IVERSON: Staa NBA aliyefilisiwa na matanuzi baada ya mechi

Muktasari:
- Iverson alizichezea timu kubwa za Philadelphia 76ers, Denver Nuggets, Detroit Pistons, Memphis Grizzlies na Besiktas akiwahi kukabana uwanjani na mastaa wa mchezo huo kina Shaquille O’Nea, Michael Jordan, Kobe Bryant na LeBron James na wengineo wenye majina makubwa duniani na ni kipindi alichotengeneza utajiri wa kutisha.
WASHINGTON, MAREKANI: "Nilitumia Dola 200 milioni kwa magari na sherehe, lakini sasa nimerudi kwa kishindo kupitia biashara ya Reebok ya Shaq yenye thamani ya Dola 2.5 bilioni." Ndivyo anavyoanza simulizi yake nyota wa zamani wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), Allen Iverson.
Iverson alizichezea timu kubwa za Philadelphia 76ers, Denver Nuggets, Detroit Pistons, Memphis Grizzlies na Besiktas akiwahi kukabana uwanjani na mastaa wa mchezo huo kina Shaquille O’Nea, Michael Jordan, Kobe Bryant na LeBron James na wengineo wenye majina makubwa duniani na ni kipindi alichotengeneza utajiri wa kutisha.
Kwa nyota wa NBA kama yeye ambaye aliwahi kukunja utajiri unaofikia Dola 155 milioni msimu 2010-2011 huwezi kumwambia kitu katika suala la fedha, kwani alizikamata na zikakamatika, akazifanya alivyotaka, lakini baada ya muda akiwa mstaafu akageuka mfilisi - akiomba msaada kutoka kwa wakongwe wenzake ili aweze kuendesha maisha.

Unajua ilikuwaje
Iverson aliyeng'ara katika kikapu kati ya 1996 hadi 2011, aliondoka akiwa bilionea katika mchezo huo ndani ya miaka 17, lakini maisha ya anasa yalimfanya kutumia pesa zote alizovuna na kisha kumrejesha katika umasikini wa kutupwa.
Bahati nzuri, alipata msaada na sasa anajenga maisha upya — kwa msaada wa Shaquille O’Neal. Mwaka 2012, gazeti la The Washington Post liliripoti kuwa Iverson, mmoja wa wachezaji bora katika historia ya NBA ambaye hakuwahi kushinda ubingwa, alimwambia mkewe wa wakati huo, Tawanna Turner, kuwa hakuwa na uwezo hata wa kununua andazi wakati wa mchakato wa talaka. Mwaka huohuo, alifungua kesi mahakamani kuomba atangazwe kuwa amefilisika.
Ikiwa ni pamoja na matangazo na udhamini, Iverson inadaiwa kwamba enzi zake aliwahi kuvuna utajiri wa zaidi ya Dola 200 milioni. Hata hivyo tabia ya kutumia zaidi fedha kuliko alichokuwa akiingiza baada ya kustaafu ilimponza. Akafilisika. Na ni wakati ambao hakuwahi kuwekeza vya kutosha katika shughuli za kibiashara kama mastaa wenzake wa kipindi hicho ambao kwa sasa wanaogelea katika utajiri mkubwa.
Inaelezwa kwamba nyota huyo wa zamani wa Denver Nuggets alikuwa na mkusanyiko wa magari ya kifahari, likiwemo Lamborghini Murcielago, Mercedes Maybach 57S na Bentley Continental GT. Mwaka 1998 aliwahi kumpa Bentley mchezaji chipukizi wa Philadelphia 76ers, Larry Hughes.
Iverson aliandika makala moja katika mtandao wa Players' Tribune: “Larry alisimama pale, akiwa kama yuko ndotoni. Anaangalia ile Bentley… ananiangalia mimi… halafu akasema, ‘Yo… AI. Lazima nipate moja kama hii. Sikufikiria hata mara mbili. Nikamwambia, ‘Bro, chukua gari yangu.”

Cha kuchekesha, tanki la Bentley hiyo lilikuwa tupu bila mafuta na kumwacha Larry amekwama Magharibi mwa mji wa Philadelphia kwa saa kadhaa na hadi leo anaamini lilikuwa tukio la utani wa kumkaribisha katika timu hiyo aliyokuwa akichezea Iverson.
Larry ambaye pia aliwahi kucheza na LeBron James na Michael Jordan, alisimulia alivyokutana na Iverson kwa mara ya kwanza alipokuwa chipukizi akisema: “Nilipojiunga na ligi kulikuwa na mgomo (wa wachezaji kutocheza). Kwa hiyo hatukupata mishahara NBA, lakini kama ulikuwa na matangazo ya biashara hayo yaliendelea.
"Siku moja nilienda benki nikatoa pesa kidogo kwenye ATM. Lakini nilipoenda benki na Allen Iverson yeye hakwenda ATM wala hakuongea na mhudumu wa benki. Aliingia moja kwa moja kwenye chumba cha kuhifadhia pesa. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona mtu mwenye pesa nyingi namna ile. Walimpa pesa zake zikiwa bado zimefungwa kwenye plastiki.”
Iverson, aliyewahi pia kuichezea Detroit Pistons na Memphis Grizzlies alikuwa mtu wa kutoa misaada sana na runinga ya Fox Sports ilidai aliwahi kuwa na kundi la takriban watu 50 waliokuwa wakiishi kutokana na kipato chake.

