Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo matano Twiga WAFCON

Muktasari:

  • Katika ratiba ya michuano hiyo Twiga Stars imepangwa Kundi C na itaanza kwa kuvaana na Mali kesho Jumatatu kisha Julai 11 kupambana na watetezi - Afrika Kusini kabla ya kumaliza kwa kuumana na Ghana Julai 14.

ZIMEBAKI saa zisizozidi 24 kabla ya timu ya taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ kuandika historia katika mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 zilizoanza jana Jumamosi na kutarajiwa kufikia tamati Julai 26 nchini Morocco.

Katika ratiba ya michuano hiyo Twiga Stars imepangwa Kundi C na itaanza kwa kuvaana na Mali kesho Jumatatu kisha Julai 11 kupambana na watetezi - Afrika Kusini kabla ya kumaliza kwa kuumana na Ghana Julai 14.

Haya ni mashindano ya kufungua safari ya Twiga Stars katika kundi linaloitwa na wengi la kifo likiwa na mataifa makubwa kisoka Afrika yaani Afrika Kusini, Ghana (mara kadhaa nusu fainali) na Mali (waliokuwa bora hivi karibuni).

Tofauti na timu zingine ambazo zimekuwa na mwendelezo kwenye mashindano hayo, Stars ilianza kushiriki 2010 ilipoishia hatua ya makundi ikikusanya pointi moja.

Afrika Kusini ni mabingwa watetezi  WAFCON, Ghana ni taifa lenye historia ya mafanikio kwenye soka la wanawake, huku Mali ikiwa ni timu iliyopiga hatua kubwa katika miaka hivi karibuni.

Hali hiyo inazua swali kwa wadau kwamba je? Twiga Stars inaweza kufuzu hatua ya makundi au kuleta heshima kwa taifa na kuvunja rekodi za awali?

Haya hapa mambo matano ambayo inapaswa kuyazingatia.


MAMBO MATANO

Jambo la kwanza ni kufanya uchambuzi wa wapinzani. Maarifa ni silaha kubwa.

Benchi la ufundi la Twiga Stars lina jukumu la kumchambua kila mpinzani kwa mechi za karibuni kujua mbinu wanazotumia, aina ya uchezaji, safu hatari, pamoja na upungufu ili kuutumia kwa faida.

Mfano mzuri ni Afrika Kusini hupenda kumiliki mpira na kutumia mashambulizi ya pembeni, hivyo wanahitajika mabeki wa pembeni wenye nguvu na wataokaoweza kuzuia mashambulizi.

Ghana hucheza kwa kasi na nguvu, huku Mali ikitegemea mashuti ya mbali na uwezo binafsi wa wachezaji wa kiungo, hivyo Stars ina kazi kubwa.


2.KASI YA WAPINZANI

Twiga Stars imeonyesha uwezo wa kucheza soka la kuvutia hasa ikikutana na timu za Afrika Mashariki.Hata hivyo dhidi ya mataifa yaliyoendelea kisoka kama Afrika Kusini au Ghana kasi ya mchezo huwa juu zaidi hivyo inapaswa kuendena na kasi ya wapinzani.

Wachezaji wa Stars wanapaswa kupiga pasi za haraka na zinazofika sambamba na kuwa na uwezo wa kumiliki mpira na kutuliza mashambulizi ya wapinzani.

Unapocheza na timu zenye kasi kama Afrika Kusini na Ghana Stars haipaswi kurudi nyuma, bali kushambulia kwa kasi na kurudi haraka kujilinda. Wachezaji wanapaswa kujengwa kisaikolojia ili kuwaondolea hofu ya kucheza na timu kubwa na wachezaji wenye majina makubwa.


3.MBINU ZA KOCHA

Hivi karibuni kocha Bakari Shime amekuwa akitumia mfumo wa kucheza na mabeki watatu wa kati yaani  Violeth Nicholaus, Anastazia Katunzi na Ester Maseke, lakini kwa mechi hizo ngumu anapaswa kuangalia mfumo mzuri wa kuendana na wapinzani. Benchi la ufundi linapaswa kuhakikisha wachezaji wanacheza kitimu na nidhamu ya mchezaji mmoja mmoja ni jambo muhimu.

