UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Fiston Mayele bidhaa adimu isiyopatikana sokoni

Thursday January 13 2022
Mayele PIC
By Oscar Oscar

MARA ya mwisho Yanga kuwa na safu ya uhakika ya ushambuliaji ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Ni kipindi kile ambacho Mrundi Amiss Tambwe alikuwa anaongoza mstari wa ushambuliaji, huku pembeni akiwapo Donald Ngoma na mkono wake wa kulia alikuwa anatembea Saimon Msuva.

Ilikuwa safu imara ya ushambuliaji ambayo mashabiki wa Yanga walikuwa wakiiota kwa muda mrefu walipokuwa wakipitia magumu. Kilichokuwa kinawauma zaidi ni kwamba majirani na ndugu zao - Simba walikuwa na kikosi imara wakiwa na safu hatari ya ushambuliaji iliyoongozwa na John Bocco, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Chris Mugalu aliyekuja baadaye.

Simba waliwatambia Yanga kwamba washambuliaji wao wanaokaa benchi wanaweza kuanza kikosi cha kwanza cha Yanga. Yanga walitumia nguvu kubwa kusaka washambuliaji bila mafanikio. Walijikuta wakiibuka na koroma mara nyingi hadi walipomnasa Fiston Mayele msimu huu.

Tutoe heshima kwa Heritier Makambo. Katikati hapo Yanga walimpata Makambo aliyeibeba safu yao ya ushambuliaji licha ya kucheza katika kikosi kisichokuwa na wachezaji imara sana.

Makambo aliondoka kwenda Horoya kisha akarejea tena msimu huu baada ya maisha kutokwenda vizuri huko Horoya. Mpaka sasa ameshindwa kutamba na kuingia katika kikosi cha kwanza kwa sababu ya Mkongomani mwenzake anayeitikisa nchi kwa sasa, Fiston Mayele Kalala.

Mayele hatikisi kwa bahati mbaya. Kwanza anacheza katika klabu inayopendwa zaidi na mashabiki wake nchini. Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za mashabiki walioingia uwanjani msimu uliopita zilizotolewa na Bodi ya Ligi Tanzania.

Advertisement

Hapo unajiuliza timu ambayo haikutwaa ubingwa kwa kipindi cha miaka minne na ilikuwa haifanyi vizuri iliwasihi vipi mashabiki wake waingie uwanjani kuliko timu zingine? Ni upendo tu walionao watu wa Yanga kwa timu yao.

Watu wa Simba wanaweza kung’ata meno kwenye hili, lakini hatuna budi kuamini takwimu.

Kama Simba wanaipenda timu yao walipaswa kuongoza kuingia viwanjani nyakati ambazo timu ilikuwa inafanya vizuri zaidi nchini.

Tuondoke huko tuendelee na Fiston Mayele.

Kama Yanga wanavyoipenda timu yao ni vivyo hivyo wanawapenda wachezaji wao wanaofanya vizuri uwanjani.

Hili la kupenda wachezaji wanaofanya vizuri ni kwa klabu zote kubwa nchini. Tanzania mchezaji anapendwa kipindi akiwa kwenye ubora wake. Anapopitia nyakati ngumu mara nyingi anabaki mwenyewe.

Huyu Mayele yupo katika nyakati bora kwa sababu anafanya vizuri. Amewasahaulisha Yanga matatizo waliyokuwa nayo katika safu yao ya ushambuliaji.

Bahati njema zaidi kwake ni kwamba amechukua nafasi ya watu ambao walikuwa wanafanya vibaya. Hajapata kazi ya kuziba pengo. Amekuja kucheza katika nafasi aliyoipita David Molinga, Michael Saprong na Fiston Abdulrazack. Hawa wote waliboronga. Hawakuacha kazi ngumu kwa ambaye angekuja baada yao.

Kazi ingekuwa ngumu kidogo kwa Mayele kama angekuja baada ya Donald Ngoma na Amisi Tambwe wakiwa katika ubora wao.

Uimara mkubwa zaidi wa Mayele upo katika kufumania nyavu. Anajua kuweka mpira wavuni, lakini ana kitu kimoja cha ziada kinachomtofautisha na washambuliaji wengi nchini.

Mayele anajihusisha zaidi na mchezo kuliko washambuliaji wengi wa kati. Badala ya kusubiri na kujiweka katika nafasi ya kufunga, Mayele anapenda kushuka kwenye eneo la kiungo kuisaidia timu kucheza. Kiburi cha kufanya hivyo anakipata kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kumiliki mpira aliobarikiwa.

Hicho ndicho kinachomfanya kocha Nabi amtumie zaidi na kuzidi kumsahau mshambuliaji mwingine wa DR Congo, Heritier Makambo.

Huwezi kumlaumu Nabi na Makambo.

Washambuliaji wengi wa katikati hawana uwezo mkubwa wa kumiliki wa mpira. Wengi ni wafungaji zaidi. Hiki ndicho kinachomtofautisha Mayele na wengine. Kuanzia kwa John Bocco na Meddie Kagere mpaka kwa Prince Dube. Sio wazuri wa kumiliki mpira na kujihusisha na mchezo.

Mayele anaweza asiwe mfumania nyavu mzuri kama Meddie Kagere, lakini linapokuja suala la kuhusika na mchezo hayupo wa kumsogelea.

Tazama hata washambuliaji wengi wa katikati kutoka Afrika wanaocheza Ulaya, wengi sio wazuri katika kuhusika na mchezo. Wengi ni wazuri kujitega katika nafasi na maeneo mazuri ya kufunga. Ni ngumu kuwapata hawa wanaocheza kama Mayele.

Advertisement