Tukumbuke na ile ishu ya uchawi wa Zaire kipindi kile
Muktasari:
Wapo wanaoamini kuwa uchawi ni elimu kwa maana ya taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ila tofauti ni mfumo wa mafundisho na matumizi yake ambayo hufanyika katika hali ya usiri mkubwa na masharti yake ni magumu hivyo kuifanya elimu hiyo kuwa adimu kiasi ambacho sio kila mtu kuipata.
MAELEZO mengi yamewahi kutolewa na vitabu mbalimbali vya wasomi wa kada tofauti tofauti wamewahi kuandika kuhusu suala la uchawi au kama siku hizi linavyoitwa ‘Misumari’ kwa lugha ya mtaani.
Wapo wanaoamini kuwa uchawi ni elimu kwa maana ya taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ila tofauti ni mfumo wa mafundisho na matumizi yake ambayo hufanyika katika hali ya usiri mkubwa na masharti yake ni magumu hivyo kuifanya elimu hiyo kuwa adimu kiasi ambacho sio kila mtu kuipata.
Kamusi ya Kiswahili sanifu inauelezea uchawi kuwa ni ufundi wa kutumia dawa, aghalabu mitishamba na vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe.
Tukio kubwa la kuhusishwa kwa uchawi waziwazi katika soka ya kiwango cha kimataifa ni lile la mwaka 1973 wakati Zaire ambayo siku hizi inaitwa DRC Congo iliposhiriki katika fainali za Kombe la Dunia la na kuwa nchi ya kwanza kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kushiriki katika fainali hizo zilizofanyika nchini Ujerumani Magharibi.
Kuelekea katika fainali hizo, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko aliwakusanya waganga na wachawi wote nguli kutoka katika kila jimbo la nchi hiyo, kisha aliwasafirisha wote pamoja na timu huku akiwapa jukumu maalumu la kuwaloga wazungu na kuhakikisha Zaire inarudi kutoka Ujerumani na Kombe la Dunia na kuandika historia.
Matokeo yake katika michuano hiyo hiyo Zaire ilicharazwa 2-0 na Scotland, 9-0 na Yugoslavia na 3-0 na Brazil na kurudi nyumbani na mzigo wa magoli 14 katika mechi zake tatu za makundi.
Nimezungumzia hilo kuwakumbusha tukio hilo lililotokea miaka ya nyuma. Nawakumbusha kwa kuwa matukio kama hayo yanayohusisha uchawi moja kwa moja sidhani kama yanaweza kujitokeza tena katika dunia ya soka la siku hizi ambalo ni soka la kisayansi. Endapo matukio kama hayo yatatokea basi watakaokuwa wanayasimamia pengine wanaweza kuwa na ushahidi wa kisayansi. Nimeandika hilo kwa kuwa katika mechi kadhaa za Ligi Kuu ambayo imemalizika mwezi uliopita yapo matukio ambayo binafsi yalianza kunitia wasiwasi.
Kwa mfano tukio lililotokea katika mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga la wachezaji kuondoa taulo la kujifutia jasho lililowekwa na golikipa wa Simba, Ivo Mapunda pengine lilikuwa linahitaji maelezo zaidi kwani iwapo kama hata wachezaji wenyewe wanaweza kuwa na fikra hiyo basi kumbe kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika.
Kama wachezaji wanaofanya mazoezi kila siku asubuhi na mchana kwa ajili ya maandalizi ya mechi kisha akili zao zikawa zinakinzana na misingi ya sayansi hivyo kuwafanya waamini kabisa kuwa uwepo wa kitaulo pembeni ya goli unaweza kuwafanya washindwe kufunga basi makocha wao watatakiwa kufanya kazi ya ziada katika hilo kwani mfano nilioutoa wa Zaire unatosha kabisa kuonesha mahusiano baina ya mpira na hicho kinachoitwa uchawi.
Ikumbukwe hatua tuliyopiga katika mchezo wa soka inatakiwa kwenda sambamba na urekebishwaji wa sheria na kanuni ili tuweze kwenda sambamba na wenzetu na iwapo tutayafanya haya tunayoyafanya kwenye Ligi Kuu katika mechi za kimataifa tutaishia kulalamika kuwa tunaonewa.
Hivyo rai yangu kwa mamlaka zinazosimamia soka ni kuweka sheria kali ili vitendo vitakavyooneha kulichafua soka vidhibitiwe kwa kutolewa adhabu kwani ligi yetu kwa inaonekana katika nchi mbalimbali. Naomba kuwasilisha.