosha watu wa Simba nje ya uwanja huku akiwakera watu wa Yanga nje ya uwanja.

Anajirekodi katika video anasema “nitawakeraaa.” Anaongea Kiswahili cha ndani ndani. Lakini zaidi ni kwamba anaonyesha ‘Utanzania’ wakati wake wa kubishana na mashabiki wakati tumewahi kukaa na mastaa wengi ambao hawakuwa na muda wa kubishana na mashabiki.

Wachezaji wa kulipwa waliokuja nchini wamekuwa watu wa mifano katika maisha yao binafsi lakini sio Morrison. Kuna wachezaji wengi ambao walisimama katikati ya chuki lakini wakajua namna ya kustahimili chuki hizo. Haikuanza leo wala jana.

Kwa mfano, walikuwepo kina Emmanuel Okwi ambao walishambuliwa vikali na mashabiki wa Yanga baada ya kurudi tena Simba, lakini Okwi hakuwa na muda nao. Aliendelea kuwakera mashabiki wa Yanga kwa kupiga kandanda safi pale Msimbazi. Hakutumia mitandao ya kijamii kuandika kitu chochote wala kujirekodi.

Amis Tambwe alikuwa anashambuliwa na watu wa Simba wakati alipokwenda Yanga na kuendelea kupachika mabao. Hakuwa na muda wa kujibizana na mtu. Wachezaji wa Kitanzania wana uwezo wa kujibishana na mashabiki lakini sio wachezaji wa kigeni. Hata hivyo Morrison amekuwa na muda huo kama wachezaji wa Kitanzania.

Lakini huwa namtazama tena na tena Morrison na kisha kujikumbusha Utanzania wake kwa jinsi alivyo na kipaji kikubwa. Napata maswali mawili. Kwanza amefikaje nchini? Waghana wa kipaji chake huwa wanakwenda mbali. Wakikosa kwenda Ulaya basi wanaishia Uarabuni.

Lakini kwanini nishangae wakati ‘Watanzania’ wenzake tupo hivi hivi. Kuna Watanzania tunawajua walikuwa na vipaji kama Morrison lakini waliishia hapahapa kwa sababu ya kupenda mambo ya Simba na Yanga. Hawa tunawafahamu.

Kuna wachezaji wengi ambao tunajiuliza kwanini mpira wao uliishia hapa nchini? Ni kwa sababu ya Utanzania wao zaidi na sio vipaji vyao. Wangeweza kufanya jambo na kwenda katika malisho mema lakini walijikuta wakiishia hapa hapa.

Swali jingine ambalo linanikwaza kuhusu Morrison ni jinsi ambavyo maisha yake ya soka yamebakia kuwa nusunusu tu. Orlando Pirates amecheza kidogo. Vita amecheza kidogo. Yanga amecheza kidogo. Simba inaweza kuwa timu yake pekee ambayo huenda akacheza kwa misimu miwili kamili.

Msimu wake wa kwanza nao umekuwa nusunusu tu. Labda atapata msimu kamili katika msimu ujao huku akicheza bila ya majeraha na akijikita zaidi katika kukaa klabuni hapo kuliko vimbwanga ambavyo aliwafanyia watani wao Yanga.

Kama akituliza kichwa na kucheza misimu miwili takatifu huku akiuweka kando ‘Utanzania’ wake huenda Morrison akawa mmoja kati ya wachezaji bora wa kigeni kuwahi kucheza nchini. Sidhani kama ataweza kutuliza kichwa kwa sababu ya Utanzania wake. Amekutana na Watanzania na amekaa katikati ya ushabiki wa Simba na Yanga. Ni ngumu kujua hatima yake.

Akituliza kichwa atafanya vizuri zaidi lakini akiendelea kucheza kwa ajili ya kuwakera mashabiki wa Yanga basi kila siku watakuwa wanamtoa mchezoni. Kama akiweza kutulia na kufanya anachoweza basi inaweza kuwa vema zaidi kwake. Mashabiki wa Yanga hawataacha kumuandama.

Lakini bado siamini kama kichwa chake kinaweza kutulia. Labda ni hulka yake. kama angetulia si ajabu angekuwa anakipiga katika moja kati ya timu kubwa barani Ulaya. Kata kubali lakini ukweli ni kwamba Morrison anajua sana.

Morrison ni miongoni mwa mawinga ambao wanawafuta mabeki. Hawawaogopi. Anajua kuuficha mpira, anajua kupiga chenga, na majuzi ametukumbusha kipaji chake cha kufunga. Si mawinga wengi ambao wana uwezo mkubwa wa kufunga. Morrison anaonekana kuwa mmaliziaji mzuri.

Simba wanachoweza kufanya ni kuhakikisha wanajaribu kumrudishia Morrison ‘Ughana’ wake. Lakini naambiwa eneo ambalo Morrison ametoka huko Ghana lina watu wa aina yake. watu watukutu. Sijui kama ni kweli lakini Waghana wote waliokuja nchini tangu zamani akina Yaw Berko na hadi sasa Lamine Moro hawana tabia za Morrison.

Imeandikwa na EDO KUMWEMBE