Mabadiliko ya haraka endapo mfumo wa mabeki watatu hauendi vizuri kwani Shime hivi karibuni amekuwa akitumia 3-4-2-1 yaani mabeki watatu, viungo wanne wakiwemo wing-back, viungo washambuliaji wawili nyuma ya mshambuliaji mmoja.


4.HAMASA

Hii ni sehemu mojawapo ya kufanya wachezaji wapambane kwa jasho na damu kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi ngumu kama hizi.

Katika michuano mikubwa kama timu hupata mafanikio enndapo wachezaji wanakuwa na motisha ya kutosha ya kifedha na kiuzalendo.

Soka la wanawake linakua siku hadi siku hivyo Shirikisho la Soka nchini (TFF) linapaswa kuwaangalia nyota hao na pengine hata kuwaahidi zawadi nono wakifanya vizuri kwenye mechi za makundi na kuvuka hatua inayofuata.


5.SAFU YA ULINZI

Hili ni miongoni mwa maeneo yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi kwani likifanya makosa linaweza kuleta madhara.

Mabeki wanapaswa kuwa na mawasiliano mazuri, wepesi wa kuusoma mchezo kwa urahisi, uwezo wa kukaba bila kufanya makosa na nidhamu ya hali ya juu ndani ya eneo la hatari itasaidia kupunguza hatari.

Kipa wa Stars, Naijat Abbas anapaswa kuwa kwenye kiwango cha juu, sio tu katika kuokoa mashuti bali pia katika kuongoza safu ya ulinzi, kusoma mipira ya krosi, na kuanzisha mashambulizi kwa haraka. Hili linahitaji mazoezi maalum kwa walinda milango kabla ya mashindano.

Katika kundi lenye washambuliaji hatari kama Thembi Kgatlana (Afrika Kusini) au Doris Boaduwaa (Ghana), safu ya ulinzi ya Twiga Stars inapaswa kuwa imara zaidi.

Twiga Stars ipo kwenye kundi gumu, lakini mpira wa miguu ni mchezo wa makosa yapo baadhi ya mataifa yaliyowahi kuonekana dhaifu na bila kutarajiwa yakafanya vizuri.


WAPINZANI WA STARS

- MALI

Twiga Stars itaanza dhidi ya timu ya Mali wasio wapinzani wa kubezwa kwani wanacheza soka la nguvu, kasi na wachezaji wenye uzoefu wanaocheza ligi mbalimbali za kimataifa ambao wanaweza kuamua mechi ngumu.

Kwa miaka ya hivi karibuni Mali ni miongoni mwa timu iliyoimarika kwani WAFCON  2018 ilifika nusu fainali na kutolewa kwa mabao 4-2 na Ghana.

Ilifuzu WAFCON baada ya kushinda mechi za raundi ya kwanza dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati jumla mabao 10-2 nyumbani na ugenini na kuvuka raundi ya pili ilipokutana na Guinea ikashinda kwa idadi hiyo ya mabao.

Nyota hatari wa Mali ni Agueissa Diarra anayekipiga PSG ya Ufaransa ambaye uzoefu anaupata kwenye michuano mikubwa Ulaya.

Diarra ni mchezaji mwenye kasi, nguvu, na jicho la kuona bao, aling’ara katika mechi za kufuzu WAFCON 2024 kwa kufunga hat-trick dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mchezaji mwingine ni Aissata Traore, ni kiungo anayekipiga FC Fleury 91 inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Ufaransa.

Ni bora wa kutoa pasi za usahihi, ana uwezo wa kudhibiti kasi ya mchezo.

Uwezo wake wa kusoma mbinu za mchezo na usahihi wa kiufundi humfanya kuwa mhimili muhimu wa safu ya kiungo ya Mali lakini kama kiungo wa Stars Donisia Minja atapewa kazi ya kufuatana naye muda wote itampunguzia nafasi ya kupokea mipira akiwa huru.

