UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni muda wa kupiga soga za ‘Kariakoo Derby’ Kigoma

Thursday July 29 2021
kaliua pic

NCHI ilikuwa mikononi mwa Yanga wiki tatu zilizopita, licha ya kwamba ubingwa walitwaa watani na wapinzani wao wa karibu Simba, bado Yanga walikuwa na sababu ya kutamba kwa sababu waliwafunga Simba.

Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ninayoifahamu ambayo ubingwa haunogi kama haujamfunga mtani wako. Unaweza ukabisha mdomoni, lakini chinichini moyoni utakuwa unakubaliana na mimi kwamba raha ya ubingwa iambatane na kumfunga mtani.


IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR

Huu utamaduni ulianzia wapi? Kama unayo majibu unaweza kuniandikia kupitia namba zangu za simu hapo juu.

Baada ya wiki tatu za furaha, Jumapili Yanga walirejea kwenye maisha yao ya zamani. Maisha machungu. Maisha ya huzuni. Maisha ya unyonge mbele ya watani zao Simba. Maisha haya yanakuja baada ya kupoteza fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Advertisement

Bahati mbaya sana ni kwamba wamepoteza fainali mbele ya watani zao. Ingekuwa rahisi zaidi kwa Yanga kama wangepoteza mbele ya timu nyingine yoyote lakini sio Simba. Kupoteza mbele ya Simba inauma mara mbili zaidi. Unaumia kupoteza fainali na kupoteza dhidi ya mtani. Kwa Tanzania hii sababu ya pili inaumiza zaidi.

Kwa mantiki hiyo sasa ni rasmi kuwa Yanga wanamaliza msimu wa nne bila taji lolote kubwa. Tanzania kuna mataji mawili makubwa. Taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara na lile la ASFC. Jumapili walikuwa na nafasi ya kujipoza kwa kutwaa kombe hilo, lakini bahati haikuwa kwao. Hivi ni bahati haikuwa kwao au ulikuwa ni uzembe wao?

Labda tutafute jibu kwa kuitazama sura ya mechi ilivyokuwa.

Kwanza, Uwanja wa Lake Tanganyika ulimeza ubora wa mchezo. Unapoona Clatous Chama analazimika kupiga mpira mbele akiwa peke yake ujue kulikuwa na tatizo mahali. Nyasi hazikuruhusu mpira utembee chini, matokeo yake kila timu ikaamua kujilinda kwa kuhakikisha mpira haukai katika eneo lao. Mwisho wa siku tukawa na fainali ‘butua butua’ kati ya Simba na Yanga. Hakuna kocha ambaye

angethubutu kuituma timu yake ikatafute mabao kwa kucheza mpira. Kila mmoja aliamua kujihami akisubiri bahati itokee na hauwezi kuwalaumu hata kama angekuwa Pep Guardiola pale Lake Tanganyika angewaagiza kina De Bruyne wabutue tu. Asingekuwa na ujanja mwingine.

Simba ‘walipata ahueni’ kipindi cha pili baada ya kiungo mahiri wa Yanga, Tonombe Mukoko kuonyeshwa kadi nyekundu. Kadi nyekundu ya Mukoko iliwafanya Yanga warudi nyuma kuzuia kisha ikawapa Simba kujiamini kwa sababu walikosa mashambulizi kutoka kwa Yanga.

Kwa jinsi fulani Yanga wanaweza kumlaumu Mukoko kwa kadi nyekundu aliyoipata kwa kujitakia. Kwa namna mchezo ulivyokuwa labda wangeweza kupambana kupata chochote kama wangekuwa wote.

Huwezi kujua, labda, wangeweza pia kupoteza Mukoko akiwa ndani, lakini isingekuwa kirahisi vile. Kilichobadilisha upepo wa mchezo ni kadi nyekundu ya Mukoko.

Kinachomhukumu zaidi Mukoko ni namna alivyopata kadi nyekundu. Angeweza kusamehewa kama angepata kadi katika mazingira ya kuzuia timu isifungwe. Kadi yake ilikuja baada ya kumpiga kiwiko John Bocco.

Ni tukio la kitoto na la kijinga kufanywa na mchezaji kama Mukoko - mchezaji muhimu zaidi anayetegemewa. Mchezaji mkongwe.

Mchezaji wa kimataifa anayelipwa kwa dola anafanyaje tukio kama lile kwenye mechi ya fainali? Hakuna anayejua jibu. Hata Mukoko mwenyewe hana jibu.

Japo watamsamehe, lakini ni tukio ambalo mashabiki wa Yanga hawatakaa walisahau kwa Mukoko. Hata msamaha wanampa kwa shingo upande kwa sababu wanajua umuhimu wa Mukoko. Ingekuwa ni Deus Kaseke kusingekuwa na mjadala moja kwa moja wangetaka aondoke.

Lakini, pili, historia inambeba Mukoko. Hana rekodi ya matukio ya usumbufu na ukorofi ndani na nje ya uwanja.

Kwa upande mwingine unaweza kumtetea kuwa na yeye ni binadamu. Ingekuwa ni tabia ya kujirudia mara kwa mara ‘ungeweza kumng’atia meno’, lakini ndio mara ya kwanza kumuona akifanya haya, labda alipitiwa tu.

Tukirejea kwenye mchezo. Baada ya kadi nyekundu ya Mukoko unaweza kuwapongeza Simba kwa kufanikiwa kutumia upungufu wa Yanga na kupata bao

Pia unaweza kuwapongeza wachezaji wa Yanga kwa kufanikiwa kupambana hadi mwisho. Watu ambao huwezi kuwapongeza ni viongozi wa Yanga waliowahidi mashabiki wao taji mwisho wa msimu. Kitu unachoweza kuwasaidia ni kuwakumbusha kutumia vizuri dirisha la usajili kusaini mastaa watakaoweza kupambana na Simba ndani ya uwanja. Labda kama Azam FC wanavyosajili sasa.


Advertisement