Tigere Mchanganyiko wa Modric, Pogba Azam

MWAKA 2018, kiungo nyota wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia Luka Modric alivunja ufalme wa Christiano Ronaldo na Lionel Messi katika tuzo za mwanasoka bora duniani (Ballorn d’Or) na kushinda tuzo hiyo.

Modric (35) aliushangaza ulimwengu kwa kushinda tuzo hiyo katikati ya miamba miwili iliyokuwa ikipokezana tuzo hiyo tangu mwaka 2008.

Ushindi wa Modric ulichagizwa na kubeba Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara tatu mfululizo akiwa na Madrid pia kufanikiwa kuifikisha timu yake ya taifa kwenye fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

Kwa wakati ule wadau wengi wa soka hawakuwaza juu ya Modric ambaye ni kiungo huku nje ya Ronaldo na Messi wengine waliopewa nafasi ya kushinda tuzo hiyo walikuwa Antonio Greizmann, Kylian Mbape, Mohamed Salah na Raphael Varane lakini wote walitulizwa na Modric.

Sahau kuhusu Modric. Rudi Tanzania kikosi cha Azam FC utakutana na kiungo mshambuliaji mmoja jezi yake mgongoni namba 12 na juu limeandikwa jina Tigere.

Anaitwa Never Tigere raia wa Zimbambwe ambaye malengo yake makubwa ni kuwashangaza watu kwa kufanya makubwa kama aliyoyafanya Modric mwaka 2018 bila ya kutarajiwa.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na kiungo huyu ambaye amefunguka mambo kibao kuhusu safari yake ya soka binafsi:

Tigere ni kama wachezaji wengine wengi wa Kiafrika kwani historia yake ya soka imeanzia mtaani tangu mdogo na alivyokuwa Sekondari nchini kwao alizidi kucheza na kujifunza soka kwa ukubwa zaidi.

“Baada ya shule nilicheza timu tofauti tofauti za nchini kwetu kabla sijajiunga na Dongo Sawmills mwaka 2015 na nilicheza misimu miwili kisha nikahamia ZPC Kariba kabla ya kwenda FC Platinum mwaka 2018 nilikodumu hadi natua Azam katikati ya msimu uliopita.”

AL AHLY WAMLETA AZAM

Alifunguka namna mabosi wa Azam walivyomuona na kumsajili kuwa walimwona akicheza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly nchini Misri ndio wakaanza kumnyatia.

“Sikuwatafuta Azam hapo kabla bali waliniona kwenye mechi dhidi ya Al Ahly nchini kwao, kipindi hicho nilikuwa na FC Platinum na nilionyesha kiwango bora jambo lililowafanya baada ya mechi ile kutaka saini yangu,” anasema.


KWA NINI MODRIC NA POGBA

“Ni viungo wanaonivutia namna ya uchezaji wao, kingine kwa mara nyingi nimekuwa nikichukuliwa kama mchezaji wa kawaida jambo linaloniumiza roho na nataka siku moja niwaoneshe kuwa naweza kama alivyofanya Modric kwa kubeba Ballon d’Or, vile vile kwa Pogba ni kiungo ambaye anasemwa sana lakini bado anapambana na kuwaumbua wanaomsema,” anasema Tigere.


MAISHA YA BONGO

Tigere ambaye anamudu kucheza pia eneo la winga uwanjani anasema anayafurahia maisha ya Bongo na anajisikia fahari kucheza Ligi Kuu Bara akiwa katika moja ya klabu kubwa tatu za nchini hapa.

“Maisha ni mazuri kwa kweli, najivunia kuwa katika timu kubwa (Azam) ambayo ni miongoni mwa klabu kubwa za hapa Tanzania, pia nafurahi kucheza ligi yenye ushindani mkubwa namna hii. Hili ni daraja zuri kwangu kutimiza malengo niliyojiwekea,” anasema.


FAMILIA INAMPA HASIRA

Kiungo huyu ameweka wazi yeye ni Baba wa familia kwani anaishi maisha ya ndoa na mwanadada aitwaye Rhodah Moloteni raia wa Zimbabwe ambaye amemzalia watoto wawili ambao anasema wanamuongezea hasira katika upambanaji wake.

“Mke wangu na watoto ndio wananipa hasira ya kuendelea kupambana ili niwe bora zaidi na kupata mafanikio makubwa kwa ajili ya familia yetu kwa miaka ya hivi karibuni na baadae, hao watoto wangu mmoja ni wa kike na mwingine ni wa kiume,” anasema Tigere.


YEYE NA CHAPATI

“Napenda aina nyingi za vyakula vinavyopatikana hapa Tanzania lakini nadhani napenda zaidi Chapati, kivyovyote vile ukinipa chapati nafurahi sana iwe kwa chai, soda, supu au juisi kikubwa ziwe zimechomwa vizuri.”


NDOTO KUBWA

“Nina ndoto kubwa za kucheza soka sehemu bora zaidi ya hapa nilipo ila kwa sasa kila kitu nafanya kwa ajili ya kuhakikisha Azam inafikia malengo yake pia napambana kupata nafasi kwenye timu ya taifa langu ili niweze kuwa miongoni mwa wachezaji waliosaidia taifa letu,” anasema Tigere ambaye alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani na kufunga mabao mawili.


KAZI INAENDELEA

Kuhusu ubora wake ndani ya Azam na nini anawaahidi mashabiki wake na amefunguka sasa yupo fiti na atahakikisha anawapa furaha mashabiki wa timu hiyo.

“Hadi sasa nimetoa pasi nne za mabao kwa msimu huu, nadhani ni wakati sasa wa kuongeza juhudi na kuisaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea, niwatoe wasiwasi mashabiki wa Azam kwani siku nzuri zaja,” anasema.