Nyota mwingine ni kiungo Diana Msewa ambaye ana uwezo wa kumminya kwa kasi pindi anapopata mipira ili asipate muda wa kupanga au kupenyeza pasi kwa washambuliaji wa Mali.


AFRIKA KUSINI

Timu ya  Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ndio mabingwa watetezi na kabla ya fainali zilizopita, walishika nafasi ya pili katika fainali 2018.

Banyana Banyana imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ikiishia 16 bora.

Timu hiyo ina wachezaji wenye uwezo wa kuamua mchezo lakini mmojao ni Jermaine Seoposenwe anayecheza nafasi ya ushambuliaji.

Kinachomtofautisha na washambuliaji wengine ni uwezo wake wa kubadilisha mitindo ya uchezaji. Anaweza kukimbia moja kwa moja kuelekea lango la wapinzani, kukaa na mpira kwa ustadi na pia kusogea kwa akili katika nafasi nusu wazi ili kuvuruga safu ya ulinzi ya wapinzani.

Hii ni silaha muhimu kwa kocha wa Banyana Banyana, Desiree Ellis ambaye humtumia kwenye mifumo mbalimbali kwani mbali na kucheza mbele anaweza kushuka hadi chini kuchukua mpira.

Kwa hiyo, Twiga Stars wanapaswa kumdhibiti kwa akili, nguvu na nidhamu ya hali ya juu kwani mafanikio dhidi ya Afrika Kusini yanategemea kwa kiasi kikubwa jinsi atakavyodhibitiwa.

Mwingine ni Hildah Magaia ambaye ni silaha ya ushambuliaji na WAFCON 2022 ndiye alikuwa mwiba kwa Morocco kwani alifunga mabao 2-1 yaliyoipa Sauzi taji la kwanza.

Anaichezea klabu ya Mazatlain ya Mexico. Hii inamaanisha kuwa akiwa ndani ya boksi ama eneo hatari, huwa hatumii nguvu badala yake hutumia akili na uamuzi sahihi kufunga mabao kwa ufanisi mkubwa.

Magaia hupokea pasi nyingi za mwisho kutoka kwa viungo kama Kgaelebane Mohlakoana ama Seoposenwe. Ni muhimu kuziba njia hizo na Minja ana jukumu la kuharibu pasi zinazoelekezwa kwake.


GHANA

Mechi ya mwisho Stars itamaliza na Ghana ‘Black Queens’ambayo imeshiriki mara tatu fainali za Kombe la Dunia ambapo zote iliishia hatua ya makundi.

Imeshiriki mara 12 tofauti katika fainali za WAFCON ambapo mafanikio makubwa ni kumaliza nafasi ya pili 1998, 2002 na 2006 huku ikiishia nafasi ya tatu mara tatu  2000, 2004 na 2016. Baada ya kupitia kipindi cha kuporomoka kilichoambatana na kutolewa mapema na kushindwa kufuzu baadhi ya mashindano, Ghana imeanza kurudi kwenye ramani ya soka. Timu hiyo ilifuzu WAFCON kwa kuiondoa Rwanda kwa jumla ya mabao 12-0 ikishinda ugenini 7-0 na nyumbani 5-0 ikavuka raundi ya pili na kukutana na Namibia ikaishinda mabao 3-2.

Ghana ilishinda mabao 3-1 nyumbani kisha ikafungwa bao 1-0 ugenini kwa maana hiyo pia licha ya ubora wao lakini timu hiyo inaruhusu mabao ikikutana na timu zenye washambuliaji wenye njaa ya mabao kama Stars.

Nyota wa kuchungwa ni mshambuliaji Princella Adubea anayekipiga Abu Dhabi Country Club huko Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na alishawahi Sporting Huelva ya Hispania. Mchezaji mwingine Stars inapaswa kumchunga ni Alice Kusi. Huyu ni kiungo mshambuliaji ambaye ni injini ya ubunifu katika kikosi cha Black Queens akiwa na uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga.

Kusi anakipiga Al Ahli ya Saudi Arabia, anasifikwa kwa utulivu mkubwa akiwa na mpira miguuni.