VIWALO, VITO VYA THAMANI
Mapenzi ya Iverson kuvaa mavazi ya kifahari na vito vya thamani vilichangia matatizo yake ya kifedha, na mchezaji mwenzake wa zamani Philadelphia 76ers, Matt Barnes aliwahi kuiambia Sports Illustrated kwamba Iverson alikuwa na kawaida ya kutumia maelfu ya dola kwenye vilabu vya burudani nyakati za usiku.
“Kila tukienda (kilabu) alikuwa anawarushia watu na mashabiki Dola 30,000 hadi 40,000,” anasema Barnes.
“Nikamwambia, ‘unajua mimi ningeweza kufanya nini na pesa hizi?’” Bahati nzuri, Iverson aliyewahi kumuacha Shaquille bila la kusema alipomtaja katika kikosi chake cha wachezaji bora wa muda wote amefanikiwa kurekebisha hali yake.
“Sikuwa na mpango. Nilikuwa na miaka 21. Nilikuwa naishi kwa uamuzi wa papo hapo. Sikuwa nimewahi kuwa na pesa kabla maishani mwangu,” anasema Iverson akijutia kwa alichofanya hadi akafilisika.
Na sasa nyota huyo wa zamani ameanza maisha upya akifanya kazi ya kuajiriwa na Shaquille O’Neal kupitia kapuni yake ya Authentic Brands Group (ABG) inayomiliki sehemu ya hisa ya kampuni kubwa ya mavazi na viatu ya Reebok. Iverson amepewa

mkataba wa maisha na Shaquille unaomlipa Dola 800,000 kila mwaka na atapata pensheni ya Dola 32 milioni atakapofikisha umri miaka 55 ndani ya miaka sita ijayo.
Mwaka jana, alijiunga na kampuni hiyo ya vifaa vya michezo kama makamu wa rais wa kitengo cha mpira wa kikapu.
Iverson kutokana na ajira aliyonayo kwa sasa anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola 1 milioni ingawa ni mdogo sana ukilinganisha na aliokuwa nao zamani lakini mambo yanamwendea vizuri mwanamichezo huyo mwenye kipaji na ambaye amekubali kuwa mjasiriamali.
Reebok, iliyouzwa kwa Dola 2.5 bilioni kwa Authentic Brands Group 2021 hivi sasa imezindua viatu vya gofu maarufu aina ya Nano Golf vinavyovaliwa na staa wa LIV Golf, Bryson DeChambeau. "Ni heshima kuiongoza Reebok kurudi kwenye mchezo wa gofu kwa uzinduzi wa Nano Golf kiatu cha gofu chenye ubora wa hali ya juu na kinachochanganya ubunifu na mtindo mpya kwa ajili ya kuvutia wanamichezo wapya," anasema DeChambeau.
Viatu vya Question Golf vinavyouzwa kwa Dola 180, ni heshima kwa Iverson na muundo wake maarufu unaofahamika kama Question ambavyo hivi sasa vimekuwa vikivaliwa na mastaa kibao wa NBA.

BOSI WAKE GWIJI NBA
Akizungumza hivi karibuni, Shaquille anasema ameamua kumsitiri Iverson kwa sababu maisha siku zote hayapo sawa duniani.
Ubunifu wa watu aliowaajiri katika kapuni hiyo akiwamo Iverson ni katika juhudi zake za kulitawala soko la viatu na kufufua chapa ya mpira wa kikapu kupitia Reebok.
“Nimesema siku zote kwamba Reebok haikuwa namba moja, lakini pia haikuwa namba tatu,” anasema Shaquille na kuongeza:
“Nakumbuka niliposaini Reebok ilikuwa kampuni inayoibukia. Tukamsainisha mkataba Allen Iverson na Shawn Kemp, na tulikuwa sehemu ya washindani. Awali Adidas waliinunua Reebok, ikapotea sokoni. Iliporudishwa sokoni mshirika wangu Jamie Salter akanunua kampuni hiyo na kwangu ni changamoto kuirudisha tena kwenye nafasi ya heshima.
"Ni jambo la kufurahisha, imenilazimu kujifunza mengi.”