Tambwe ataja 'uchawi' wa kutupia nyavuni

Muktasari:
- Tambwe ana rekodi nyingi kwenye soka ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmmoja, hat trick nyingi akifunga sita ndani ya misimu minne, lakini pia ndiye aliyekuwa mkali wa vichwa Bara tangu alipojiunga nayo hadi anastaafu.
UKITAJA washambuliaji watatu bora wa kigeni katika miaka ya hivi karibuni kwenye Ligi Kuu Bara huwezi kusita kulitaja jina la Amissi Tambwe ambaye amestaafu kucheza mpira, na kuibukia kwenye umeneja katika timu aliyowahi kuitumikia miaka ya nyuma, Singida Black Stars.
Tambwe ana rekodi nyingi kwenye soka ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmmoja, hat trick nyingi akifunga sita ndani ya misimu minne, lakini pia ndiye aliyekuwa mkali wa vichwa Bara tangu alipojiunga nayo hadi anastaafu.
Mwanaspoti limefanya naye mahojiano akazungumza mambo kibao ukiwamo mpango wake wa kurudi darasani kusomea ukocha ambao anakiri kuwa ni kazi ambayo ameshawishika zaidi baada ya kukaa benchi la ufundi akiwa meneja.

AGEUKIA UKOCHA
Wakati mambo yakimnyookea akiwa meneja, nyota huyo mwenye rekodi tamu Bara anasema yupo mbioni kusomea leseni C ya ukocha.
“Nina leseni D na hivi karibuni narudi darasani kusoma C hivyo tayari nipo darasani najifunza kwa vitendo kabla ya kurudi darasani, nafurahi napata vitu vingi kutokana na makocha waliopo. Mchezaji unatakiwa kuwa na kitu cha kujifunza hasa ukiwa unacheza maelekezo unayopewa kipindi ukiwa mchezaji, unatakiwa kuyahifadhi ili siku ukipata nafasi ya kusomea kozi hiyo unakuwa na sehemu ya kuanzia,” anasema Tambwe.
“Sasa nipo katika benchi kama meneja, lakini nina faida ya kuwa na uelewa wa ukocha. Kuna msaada mkubwa kuwepo benchi kwa sababu nimecheza mpira na nimeamua kufanya kazi hii, hivyo natoa hamasa kwa wachezaji kuhakikisha wanatamani kufanya makubwa niliyoyafanya.
“Wachezaji wa zamani kukaa benchi wanatoa motisha kwa wachezaji. Wanaheshimu kile ulichofanya, hivyo na wao wanapambana kuhakikisha wanafanya kitu kwa ukubwa ili kufikia malengo. Hata nikipata nafasi ya kumuelekeza (mchezaji) anaelewa vizuri kwani anajua nini nimekifanya.”
SIRI HAT TRICK SITA
Tambwe ana rekodi ya kufunga hat trick sita katika misimu minne aliyocheza hapa nchini - akifunga mbili kwa misimu mitatu mfululizo na mwenyewe anaeleza siri ya mafanikio hayo ambayo bado hayajafikiwa na mchezaji yeyote hivi karibuni.
“Kujituma, kuzingatia nini unaelekezwa na mwalimu. Nakumbuka kuna mwalimu wangu wa timu ya taifa aliniambia ukiwa kwenye boksi unatakiwa kutulia, kutumia akili na kupiga mpira bila kutumia nguvu. Kauli hiyo ilinijenga sana,” anasema mkongwe huyo.
“Nikiwa kwenye boksi nilikuwa natuliza akili na ilikuwa lazima nimeze mate. Hutakiwi kupiga shuti kubwa, unamuangalia kipa kakaa vipi unapiga mpira kwa akili na sio kutumia nguvu. Nafikiri hayo mambo ndio yalikuwa yananibeba sana na kunipa mafanikio hayo unayoyazungumza sasa.”
Tambwe anasema mbali na hivyo, pia alikuwa muumini wa mazoezi binafsi baada ya mechi kwani alirudi na kufanya kile ambacho alishindwa kukifanyia kazi kwenye mchezo, husika na alikuwa amepewa maelekezo na kocha.
“Nikiona uwanjani sijafanyia kazi kile ambacho kocha alinisisitiza kukifanya au sijatumika kwenye mchezo husika nilikuwa na tabia ya kurudi uwanjani na kufanya mazoezi binafsi.”

SIRI YA KUVIZIA
Mkali huyo wa kutupia mabao wengi wamekuwa wakizungumza kuwa alikuwa mviziaji na si mchezaji wa kutafuta mipira kama washambuliaji wengi wanavyofanya, na hapa anazungumzia hilo akisema sio kuvizia, bali kuwa na mikakati bora ambayo ilikuwa ikimfanya awe bora eneo la ushambuliaji.
“Sio kuvizia, kitu ninachoweza kusema kuchezesha kichwa nafahamu sana na nilikuwa na tabia ya kuusoma uelekeo wa mpira na kujiandaa nini nikifanye kuhakikisha unatua eneo nilipo na ndicho kilikuwa kinanibeba sana,” anasema Tambwe.
“Mabeki wengi mara nyingi wana tabia ya kusubiri mpira, ukiwa mshambuliaji wa kupita haraka mbele yao lazima utawaadhibu sana na ndicho nilichokuwa nakifanya, nikiona mpira nacheza na akili ya beki na kuufikia haraka mpira.
“Nasimama nikiuona mpira namna unavyokuja najua namna ya kuuwahi sio kuvizia. Mimi nikiwa nyuma nauona mpira, hivyo nakimbia haraka nikiamini nitaufikia akili yangu ilikuwa inacheza vizuri, naufikia kama ambavyo nilikadiria.”
Tambwe anasema mabeki wengi kwenye nchi alizocheza wana tabia ya kutokuwa makini, hivyo alikuwa anautumia udhaifu wao kuziadhibu timu nyingi na hiyo ndio ilikuwa siri kubwa ya mafanikio yake Bara hasa kupachika mabao.

MASTRAIKA KUSTAAFU HARAKA
Ni nadra sana kuona washambuliaji wakidumu kwenye soka miaka mingi kama ilivyo kwa makipa na mabeki na nyota huyo aliyecheza nafasi hiyo ameeleza sababu za wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kustaafu mapema kuwa ni kutokana na ukatili wanaofanyiwa na mabeki.
“Ukiwa mshambuliaji muoga huwezi kucheza mpira muda mrefu kwa sababu tunakutana na mabeki wakatili ambao soka lao ni la kijeshi. Kazi yao ni kutukata sana. Ili uwe mshambuliaji bora ni lazima kutumia akili ili kukwepa shida hiyo,” anasema.
“Beki hana sifa nzuri, kazi yake kama yupo jeshini ana roho ya tofauti sana. Wanatuchosha sana na kutunyima furaha uwanjani. Mimi nilikuwa napenda kukutana na beki ambaye hana akili anayetumia nguvu kuliko akili kwa sababu ni rahisi kumtoka na kumfunga tofauti na yule ambaye anatumia akili.”
KUNA YONDANI MMOJA TU
Licha ya kucheza kwa mafanikio akitumikia timu tofauti akicheza Ligi Kuu Bara na Championship, mshambuliaji huyo wa zamani tishio anamtaja beki wa KenGold ambaye zamani aliitumikia Simba na Yanga, Kelvin Yondani kuwa ndio beki tishio ambaye amekamilika kila eneo, kukaba na kutengeneza mashambulizi.
“Yondani ana akili ya mpira. Ni beki ambaye hatumii nguvu sana na mbali na kuzuia ni mchezaji ambaye anajua sana kutengeneza mashambulizi. Mbali na kunikaba kwa akili nimefurahia kucheza naye kwa sababu alikuwa ananitengenezea nafasi,” anasema na kuongeza:
“Ukicheza na beki ambaye hana akili anatumia nguvu sana lazima ufunge. Wakati nipo Simba na Yanga timu nyingi nimezifunga sana kwa sababu unampita (beki) na kumuacha kutokana na kutokaa karibu yake.
“Timu ndogo nimezifunga kubwa Simba, Yanga na Azam FC pia nimezifunga. Hii ni kutokana na kucheza na akili ya beki ambaye anatumia nguvu sana na sio akili, na ndio maana naamini Yondani alikuwa bora kumpita lazima uumize kichwa.”
Tambwe anasema mara ya kwanza aliposajiliwa Yanga hakumbuki kama kuna timu hakuwahi kutoifunga kutokana na namna alivyotumia sana nafasi hasa mipira ya juu ya vichwa ambayo anadai kuwa ni mwepesi kuchezesha kichwa ili kutupia nyavuni.

KUNA WAAMUZI WAZINGUAJI
Wadau mbalimbali wa soka nchini wamegawanyika kuhusu makosa yanayojirudia ya waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Bara, tatizo lililomuibua meneja huyo wa Singida Black Stars ambaye anasema anatambua kuwa na wao ni binadamu, hivyo kupitiwa ni jambo la kawaida, lakini makosa yao yamekuwa mengi.
“Mwamuzi kama anakuja na mipango yake uwanjani unaamua kumuachia Mungu na kuhakikisha unaiandaa timu kupambana ili iweze kupata matokeo kwa njia ya uhalali bila kutegemea makosa madogomadogo kama penalti,” anasema Tambwe.
“Mwamuzi ni binadamu, lakini makosa yanazidi (Ligi Kuu). Nazungumzia mechi yetu dhidi ya Simba (ile ya mwisho ya ligi baina ya timu hizo) kulikuwa na penalti zaidi ya tatu, kweli alishindwa kuona hata moja? Sisi tumemuachia Mungu. Tunafuraha tulisawazisha makosa, tumewatoa (Simba) hatua ya nusu fainali na tumetinga fainali.”
Tambwe anasema kitu kikubwa ambacho wanapambana ni kujenga kikosi bora cha ushindani ambacho hakitacheza zaidi na uamuzi wa mwamuzi zaidi ya soka la ushindani ambalo litawapa matokeo halali.
TIMU BORA NI BENCHI
Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), lilitangaza Ligi Kuu Bara kuwa ya nne kwa ubora Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024 ikipanda kwa nafasi mbili kutoka ya sita 2023 ikizipiku bora kama Afrika Kusini na Tunisia.
Tambwe anaungana na IFFHS akikiri kuwa Ligi Kuu Bara inakua siku hadi siku na ndio maana wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakija kwa wingi kucheza soka. “CAF imepitisha ubora wa ligi ya Tanzania kuwa namba nne kwa ubora ni sahihi kwa sababu inakua na viwango vinaongezeka. Ni sahihi kuwa kwenye nafasi hiyo na naamini kama mambo yataendelea hivi ubora utakuwa ukiongezeka kila mwaka,” anasema.
“Ubora wa ligi unatokana na uwekezaji ulivyo. Kama timu inaweza kusajili nyota bora kutoka mataifa makubwa na wakaja kucheza ligi na kuonyesha ushindani, ni lazima viwango vikue na wachezaji wengine wengi wakubwa watatamani kuja kucheza.
“Ukiangalia hivi karibuni Tanzania inaendelea kuongoza mataifa mengine mengi kwa wachezaji kutoka mbali kuja kucheza mpira huku, tofauti na zamani kulikuwa na Rwanda, Kenya na mataifa mengine ya karibu kama DR Congo.”